Tunahitaji sauti moja kukabiliana na nimonia

07Mar 2021
Joseph Kulangwa
Nipashe Jumapili
MADONGO YA MGAGAGIGIKOKO
Tunahitaji sauti moja kukabiliana na nimonia

DUNIA inapitia kipindi kigumu sana kiafya kwa sasa. Wakati ikipambana na ugonjwa wa COVID -19, sisi Tanzania tunapamba na nimonia ambayo inaonekana kutuathiri vibaya kimaisha.

Mwaka jana, Tanzania tulipambana sana na COVID-19 lakini kwa maombi yaliyosikika na Mwenyezi Mungu tuliitokomeza na kuishi maisha tofauti na mataifa mengine, ambayo yaliendelea kuteseka.

Lakini wakati mataifa hayo mwaka huu yakilalamika kukumbana na aina mpya ya virusi vya korona, sisi tukajikuta tunaingia katika wimbi la maambukizi ya nimonia, ambayo inasababisha changamoto za upumuaji.

Nimonia hii imetupokonya wapendwa wetu, huku dalili zake zikifanana kabisa na za COVID-19 na mbinu zake za kujikinga zikifanana pia, katika kuvaa barakoa, kutumia vitakatishi, kunawa maji tiririka na sabuni na kujiepusha na misongamano.

Inaonekana kila mwaka kutakuwa na ugonjwa mpya kwani baada ya Corona sasa tuna nimonia, hatujui mwaka ujao tutakuwa na ugonjwa gani. Baadhi ya wataalamu wanasema nimonia hii inatokana na mabadiliko ya hali ya hewa, ambayo hutokea nyakati hizi kila mwaka.

Lakini kinachoonekana ni tofauti, kuwa nimonia ya miaka iliyopita haikuwa kali kama hii ya mwaka huu na kushabihiana na Corona, ndiyo sababu hata baadhi ya watu wakiwamo wanasiasa, hawataki kabisa nimonia hii iitwe Corona, kwa sababu ni magonjwa tofauti, ingawa yanashabihiana.

Hata baadhi ya wataalamu wetu wa tiba nao wanamsimamo huo huo, hivyo Watanzania kukosa budi kuwaamini kwa kuwa katika fani hiyo, wao ndio Alfa na Omega. Bora waachwe waendelee kupambana na nimonia mpaka tuitokomeze kama tulivyofanikiwa kwenye Corona.

Pengine tofauti na mwaka jana kwenye mapambano dhidi ya COVID-19, mwaka huu dhidi ya Nimonia, karibu kila mtu anapambana kivyake. Imekosekana sauti ya pamoja kama tulivyozoea Watanzania katika kuhamasisha mapambano. Rejea mwaka jana kwenye Corona, rejea miaka ya sabini kwenye Vita vya Kagera.

Leo kwenye nimonia, kila mtu anasema lake, kila mtu anashauri lake, waganga wa jadi ni wengi, wataalamu wa tiba ni wengi, dawa za kukabiliana na Nimonia ni nyingi tena za aina mbalimbali, kila taasisi ina dawa yake, fomula na bei yake.

Wakati wataalamu wa tiba wanakuja na dawa za kisasa, wa asili wameshikilia nyungu-kujifukiza; wanasiasa nao wamekumbatia nyungu, kiasi kwamba wapo wanaopendekeza kila hospitali iwe na chumba maalumu cha kujifukizia.

Wakati hilo likiendelea, baadhi ya wataalamu wanasema kujifukiza kuna athari mbaya kwenye mapafu, lakini waliojifukiza wanasema nyungu imewaondolea nimonia.

Juhudi za Rais John Magufuli kujenga hospitali, zahanati na vituo vya afya nchi nzima, zikisimamiwa na Waziri wa TAMISEMI, Selemani Jafo, zinafunikwa na sauti ya nyungu. Watu wanahamia kwenye nyungu na kuacha vituo vya afya!

Ukweli ni kwamba miluzi inaanza kumpoteza mbwa. Tangawizi, limao, vitunguu, pilipili kichaa na asali, vinaanza kufunika dawa za hospitali, vinafunika mashine za kusaidia kupumua. Wangapi wanapona, Mungu ndiye anajua.

Pamoja na yote hayo, na imani zote hizo, na mikanganyiko yote hiyo, bado ipo haja ya kuwa na sauti moja katika kukabiliana na matatizo. Ugonjwa uliopo bila kujali unaitwaje, unatakiwa kuchunguzwa na kuja na njia moja ya kuukabili kwa maslahi mapana ya afya ya jamii.

Tukishindwa katika nimonia ya mwaka huu, je, hiyo ya mwakani itakayoibuka kipindi kama hiki kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, tutafanya nini katika kuikabili?

Alamsiki!