Tushikamane kuendeleza serikali ya mtaa

25Feb 2016
Elizaberth Zaya
Nipashe
Mjadala
Tushikamane kuendeleza serikali ya mtaa

OFISI za serikali za mitaa ni miongoni mwa sehemu zinazotegemewa katika kuhakikisha ustawi na kulinda maisha ya wananchi katika sehemu husika hata yanafikia hatua ya kuboreka.

Kwa namna moja au nyingine, ofisi hizo ni muhimu zaidi kwa sababu zina uwezo mkubwa wa kubeba taarifa za kila mtu katika mtaa husika na kuzifanyia kazi.

Pamoja na umuhimu wake, nyingi zimekuwa zikikabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwamo kutokuwa na mapato ya kutosheleza kuendesha wa shughuli za maendeleo mahali hapo.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Oysterbay, jijini Dar es Salaam Zefrin Lubuva, anasema pamoja na changamoto zilizoko katika ofisi yake, amepanga kuufanya uwe mfano wa kuigwa mbele ya mitaa mingine.

Akiwa hana muda mrefu tangu ashike wadhifa huo, anajigamba tayari amepanga kuubadilisha mtaa huo katika hatua ambayo hata viongozi wengine waliopita happ hajakuwahi kukifanya.

Anasema pamoja na kwamba ofisi yake haina pesa ya kutosha ambayo inaweza kufanya mtaa wake kuwa wa mfano, lakini zipo njia mbalimbali alizobuni, akiamini zinaweza kuubadilisha mtaa huo.

Mtazamo wa Lubuva ni kwamba, si lazima kiongozi akawa na fedha mkononi, bali atatumia rasilimali mbalimbali zilizopo chini ya himaya yake kuubadilisha mtaa anaouogoza.

Kimsingi, mtazamo wa Lubuva unapaswa kuwa mwelekeo wa kufuatwa na sehemu nyingi na ni somo la kiuongozi linalojitegemea.

Ofisi hizo za umma zina maana kubwa iwapo zitaendeshwa katika mfumo kama wa Lubuva. Tunajua kwamba ofisi hizi zinakabiliwa na changamoto nyigi tu.

Sehemu moja ya changamoto hizo ni kukidhi matakwa ya wanananchi wanaowahudumia katika matatizo mbalimbali na tukiingia kwa kina tunakuta kina cha mahitaji ya matatizo ya wananchi na uwezo wa ofisi, wakati mwingine haulingani.
Pia, katika sura nyingine ni kwamba, hali halisi ya uwezo wa kibajeti unaohitaji kuhudumia ofisi ni ngumu kufanikisha hata ukahitaji msaada wa ziada.

Sasa sote tulio wadau wa ofisi hizo za umma tunapaswa kuongozwa na mtazamo wa kiongozi wa Mtaa wa Oysterbay, kwamba mipango ya kina ndiyo ikatayofungua milango ya maboresho katika ofisi za serikali za mitaa, hata kabla ya fedha.

Hali kadhalika, sote tunaohusika kuanzia wenzetu viongozi madiwani, wabunge na wengine wa karibu katika safu ya uongozi na wananchi wa kawaida, kwa pamoja wanapaswa kuungana kusukuma mpango huo.

Mara nyingi katika utekelezaji wake huwa tunakwamishwa na utashi wa kisiasa hata tunapingana katika masuala ya maendeleo. Tunapaswa kubadilika sasa.

Kuiendeleza serikali ya mtaa ambayo kimsingi ina tafsiri ya moja kwa moja na maisha yetu, inasimama katika dhana ya ushirikiano.