Tuna mengi ya kujifunza kutoka ziara ya Wavietnam nchini

15Mar 2016
Gwamaka Alipipi
Nipashe
Mjadala
Tuna mengi ya kujifunza kutoka ziara ya Wavietnam nchini

MGENI njoo mwenyeji apone. Ni msemo uliozoeleka katika jamii yetu wenye maana pana, endapo tu mwenyeji mwenyewe akiwa na dhamira ya dhati kumsikiliza mgeni wake amekuja kufanya nini au amemletea nini.

Wiki iliyopita Tanzania ilimepokea ugeni mzito kutoka bara la Asia, wa ziara ya Rais wa Vietnam akiongozana na mawaziri wake watano wa fedha na utawala, pamoja na wafanyabiashara 51.

Hakika ninaweza kusema ni ugeni mkubwa tulioupokea kwa wenzetu hawa walioendelea katika sekta ya viwanda, kilimo na biashara, ukizingatia serikali ya awamu ya tano imejidhatiti kuwa Tanzania itakuwa ni ya viwanda.

Vietnam yenye idadi ya watu milioni 91.7 imepiga hatua kubwa katika kilimo cha korosho, mpunga na ufugaji wa samaki, mbegu za mazao hayo yote na samaki walichukua kwetu katika miaka ya 1970.

Unashangaa! Ndiyo, Vietnam hawa tuliowapokea, walikuja nchini miaka hiyo na kuondoka na mbegu za korosho na mpunga, kisha kuchukua watoto wa samaki katika ziwa Victoria na kwenda nao kwao kuwafuga, lakini miaka ya sasa wameendelea kiuchumi na ni nchi ya pili duniani kwa ufugaji wa samaki na kilimo cha mazao hayo.

Leo wamerudi Tanzania kuja kutufundisha namna bora ya kufuga samaki, namna ya kulima korosho na mpunga, hakika ni maajabu.

Wamekuja kutufundisha sisi Watanzania masuala ya kibiashara katika sekta mbalimbali kama vile, benki, uchumi na fedha, mafuta na gesi, ujenzi na majengo, posta na mawasiliano, teknolojia ya habari, umeme na elektroniki, samani, utalii, kilimo na usindikaji, chakula na vinywaji, dawa, nguo na viatu.

Tusione aibu kujifunza kutoka kwao ili nasi tuwe bora hata kama walichukua vitu hivyo kwetu, inatupasa tuwasilikize na tuwe wapole kama wanafunzi darasani wakimsikiliza mwalimu.

Ujio wa Wavietnam hawa umeshafungua milango ya kibiashara baina ya wafanyabiashara nchini kupitia Taasisi ya Sekta binafsi nchini (TPSF) na Baraza la wafanyabiashara na Viwanda wa Vietnam (VCCI).

Rais wa Vietnam, Truong Tan Sang, alipokuwa nchini katika ziara yake ya siku nne, alieleza kuwa Vietnam itashirikiana na Tanzania katika kukuza na kuendeleza sekta ya viwanda na kilimo, na kwamba Tanzania ina fursa nyingi za kuendeleza uchumi wake kupitia viwanda.

Kwa kudhihirisha hilo, VICC na TPSF walisaini mkataba wa makubaliano utakaofungua njia za kushirikiana kibiashara, mawasiliano, uwekezaji na uchumi kati yao; na kwa Tanzania iliwakilishwa na Mwenyekiti wa TPSF, Dk. Reginald Mengi.

Ni jukumu la serikali ya awamu ya tano kuhakikisha wageni hawa wanapoondoka basi nasi tunabaki na kitu tulichojifunza kutoka kwao, siyo baada ya kukaa na kucheka nao na kuwaonyesha mandhari ya nchi.

Ninampongeza Rais. Dk. John Magufuli alipotoa agizo kwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba kwenda nchini Vietnam mara moja kabla ya yeye hajakwenda, wakajifunze namna gani nchi hiyo ilivyopiga hatua ya kimaendeleo kupitia kilimo na biashara.

Ninaimani wakienda huko watajifunza na kuchukua ujuzi na kurudi nao Tanzania, na miaka kadhaa ijayo Tanzania nasi tutakuwa kama wao, itakuwa Tanzania ya kilimo bora na yenye maendeleo ya viwanda.

Hofu yangu na wasiwasi wangu kwa mawaziri hawa wasije wakaenda huko Vietnam badala ya kujifunza wakaanza kufanya mambo mengine, tungependa kuona wanarudi nchini na kuwaelimisha wakulima wa korosho kule Mtwara na wakulima wa mpunga kule Kyela mbinu bora za kilimo ili nchi hii iende kwa kasi ya ‘Hapa Kazi tu.’

Kitu kingine cha msingi sana ni kwamna Mwijage na Mwigulu sio wataalamu, bali ni wanasiasa, hivyo, sina uhakika kama watakwenda Vietman na kurudi na utaalamu huo kisha kuwafundisha Watanzania.

Binafsi nashauri kwamba kama kweli serikali ina dhamira ya kujifunza kutoka Vietman, basi itume wataalamu watakaoleta mbinu hizo nchini na siyo Mwijage na Mwigulu, ambao kazi yao ni wanasiasa.