Tushirikiane kudhibiti kuzagaa vilainishi hafifu

21Apr 2016
Christina Mwakangale
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tushirikiane kudhibiti kuzagaa vilainishi hafifu

BAADHI ya watu hutumia mwanya wa kupitisha bidhaa katika mipaka kwa njia za panya kutoka nje ya nchi, ambazo hazina viwango na ubora kwa mujibu wa sheria.

Hivi karibuni mikoa minne ya Arusha, Mwanza, Kilimanjaro na Dar es Salaam ilibainika kuwa vinara wa kuwa na vilainishi visivyo na ubora vilivyopo sokoni vinavyotumiwa katika magari na mashine mbalimbali.

Vilainishi hivyo ni vile ambavyo huingizwa nchini kiholela, huku baadhi ya wazalishaji wa ndani hutumia fursa ya soko kubwa lililopo na kuzalisha vilainishi visivyo na ubora na kuvipenyeza sokoni.

Aprili 5, mwaka huu, Shirika la Viwango Tanzania lilitangaza ongezeko kubwa la vilainishi hivyo sokoni, ambavyo hutumika katika magari na mitambo mbalimbali huku wadau wa vilainishi, wakiwamo wazalishaji, waagizaji, taasisi na mamlaka za serikali walikuitana ili kutoa maazimio ya pamoja.

Wizara ya Viwanda na Biashara, Mamlaka ya Udhibiti Nishati, Maji na Mafuta (Ewura), Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Shirika la Viwango la Tanzania (TBS), waliweka maazimio ya pamoja ya kuwataka wazalishaji nchini na waagizaji wa bidhaa hiyo nje kusajiliwa kabla ya bidhaa hizo kuingizwa sokoni kisha kuchukuliwa hatua za kisheria.

Ukweli uko bayana kuwa, ongezeko kubwa la vilainishi na oil sokoni, linatajwa kuwa na athari kubwa kiuchumi kwani iwapo mitambo ya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali ikitumia vilainishi hivi, inaweza kuharibika lakini hata injini za magari zinaweza kuharibika pia.

Ushirikiano na kuimarisha ulinzi katika mipaka ya nchi itakuwa ni suluhisho, huku waagizaji na wazalishaji wa vilainishi wakizingatia kanuni, sheria zilizopo.

Kwa mtazamo wangu ni kuwa, changamoto hiyo itaondolewa kwa ushirikiano wa pamoja kati ya taasisi za serikali ikiwamo wadau mbalimbali kwa kuwapa elimu kuhusu umuhimu wa matumizi ya sheria, kusajili waagizaji ili kubaini wanaokiuka kanuni na taratibu zilizopo hata kuwachukulia hatua mapema kabla hawajasababisha madhara kwa jamii.

Katika hali hiyo, ndio maana Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Joseph Masikitiko alisema kuwa kwa sasa hali ni mbaya nchini, kutokana na kukithiri kwa vilainishi hivyo, ambayo ni hatari kwa wamiliki wa magari na mitambo kutokana na ukweli kuwa vinahatarisha kushusha uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Ninachoshauri ni kuwa,kila mmoja katika nafasi yake kuhakikisha kuwa anatoa ushirikiano wa kutosha wa kudhibiti uingizaji holela wa bidhaa hizo feki ambazo haziingii kwa njia halali na kama zinaingia basi ni kwa hila ya watu wachache wasioitakia mema nchi yetu.

Kama kila mmoja wetu atafanya kila awezalo katika kuhakikisha kuwa, anachunguza na kutoa taarifa za uhakika kwa mamlaka husika, kwa watu wote wanaojishughulisha na vitendo hivyo vya kuhujumu uchumi ni kwamba naamini kabisa kuwa, idadi ya wahujumu uchumi itapungua kwa kiwango kikubwa kabisa.

Ifahamishe kuwa, kuruhusu watu hao kujineemesha kwa kutumia uchache wa vyombo vya sheria vyenye dhamana ya suala hilo ni kujimaliza wenyewe.

Vilainishi hivyo hutumiwa katika mitambo na mashine ambazo zitashindwa kufanya kazi sawasawa na hivyo kusababisha athari mbaya sana kwa maisha na uchumi kwa ujumla.

Katika hali hiyo kwa nini turuhusu hali ifikie kuwa ya mashaka matupu wakati kinachotakiwa ni kuwaumbua wahusika ili wachukuliwe hatua thabiti.

Linalowezekana leo lisingoje kesho