Tumieni fursa hii kujipima dengue

04Jul 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tumieni fursa hii kujipima dengue

MEI mwaka huu, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dk. Yudas Ndugile, aliwataka wakazi wa jijini kuchukua tahadhari kipindi cha mvua kwa kusafisha mitaro na maeneo yanayowazunguka, ili kujiepusha na ugonjwa wa dengue.

Dk. Ndugile anasisitiza juu ya uvaaji wa mavazi marefu yanayoziba sehemu ya mikono na miguu ili kuwaepusha na maambukizi ya ugonjwa huo unaoletwa na vimelea vinavyosambazwa na mbu aina ya Aedes Egyptae.

Kwa mujibu wa Dk. Ndugulile, mbu huyo hupendelea kuishi karibu na makazi ya watu na huweza kuuma binadamu mchana na usiku, hatimaye kumsababisha ugonjwa huo.

Mbali na hayo, anawataka wananchi kuwahi katika vituo vya afya mapema pale wanapohisi dalili za ugonjwa huo, badala ya kunywa dawa kiholela, hali ambayo inaweza kuwaletea madhara zaidi.

Dalili za ugonjwa huo zimeshawekwa wazi kuwa ni homa kali ya ghafla, maumivu makali ya kichwa, macho kuuma, maumivu ya viungo, kichefuchefu, kutapika, vipele ambavyo hutokea siku nne baada ya homa kuanza na kutoka damu puani, kwenye fizi na kuchubuka kirahisi.

Nikirejea kwenye hoja ni kwamba serikali imeamua kutolewa bure vipimo vya ugonjwa huo kwenye vituo vya afya vya umma ili kupambana nao usiendelee imepoteza maisha ya Watanzania.

Lakini kama kawaida ya baadhi ya Watanzania, inawezekana baadhi wakazembea kutumia fursa hiyo ya kwenda kwenye vituo hivyo ili kupima ugonjwa huo wanapobaini dalili zake.

Kwa kuwa serikali imeshatangaza kwamba vipimo vya ugonjwa huo ni bure, basi kila mmoja hana budi kuchukua hatua ya kwenda kwenye kituo cha afya cha umma kuliko kuzembea na kujikuta akipoteza maisha.

Inaelezwa kuwa mara nyingi dalili huwa sio kali na wengi hudhani ni homa ya mafua au maambikizi mengine ya virusi na kwamba dalili hizo huanza kutokea baada ya wiki mbili, lakini kwa wengi huchukua wiki moja ya kwanza na tayari ataanza kuona dalili za dengue.

Lakini kwa sababu tayari kila kitu kimeshaweka wazi, sidhani kwamba kuna haja ya kuzembea kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakizembea  hata kwenye ugonjwa wa kipindupindu.

Kwa mfano kwenye suala la kujikinga na ugonjwa wa kipindupindu, watu wamekuwa wakihimizwa kuzingatia usafi ili kuepuka ugonjwa, lakini baadhi yao hawako makini.

Unaweza kukuta wakitiririsha majitaka mitaani, kutochemsha maji ya kunywa au kwa ujumla wake kutozingatia kanuni za afya na kusababisha ugonjwa huo kuendelea kuwanyemelea.

Inawezekana ni kutokana na kutozingatia maelekezo ya wataalamu wa afya au kutojua chochote, lakini jambo la msingi hapa ni kuwa makini kwa kufuata kile kinachoelekezwa.

Wakati mwingine inawezekana hata uamuzi uliochukuliwa na serikali wa kupima watu bure homa ya dengue ukawapita wengine ndio maana nikasema hiyo fursa ichangamkiwe.

Mtindo wa kuzembea mambo ya msingi haupaswi kupewa nafasi. Hili suala la homa ya dengue wasiwapo watu kuzembea pale wanapohisi kuwa na dalili za homa hiyo wakajikuta kwenye hatari ya kupoteza maisha.

Hii ndio inanifanya niwakumbushe kuwa serikali imeshaamua kutoa bure vipimo vya homa ya dengue, hivyo ni vyema fursa hiyo isipite bure bali waitumie ili kujihakikishia usalama wa afya zao.

Kama alivyosema bungeni hivi karibuni, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu aliweka wazi kuwa mbali na kutoa vipimo bure, wizara imeshanunua lita 60,000 za viua vidudu.

Kwamba lita hizo zimesambazwa kwenye mlipuko wa ugonjwa huo ikiwamo halmashauri tano za Mkoa wa Dar es Salaam, Geita, Kagera, Kigoma, Lindi, Mtwara, Pwani, Morogoro, Tanga na Singida.

Aidha, anasema serikali imeshaagiza mashine kubwa sita kwa ajili ya kupulizia mbu, ambazo zinatarajiwa kufikishwa nchini mwishoni mwezi huu.

Pamoja na hayo suala la msingi ni kwamba hatua ya kuruhusu watu kupimwa bure homa ya dengue ni ya msingi hasa kutokana na hali ya wengi wao kiuchumi siyo hivyo ni muhimu kuchangia fursa hiyo ya kupmwa bure.

Kila mmoja akizingatia kile kinachoelezwa na wataalamu wa afya kujikinga na ugonjwa huo na pia kwenda kwenye vituo vya afya, mapambano dhidi ya dengue yanaweza kuwa na mafanikio makubwa.