Tusibweteke kulaumu watoto, kuhusu Mchina, hisabati je?

26Feb 2016
Peter Orwa
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tusibweteke kulaumu watoto, kuhusu Mchina, hisabati je?

TANGU yatoke matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne, mjadala uliotawala ni mambo makubwa yaliyofanywa na binti wa Kichina katika mtihani huo.

Mjadala huo ukiangaliwa kwa kina, dhana kuu imesimama katika mazingira ya kulaumu, inakuwaje Mchina kutuongoza na sauti ya malalamiko inapazwa zaidi katika somo la Kiswahili.

Naam! Wanamichezo wana usemi wao, raha ya mpira magoli. Binti wa Kichina kafanya vyema katika mtihani ikiwemo somo la lugha aliyokutana nayo ughaibuni, kwa maana ya mazingira ya mbali kutoka kwao.

Tunashindwa kujiuliza sababu za kufanikiwa huko, kwa kujiuliza alikuwa anasoma katika shule yenye ubora gani, mwanafunzi mwenyewe ana uwezo upi na namna alivyokuwa akijituma masomoni.

Mtazamo wangu ni kwamba kweli watu wameguswa na hali hiyo ya vijana nchini kushindwa na mgeni huyo wa mandhari ya Afrika Mashariki au Afrika kwa ujumla.

Kulaumu kunatakiwa kufanyike mara moja kuonyesha majuto, lakini baada ya hapo ni hoja yenye mtazamo wa kujenga zaidi ‘tunaondokaje na hili?’

Jambo muhimu ni kwamba, matokeo ya mtihani huo yanapaswa kuangaliwa katika mtazamo mpana zaidi. Somo la hisabati limeshika mkia na wala hakuna masikitiko ya wazi yanayoonekana kwa wengi.

Nikimnunkuu mwalimu mmoja wa hisabati ambaye hoja yake naikubali kwa asilimia 100, ni kwamba somo hilo linaingia kila mahali na hivyo linalofanya kuwa muhimu kwa mwanafunzi kulifahamu ‘atake asitake.’

Katika mtazamo ule ule ambao wadau wa elimu wanalia na kusikitika kwa kushindwa na Mchina, inapaswa kuwepo mjadala wa hisabati kusuasua.

Vilevile wadau wa elimu kwa kushirikiana na serikali, wanapaswa kulibeba hilo na kuingia kwa kina kutafiti sababu zipi zinazofanya kasoro hizo zitokee.

Hilo litakuwa jambo muhimu kitaaluma na kuweka msingi wa namna tunavyoweza kusonga mbele kitaaluma, kupitia utambuzi wa mapungufu yenye na namna tunavyoweza kuyazuia.

Kwa mfano siri ya mafanikio ya binti wa Kichina katika mitihani yake, ina maana kubwa katika hatima ya maisha yetu ya maendeleo ya kielimu.

Naamini kuna mengi aliiyo nayo msichana huyo ambayo yakibebwa kama dhana muhimu, yanaweza kutumika hata inapobidi kuingizwa katika mitaala katika stadi za kufundisha na kusoma kwa mwanafunzi, baada ya kufanyiwa utafiti.
Jamii inapaswa kuondoka katika uwanja wa kulaumu na kulalamika na kuhamia katika kutathmini na kufanyia kazi.

Hivi sasa nchini kuna taasisi nyingi za elimu na miongoni mwake, kuna vyuo vikuu ambavyo ni vingi zaidi ya 50 ambavyo Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alivibana akuvitaka kila kimoja kiwe na kitivo au idara inayoendesha kozi ya ualimu.

Katika lugha nyepesi taifa ina wataalam wengi wa elimu, huku taasisi hizo za elimu ya juu zikiwa na majukumu makuu matatu; Kufundisha, kutoa ushauri wa kitaalam na kufanya utafiti.

Je changamoto hiyo ya vijana wa Kitanzania “kupigwa overtake” na binti wa Kichina katika mtihani na kiwepo mwendelezo wa wimbo wa kila siku hisabati kuwa janga la kitaifa wanalichukuliaje?

Hayati Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1964 aliwaambia Watanzania namna ya kushiriki kujenga taifa lao kupitia usemi “It can be done, play your part’ akimaanisha inawezekana kila mmoja akitimiza wajibu wake.
Ni mwaka ambao Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (1964- 196) ulizinduliwa.