Tusitumie maneno tusiyojua maana yake

05Dec 2017
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
Tusitumie maneno tusiyojua maana yake

LEO naja na maneno yanayotumiwa kinyume kabisa na maana yake. Tabia hii huanzishwa na chombo kimoja cha habari na kesho yake vyombo vyote hufuata mkumbo.

Baadhi ya maneno ni kama yamepata ithibati (kitu au muhuri unaodhihirisha ukweli; uthibitisho) ya Baraza la Kiswahili Tanzania.

      Siku hizi msichana huitwa ‘demu’ na anayeitwa hivyo hashituki kwani hata yeye hujitambulisha kwa wenzake kuwa yeye ni ‘demu’ wa kijana fulani kumbe anajidhalilisha!

     ‘Demu’ ni kitambaa kikuukuu kinachovaliwa na mwanamke kufunika matiti/maziwa wakati wa kulima. Pia ni tambara au nguo iliyochanika. Kwa hiyo msichana aitwapo jina hilo hudhani anasifiwa kumbe kafananishwa na tambara au nguo iliyochanika!

     Kwani wavulana washindwa nini kuwaita wapenzi wao majina kama laazizi, muhibu, sahibu, mahabubu n.k.? Nahisi kuna wakati wasichana wataitwa ‘majamvi’ nao watakubali bila kujua maana iliyojificha!

     Kuna maneno ‘mhenga’na ‘mhanga’ ambayo hutumiwa kinyume na maana halisi. Kwa hakika ‘mhenga’ni mtu mzee anayefikiriwa kuwa babu wa kale wa jamii fulani; mjuzi wa mambo ya kale mwenye kutegemewa kutoa ushauri katika masuala ya kijamii.

     Kinyume chake, neno hilo hutumiwa kwa wachezaji wanaoonekana ‘kuchoka’ kwa maana ya kufika mwisho wa uwezo wao! Utasikia ikisemwa: “Mchezaji yule siku hizi ni mhenga!”

     Mhanga ni mtu aliyejitolea kutoa maisha yake katika kupigania haki au kumwokoa mwingine aliye kwenye hatari inayoweza kumsababishia kifo. Kwa mfano, kama unajitupa majini kumwokoa mtu aliyezama, wewe unajitoa ‘mhanga’ yaani uko tayari kupoteza maisha ili umwokoe mwingine.

     Kadhalika watu wanaodai haki zao k.m. wapigania uhuru kwa njia ya kujilipua katikati ya mkusanyiko mkubwa wa watu ni ndiwo waitwao‘wahanga.’

     Pamoja na ukweli huo, watu wanaoangukiwa na nyumba zao, wanaopata ajali ya magari kupinduka, treni au ndege (eropleni) kuanguka ama kushambuliwa na majambazi eti huitwa ‘wahanga!’ Si sahihi.

     Wanaopata ajali yoyote iwe nchi kavu, majini au angani huitwa ‘manusura’ yaani walioponea chupuchupu kupoteza maisha.

     Neno lingine litumiwalo vibaya ni ‘mashaka’ kwa dhana kuwa ni wingi wa ‘shaka’ kumbe lapotoshwa. ‘Mashaka’ ni shida zinazompata mtu katika maisha; tabu. Kwa mfano yaweza kusemwa kina mama wanaopita mitaani na watoto kuombaomba, maisha yao ni ya mashaka.

     Ni kweli wanaishi maisha ya mashaka kwani hulala mbele ya baraza za maduka na kula kwao ni kwa kubahatisha au huruma ya wenye hoteli na wapita njia wanaowapa ‘vijihela’ visivyokidhi haja!

     ‘Shaka’ ni neno  lenye maana mbili tofauti. Kwanza ni hali ya kujawa na wasiwasi na kukosa uhakika wa jambo; hatihati, wahaka. Pili ni fukuza; shunga, winga, furusha.

     Kwa hiyo ‘shaka’ halina wingi na kama likilazimishwa kuwa na wingi, yaani ‘mashaka’ linaleta maana tofauti kabisa kama nilivyoeleza huko juu.

     Neno lingine linalopotoshwa ni ‘madhehebu.’ Kwa kuwa neno hili lipo katika umoja na wingi sawia, ni kosa kuliweka katika umoja kama wengine wasemavyo ‘dhehebu!’

     ‘Dini’ moja huitwa ‘dini’ na nyingi pia huitwa ‘dini.’ Isemwapo ‘madini’ kwa maana ya wingi, ni kitu cha thamani kinachochimbwa ardhini kama almasi, dhahabu, tanzanaiti (tanzanite) n.k.

Ingawa yasemwa ‘dini hizi’ kwa maana ya nyingi, huwezi kusema ‘dhehebu hili’ ukiwa na maana ya moja. Iwe moja au nyingi huitwa ‘madhehebu.’ Yasikitisha hata vyombo vyetu vya habari hutumia sana ‘dhehebu’ badala ya madhehebu!  ‘Madhehebu’ ya Kikatoliki, Kianglikana, Kiluteri n.k.

Hivi karibuni kituo maarufu cha runinga humu nchini kilikuwa na maandishi kwenye skirini yaliyosomeka: “Serikali yawakilisha muswada wa sheria ya marekebisho.”

Watu huchanganya ‘wakilisha’ na ‘wasilisha’ kwa dhana kuwa yana maana moja. Hasha! Maneno haya yana maana tofauti kabisa.

‘Wakilisha’ ni kitenzi elekezi na maana yake ni fanya shughuli kwa niaba ya mtu mwingine. Ni neno linalotokana na ‘wakili’ (nomino) na maana yake ni mtu mwenye elimu ya sheria anayemtetea mtu katika kesi mahakamani. Pia mtu aliyepewa jukumu na mtu mwingine kusimamia shughuli yake; dalali.

‘Wasilisha’ ni fikisha kitu au ujumbe ulipohitajiwa; toa maelezo au mhadhara kwa kikundi cha watu au mbele ya watu.

     Kwa hiyo ingeandikwa: “Serikali yawasilisha muswada wa sheria ya marekebisho.”

     Namalizia na maneno ‘maambukizi’ na ‘maambukizo.’ Maambukizi ni mchakato wa usafirishaji au usambazaji wa vimelea vya ugonjwa kutoka sehemu au kiumbe kimoja kwenda sehemu ama kiumbe kingine kwa vichukuzi maalumu kama vile mmbu, nzi, chawa, kunguni, binadamu n.k.

     ‘Maambukizo’ ni tendo la kuingiza vimelea vya ugonjwa kutoka sehemu au kiumbe chenye ugonjwa hadi kiumbe au mmea usio na ugonjwa.

Methali: Udongo upatilize uli maji.

[email protected]

0715/0784  33 40 96