Tutumie Royal Tour kujitangaza, kujiimarisha kiuchumi

24Apr 2022
Salome Kitomari
Nipashe Jumapili
Nawaza kwa Sauti
Tutumie Royal Tour kujitangaza, kujiimarisha kiuchumi

FILAMU ya Royal Tour iliyochezwa na Rais Samia Suluhu Hassan, akiwa kama mwomgoza watalii akimwongoza Mwandishi Peter Greenberg, ambaye alitembezwa na kuelezwa kwa kina kuhusu vivutio vilivyopo nchini vitakavyomfanya mtu yeyote atamani kutumia fedha na kukaa zaidi nchini kwetu ina manufaa makubwa.

Katika filamu hiyo, Rais Samia anaonekana kumudu vyema kazi yake ya kuongoza watalii kwa kumweleza kuhusu vivutio kwenye Hifadhi za Taifa na Zanzibar.

Pia Rais alionekana akimwendesha mgeni wake kwenye gari la watalii huku akimweleza na mtalii akiuliza maswali mengi ya kutaka kujifunza zaidi au kufurahia safari yake anapokuwapo nchini.

Ukitazama sehemu ndogo ya filamu hiyo iliyoachiwa kwenye mitandao, utaona namna gani inatengeneza hamu au sababu ya mgeni kutoka taifa lolote anapopanga safari yake kufikiria pa kwenda ni Tanzania pekee na si kwingine.

Mara nyingi tumeona jitihada za nchi jirani kujitangaza kwa kutumia vivutio vilivyoko nchini kwao hata vile vilivyoko mpakani, wanavitumia ili kuwavutia watalii.

Mathalani, niliwahi kwenda Geneva, Uswisi nikaona mabasi na treni kwa wiki moja ambayo kulikuwa na mkutano wa dunia wa masuala ya majanga, yakiwa yamepambwa picha za Mlima Kilimanjaro, hifadhi za taifa na wanyama watano wakubwa wanaopatikana nchini lengo likiwa ni kutengeneza sababu kwa nini mtalii atembelee kwao.

Nilipofika uwanja wa ndege, niliona kwenye mbao za matangaza za ndani na nje wameweka Mlima Kilimanjaro na wanyama hao kuendelea kumshawishi mtalii kupanga safari na kuifanya nchi hiyo kuwa kituo chake muhimu.

Ndani ya ndege ya Shirika la Ndege la Uturuki, nilikuta jarida ambalo ndani yake kulikuwa na makala iliyoandikwa kwa ustadi ikiambatanishwa na picha mbalimbali, kuendelea kutengeneza sababu ya mtalii kwenda nchini humo.

Kama Mtanzania, nilisikitika kwa nini sikuona makala ya nchi yangu wakati naelewa fika Mlima Kilimanjaro uko nchini kwangu, ukitaka kuupanda vizuri kwa njia nzuri na kuuona vizuri lazima upandie Tanzania lakini ukitaka kuona nyumbu wanavyohama lazima uje upande wa Tanzania.

Kama haitoshi nyumbu wote wana hati za kusafiria za Tanzania kwa kuwa lazima wakabebe mimba Masai Mara waanze kurudi taratibu wakipita kituo hadi kituo ikiwamo eneo la mtawanyiko la Loliondo, Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCA) na baadaye kurudi Hifadhi ya Taifa Serengeti ambako huzaliana na ikiwa kutakuwa hakuna mvua basi wana uwezo wa kuahirisha kuzaa hata kwa miezi mitatu.

Filamu hii ni muhimu mno kwa taifa, kwa sekta binafsi na serikali ikiwa wataziona fursa zilizoibuliwa, mathalani Mtanzania wa kawaida kabisa anaweza kujiuliza hiyo filamu inamsaidia nini na kwa jinsi gani itaboresha maisha yake.

Watalii wanapoongezeka kwenye hifadhi na vivutio vyetu ndiyo mapato, ajira za kudumu na huduma za kijamii zinaongezeka. Mwekezaji  atajenga hoteli atahitaji watu wa kuajiri, atanunua bidhaa kutoka kwa wakulima, wananchi watauza bidhaa za utalii au zinazoendana na utalii kama vitu vya utamaduni, vyakula vya asili na kuonyesha utamaduni kisha watapata kipato.

Pia kuna maeneo yaliyohifadhiwa na jamii yanayojulikana kama Wildlife Management Areas (WMA) ambayo wanyama hupita kwenda hifadhi nyingine, wanajipatia kipato kwa kuwa na wawekezaji. Mathalani, Burunge WMA waliwahi kupata Sh. bilioni  2.2 ambazo Sh. bilioni 1.1 ilikwenda serikalini na iliyobaki iligawanywa kwenye vijiji ambavyo vilipata wastani wa Sh. milioni 100.

Kupitia utalii wamefanya miradi mingi ya huduma za kijamii na ni moja ya vijiji vyenye ofisi nzuri ambazo zinaweza kufanana na za baadhi ya halmashauri nchini.

Katika kila hifadhi, kuna ujirani mwema, kwamba sehemu ya mapato yanarudi kwa jamii kupitia vipaunbele vyao vya huduma za kijamii kama elimu, afya,  na miundombinu ya maji na barabara ambavyo ni kwa faida yao.

Kwa ujumla, kwenye utalii kuna ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, hivyo filamu hii itakapoanza kuleta matokeo ni lazima tuyatumie vizuri kwa manufaa yetu binafsi, maeneo yetu na taifa kwa ujumla.

Lazima kila mmoja katika eneo lake ikiwamo sekta binafsi kujiandaa kunyonya fursa zilizopo, ili kuona umuhimu kwa kazi kubwa iliyofanywa na Rais Samia ya kuongoza watalii kwa lengo la kuitangaza Tanzania duniani na kutengeneza sababu ya kwanini mtalii achague kutumia muda na fedha zake hapa nchini na siyo kwenda kwingine.

Katika mahojiano ya Rais Samia na Mwandishi Peter, alisema moja ya mambo  ambayo mgeni yeyote hatajutia kwa kuja nchini, ni ukarimu wa Watanzania, jambo ambalo ni kweli limekuwa utanaduni wetu kukirimu wageni kwa mengi na tunasifika Afrika kwa ukarimu mkubwa.