Tutumie Siku ya Tumbaku leo kutathmini pumzi zetu

31May 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tutumie Siku ya Tumbaku leo kutathmini pumzi zetu

LEO ni Siku ya Kimataifa Duniani ya Kutovuta Tumbaku, ikiwa na ujumbe mbalimbali kwa jamii wenye lengo la kuacha uvutaji wa kilevi hicho.

Maadhimisho ya mwaka huu yana ujumbe ‘usikubali tumbaku ichukue pumzi yako.' Hiyo inabeba maana kwamba, uvutaji wa sigara au tumbaku una madhara, hivyo mtu asikubali matumizi ya kilevi hicho yaondoe uhai wake.

Shirika la Afya Duniani (WHO), linasema madhara ya matumizi ya tumbaku kwa mapafu ya binadamu kuwa zaidi ya asilimia 40 ya vifo vikihusiana na matumizi hayo.

Ni vifo vivyohusiana na magonjwa kama saratani, magonjwa sugu ya njia ya hewa na kifua kikuu.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk. Tedros Ghebreyesus, anakaririwa kwamba kila mwaka kuna watu milioni nane wanaofariki kutokana na tumbaku, huku mamilioni wengine wanaishi na magonjwa sugu.

Anataja baadhi ya magonjwa hayo kuwa saratani, kifua kikuu, pumu au magonjwa sugu ya njia ya hewa, ambayo yamekuwa yakisababishwa na matumizi ya tumbaku.

WHO inasema, zaidi ya watoto 60,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano wanafariki dunia kwa kuvuta moshi. Watu wanaoishi hadi utu uzima wakiwa katika nafasi kubwa zaidi ya kupata magonjwa sugu ya njia ya hewa mara wanapofikia umri wa utu uzima.

Dk. Ghebreyesus anasema mvuto mmoja wa moshi wa tumbaku una mamia ya kemikali za sumu, ambazo huanza kuharibu mapafu, mifumo ya kusafisha makohozi na uchafu kutoka kwenye mapafu inadhoofishwa. Ni jambo lialoruhusu sumu iliyomo katika tumbaku kuingia kwenye mapafu kirahisi.

Anasema, kuna haja ya kujiepusha matumizi ya tumbaku kulinda afya zao, kwa kuzingatia mapafu yenye afya ni muhimu, ili mtu anaweze kuishi maisha yenye afya.

Rai yake ni kwamba, serikali zipunguze matumizi ya bidhaa za tumbaku, kwa kuongeza kodi, kutenga maeneo ya uvutaji, ili kuwasaidia wanataka kuondokana nayo.

"Wazazi, walezi na viongozi wa kijamii wanatakiwa kuchukua hatua kulinda afya za familia kwa kuwaeleza wazi madhara ya matumizi ya tumbaku na mbinu za kujiepusha na matumizi yake," anasema.

Anasisitiza kuwa, udbibiti wa tumbaku utasaidia kufanikisha kupunguza idadi ya wanaofariki dunia kabla ya muda, kutokana na uvutaji tumbaku ifikapo mwaka 2030.

Malalamiko yake ni kwamba, bado dunia haiko kwenye mwelekeo wa kutimiza lengo, hivyo kila mtu anapaswa kulinda mapafu yake, ya rafiki zake na familia, kwa kukataa kutumia tumbaku.

KILIO CHA TTCF

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Kudhibiti Tumbaku Tanzania (TTCF), Lutgard Kagaruki, anataka sheria inayoendana na matakwa ya Mkataba wa Kimataifa wa Kudhibiti Tumbaku WHO itekelezwe.

Anasema tumbaku ni kisababishi namba moja cha magonjwa yasiyoambukiza ikiwamo saratani, moyo, magonjwa sugu ya kifua, kisukari na mengine mengi na pia asilimia 90 ya saratani ya mapafu husababishwa na tumbaku.

"Tanzania ni nchi pekee ndani ya Afrika Mashariki isiyokuwa na sheria madhubuti ya kudhibiti tumbaku; Zanzibar inayo sheria bora na hata Ethiopia juzi juzi imetoa sheria bora kuliko zote Afrika," anasema.

Kagaruki anasema ni wakati sasa kwa serikali kutunga sheria bora, ili kulinda afya, mazingira, uchumi na ustawi wa jamii ya Watanzania.

Tumbaku ni miongoni mwa mazao matano ya kimkakati, ambayo katika mwaka wa fedha 2018/2019, serikali ikilenga kuimarisha masoko yake na mazao hayo kwa kuhamasisha mfumo wa stakabadhi ghalani, huku yakizalishwa na kuuzwa kupitia vyama vya ushirika kwa njia ya minada.

Mwelekeo wa kazi za serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019, wana mtazamo wa katika mkakati huo, lengo kuongeza mapato ya wakulima utokanao na chanzo cha kuaminika cha malighafi katika uchumi wa viwanda na kuendelea kuwa chanzo kikuu cha ajira na fedha za kigeni.

Inaelezwa uamuzi wa kuongeza usimamizi katika uzalishaji wa mazao hayo makuu ya biashara unatokana na ukweli kwamba, kwa kipindi kirefu uzalishaji ulishuka kutokana na changamoto kadhaa.

Miongoni mwa sababu hizo ni vyama vya ushirika kutotekeleza vyema wajibu wao, wizi, dhuluma na pia ushiriki mdogo wa maofisa kilimo katika kusimamia kilimo cha kitaalamu.