Tulinde hifadhi za mazingira asilia kuipaishaTanzania kitalii

12Jun 2016
Beatrice Bandawe
Nipashe Jumapili
Tuzungumze kidogo
Tulinde hifadhi za mazingira asilia kuipaishaTanzania kitalii

MWAKA 2010 Tanzania ilikuwa inashika nafasi ya pili kati ya mataifa 141 duniani yenye vivutio vya uhifadhi wa mazingira asilia ya kitalii, ikitanguliwa na nchi ya Brazil.

Lakini kwa mujibu wa ripoti ya utalii ya mwaka 2015, Tanzania imeporomoka na kushika nafasi ya saba.

Vivutio vya Tanzania vilivyoshindanishwa katika mashindano hayo ni Mlima Kilimanjaro, Bonde la Ngorongoro na Hifadhi ya Serengeti.

Ripoti hiyo ambayo hutolewa kila baada ya miaka miwili, inafafanua utendaji na ufanisi wa nchi 141 katika ushindani wa sekta ya utalii wa asili.

Utalii ni tegemeo la nchi nyingi kama njia kuu ya kuinua pato la nchi, kukua kwa uchumi katika njia bora endelevu na kutoa ajira.

Baadhi ya matukio yanayosababisha nchi kukosa watalii kwa wingi ni pamoja na matishio ya Al-shabab na magonjwa ya milipuko kama Ebola, hasa kwa nchi za Afrika.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo baadhi ya mambo muhimu yanayochangia watalii kuingia kwa wingi nchini kuangalia vivutio vya utalii, ni nchi kuwa na mazingira mazuri ya ulinzi na usalama, kibiashara, afya na usafi, rasilimali watu na kazi, miundombinu ya barabara na bandari, miundombinu ya huduma za kitalii, rasilimali za asili, urithi wa kitamaduni na safari za kibiashara na ushindani wa kibiashara.

Sekta ya utalii nchini inachangia asilimia 17.5 ya mapato ya ndani. Kwa mwaka jana watalii milioni 1.1 waliingia nchini na mapato ya kigeni yalikuwa Sh. bilioni 2.

Kama kasi ya watalii wa kimataifa itaendelea kuongezeka, basi Tanzania itakuwa katika nafasi nzuri ya kuongeza pato lake la ndani kupitia sekta ya utalii.

Idadi ya watalii wanaoingia nchini inatokana na mifumo ya ekolojia inayowavutia watalii na wengi wanaoingia Tanzania wanatoka nchini Marekani, kuja kuangalia vivutio vya asili ambavyo nchini kwao havipo.

Vivutio hivyo ni pamoja na wanyama, utamaduni, vyakula, mavazi na rasilimali za asili.

Hata hivyo, pamoja na kuwa na vivutio vyote hivyo, idadi ya watalii wanaoingia nchini kulinganisha na nchi ambazo hazina vivutio kama vilivyopo Tanzania, ni ndogo.

Afya na usafi ni mambo muhimu katika kuzingatia ushindani wa utalii. Ni lazima watalii wanapoingia katika nchi yoyote, wahakikishiwe usalama wa maji safi na salama.

Inapotokea mtalii anaugua, sekta ya afya kwenye nchi lazima ihakikishe anahudumiwa ipasavyo kwa kupelekwa hospitali bora na kupata huduma kutoka kwa madaktari wazuri.

Tatizo la kuongezeka kwa idadi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwenye nchi, linaweza kuwa sababu ya kuwavunja moyo watalii kutembelea nchi yako.

Ulinzi na usalama kama haupo vizuri ni sababu kubwa itakayofanya nchi kushindwa katika sekta ya utalii. Watalii hawako tayari kwenda kwenye nchi ambayo usalama wao si wa uhakika.

Hapa inazungumziwa uporaji, vurugu na ugaidi na polisi wamekuwa tegemeo kubwa la ulinzi wao.

Matukio yasiyo ya kiusalama kama watalii kuporwa mali zao wawapo nchini ni baadhi ya vitu vinavyochangia nchi kukosa watalii na fedha za kigeni katika nchi yetu.

Njia nyingine ya kuongeza idadi ya watalii ni jinsi watalii watakavyoweza kupata huduma kupitia mitandao.

Kwa mfano kutumia mtandao wa intanet kupata taarifa mbalimbali kuhusu nchi wanayotaka kutembelea. Kwa njia hiyo pia huwasaidia kutafuta hoteli wanayoweza kumudu kwa ajili ya malazi na chakula, upatikanaji wa huduma ya mtandao wa simu, huduma ya umeme wa uhakika na uwezo wa kibiashara kwa mtu mmoja mmoja wa kutumia mtandao.

Sababu nyingine inayoelezwa ya kutopata watalii wengi ni pamoja na kutokuwa na miundombinu rafiki, ikiwamo ya barabara.

Aidha, huduma mbaya inayotolewa na baadhi ya wafanyakazi wanaohudumia watalii na kutokuwa na lugha ya ukarimu inakayomvutia mteja kurudi mara ya pili au kumshawishi mwenzake kuja kutembelea nchi yako.

Watalii wanapofika kwenye nchi yoyote hutarajia kukuta upatikanaji wa usafiri wa uhakika wa kuwapeleka kwenye vivutio vya utalii. Hivyo, kuna umuhimu wa kuwa na barabara nzuri, njia za reli na miundombinu mizuri ya bandari inayoendana na viwango vya kimataifa, ikiwamo usalama.

Kuna vigezo vingi vinavyochangia watalii kuvutiwa kuja nchini kwako yakiwemo matango yanayohamisha vivutio vyako.

Nchi yako hata ikiwa na vivutio vingi, kama havitatangazwa hakuna mtu atakaye vijua. Hivyo kuna umuhimu wa Watanzania kuitangaza nchi yao, iwe kwa mtu mmoja mmoja anayepata fursa ya kutoka nje ya nchi yake, taasisi, serikali ili watalii wengi wa kimataifa waweze kuja kuangalia vivutio vyetu.

[email protected]; Simu: 0774 466571