Tuwe makini kufanikisha kukwepa yanayokaribisha magonjwa mlipuko

03Jun 2021
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tuwe makini kufanikisha kukwepa yanayokaribisha magonjwa mlipuko

MTINDO wa baadhi ya watu wa kutozingatia usafi wa mazingira, hutajwa kuwa miongoni mwa vyanzo vinavyosababisha kuenea maradhi na kuhatarisha afya za wahusika na wengine.

Utupaji taka ovyo kama kinyesi, majitaka na nyingine, vinaweza kusababisha matatizo ya afya, hivyo suala la kuzingatia usafi wa mazingira ni muhimu ili kuepusha watu kukumbwa na magonjwa ya mlipuko kikiwamo kipindupindu.

Hivyo, wale ambao wamezoea kuchafua au kutozingatia usafi wa mazingira, ni vyema wakatambua kuwa wana nafasi kubwa ya kuhatarisha afya zao na za wengine wanaowazunguka.

Kutokana na hali hiyo, Shirika la Afya Duniani (WHO), limekuwa likihimiza usafi wa mazingira, kwa kuwa uboreshaji wa mazingira una manufaa makubwa katika jamii hasa kuepusha mlipuko wa magonjwa.

Usafi wa mazingira ni muhimu kwa lengo la kuhakikisha kuwa afya inazingatiwa kila sehemu, iwe nyumbani au kwenye shughuli mbalimbali ili kuzuia uwezekano wa binadamu kukabiliana na athari za taka.

Hata hivyo, baadhi ya watu hasa kwenye miji mikubwa kama Dar es Salaam, hutiririsha majitaka kutoka katika vyoo vyao kwenda mitaani mvua inaponyesha na kuibua harufu kali inayohatarisha afya zao na za wengine.

Wapo wanaofanya hivyo kwa madai kwamba, hawana uwezo wa kulipia magari ya kunyonya majitaka na kutokana na hilo, wengine hujenga vyoo kando ya mito na kuelekeza humo mabomba kutoka vyooni.

Mtindo huo kwenye baadhi ya maeneo umekuwa kama wa kawaida, ambapo wengine wakivizia hadi usiku wa manane na kutiririsha majitaka hayo, hali ambayo kimsingi ni uchafuzi wa mazingira na ni hatari kiafya.

Itakuwa vyema, iwapo mamlaka husika zitafuatilia hali hii na kuipatia ufumbuzi wa kudumu ili kulinda afya watu kuliko kundi dogo kuendelea kuhatarisha afya za wengine kwa kuchafua mazingira.

Kwa mfano, baadhi ya mabomba ya maji ya kunywa huku mingine ikiwa imechakaa na kufungwa mipira, imepitishwa kwenye mitaro ambayo wapo watu wamegeuza kuwa sehemu ya kutiririshia majitaka yao.

Ni wazi kwamba, hali kama hiyo ni rahisi majitaka kuingia ndani ya mabomba hayo na kuchanganyika na maji ya kunywa, na  hivyo inakuwa ni rahisi watu kukumbwa na magonjwa ya mlipuko kama watayatumia.

Ikumbukwe kuwa, pamoja na kuwapo kwa elimu inayohusu unywaji maji yaliyochemshwa, bado wapo baadhi ya watu wasiochemsha, hivyo katika  mazingira hayo ni rahisi wao kukumbwa na magonjwa ya mlipuko.

Kimsingi, jamii inapaswa kutambua kuwa, uboreshaji wa mazingira una manufaa makubwa kiafya, hivyo mmoja wetu kwa nafasi ahakikishe anasafisha mazingira yanayomzunguka.

Usafi uwe ni pamoja na kuacha kutiririsha majitaka ovyo, kutojisaidia ovyo na pia kufanyia biashara katika mazingira safi ili kuepuka kukumbwa na magonjwa ya mlipuko ambayo huibuka mara kwa mara.

Katika maisha, kila siku wapo baadhi ya watu wasiozingatia usafi wa mazingira kwa kufanya biashara ama shughuli zao kwenye mazingira machafu bila kujali kuwa ni hatari kwao na kwa wateja wao.

Imekuwa kama jambo la kawaida kukuta baadhi ya mama lishe na baba lishe kufanyia biashara zao katika mazingira machafu, hali ambayo si salama kwao na kwa wateja wanaofika kupata huduma ya chakula.

Njia mojawapo ya kupunguza, kama si kumaliza mtindo wa kutozingatia usafi wa mazingira ni kuendelea kuwapo kwa elimu kwa wahusika ili kila mmoja atambue umuhimu wa kuwa katika mazingira safi.

Kila kukicha wamekuwa wakiibuka watu wapya hasa kwenye biashara ikiwamo ya mama lishe na baba lishe, hao wote wanatakiwa kuelimishwa kuhusu usafi wa mazingira ili walinde afya zao na wateja wao.

Elimu ikitolewa ipasavyo, wahusika wakaielewa na kuizingatia, ninaamini hakutakuwa na utiririshaji wa majitaka mitaani au kwenye mito ama mama lishe na baba lishe kuandalia vyakula katika mazingira machafu.

Kwa ujumla ni kwamba, elimu ya afya iendelee kutolewa kwa kina huku wale ambao watakuwa wanakiuka, wabanwe na sheria ndogondogo za halmashauri, kwani afya bora ni mtaji mkubwa.