Tunakumbushana tena ndugu ‘Mtoto wa Mwenzio ni Wako’

06Dec 2018
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tunakumbushana tena ndugu ‘Mtoto wa Mwenzio ni Wako’

MIMBA kwa wasichana, kwa sehemu kubwa inawagusa moja kwa moja wanafunzi. Ni changamoto inayoendelea kulikumba jamii, licha ya hatua mbalimbali zinazochukuliwa kudhibiti. Hapo nawataja wazazi na walezi ambao ni waathirika wa kwanza.

Pia, kuna serikali na wadau mbalimbali, kama wanaharakati wa haki za umma na kijinsia, asasi za kidini, wanaojitahidi kuvikemea vitendo hivyo.

Tatizo hili linaelezwa linatokana na sababu nyingi, miongoni mwake ni lifti ambazo wamekuwa wakipewa na madereva wa vyombo vya moto zikiwamo magari, pikipiki na bajaji.

Wakati mwingine, waathirika hao wa kwanza wa mimba – wasichana, wanalaghaiwa kwa fedha na zawadi zinazowanasa kirahisi katika mitego ghafla wanajikuta wakishindwa kumaliza masomo kwa kupachikwa mimba na hata kuolewa katika umri mdogo.

Shirika la Wanawake Katika Jitihada za Kimaendeleo (Wajiki), ni miongoni mwa wanaopambana na mimba hizo. Wanajikita zaidi katika elimu kwa madereva na makondakta wa vyombo hivyo vya moto, baada ya kuwabaini ndio wahusika wakuu.

Asasi hiyo, huwa inatumia njia kutafiti na kubaini kuwapo vitendo hivyo vinavyosababishwa na watu hao kwa kutumia lifti na kuwanasa kirahisi watoto wa kike.

Mkurugenzi wa shirika hilo, Janeth Mawinza, anasema wasichana wanarubuniwa na baadhi ya watu hao na mwisho wake wanaangukia katika mimba, pasipo kutarajia.

"Wengi wao wanalalamikia makondakta, madereva wa daladala, bodaboda na bajaj kuwa wametelekeza watoto waliozaa nao, tumebaini mambo mengi sana na sasa tunatoa elimu kwa watuhumiwa hao," anasema Mawinza.

Anasema, wamepata malalamiko kupitia klabu za wasichana walizozianzisha katika maeneo ya Mwananyamala Dar es Salaam na wanazitumia kukutana na wasichana, ili waeleze changamoto zinazowakabili.

Anaongeza kuwa, wameanza katika eneo la Mwananyamala, kwa kuwa ndiko yaliko makao makuu yao, kisha watapanua shughuli zao baadaye zifike mbali kitaifa.

"Huwa pia tunakwenda kwenye vijiwe vya watuhumiwa na kwa ajili ya elimu na kuwajengea uelewa, ili wafahamu athari za ngono na kutambua wajibu wao wa kuwa walezi pale wanaposababisha ujauzito," anasema.

Mkurugenzi huyo anaeleza kwamba, mwitikio ni mzuri na kwamba baadhi yao wamegeuka waelimishaji wa wenzao, kwa lengo la kukomesha tabia hiyo ya kurubuni wasichana kwa lifti za mgari na pesa kidogo.

Nimeanza kwa maelezo hayo marefu, lengo ni kutaka kuonyesha ni kiasi gani mashirika ya kiraia yanavyoshirikiana na serikali katika vita hii ya kupambana na tatizo la mimba.

Hiyo inatokana na ukweli kwamba, mimba za utotoni hazikubali, kwani mbali na kukatisha ndoto za wanafunzi, zina madhara kiafya.

Ujumla wake, mimba za utotoni huathiri afya, elimu na haki za mtoto wa kike. Mtoto wa kike asiye na elimu atakuwa na ugumu kupata ajira na kujijengea maisha bora na familia yake.

Wataalamu wa afya wanasema, anayeshika mimba akiwa na umri wa miaka 14 au chini ya hapo ni ambaye hajawa tayari kuyakabili majukumu ya uzazi na unyumba, nyonga zake zinaendelea kukua na mara nyingi njia ni finyu za uzazi, kiasi cha kwamba inawasababishia matatizo mengi ya uzazi, wakati wa kujifungua.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa Linaloshughulikia Watoto (Unicef), kati ya mwaka 2010 na 2017, Tanzania imeshika nafasi ya tatu kuwa na viwango vya juu vya ndoa za utotoni, nyuma ya baada ya Sudan Kusini na Uganda.

Kupitia mtazamo huo, ni kiashiria na mwongozo tosha kila Mtanzania mwenye mapenzi mema kwa taifa lake, ashiriki katika vita hivyo, badala ya kuachia serikali na mashirika ya kiraia. Ikibidi, anapaswa akumbuke kaulibiu: 'Mtoto wa mwenzo ni wako'.

Inapojitokeza asasi ya kiraia mtaani kwako inapiga vita mimba kama hiyo, ni muhimu kuunga mkono juhudi hizo kwa ajili ya kukomesha vitendo hivyo ili watoto wa kike wawe salama.

Jamii nayo inapaswa kukataa vitendo hivyo kila mahali waliko. Wanaotumia fursa ya kuwapeleka wanafunzi shuleni bure na kujenga mazoea ambayo yanaishia katika tamaa ya ngono.

Katika hilo jamii iendeleze msimamo wa kutokuwa na masihara nalo hata kidogo. Umma unapaswa kuwafuatilia wahusika kila wanapogundua dalili hiyo na kuwachukulia wahusika hatua, kwani hilo si la kuvumilia.