Tuzo maalumu kwa walimu ziandaliwe ili kuwatia moyo

16Apr 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tuzo maalumu kwa walimu ziandaliwe ili kuwatia moyo

KATI ya kazi zenye changamoto nyingi ni ya ualimu.

Hiyo inatokana na ukweli kwamba walimu wamekuwa wakikumbana na kila adha kwenye maisha yao ya kila siku.

Unaweza kukuta shule ina wanafunzi zaidi ya 200, lakini ina walimu wachache wasioweza kumudu wingi huo.

Hata hivyo, utakuta wanachapa kazi kama kawaida kwa vile wanatambua kazi yao ni ya wito.

Kwa kifupi walimu ni watumishi wanaokabiliwa na changamoto nyingi katika utekelezaji wa majukumu yao, ingawaje kuna baadhi ya wenzetu ambao wamekuwa wakiwaona kama si wa muhimu kwenye jamii.

Ninaposema baadhi ya watu wanaiona kazi hiyo si ya muhimu, maana yangu ni kwamba wapo wanaowadharau na kuwaona wa kawaida na ndio maana kuna walimu waliowahi kuchapwa viboko hadharani.

Iliwahi kuripotiwa katika vyombo vya habari kuwa baadhi ya watu walikusanyika eneo la wazi na kuwachapa walimu mbele ya wanafunzi, wakiwatuhumu kuwapa adhabu watoto wao.

Tukio hili liripotiwa kutokea kwenye moja ya mikoa ya kanda ya ziwa Viktoria, ambapo waliotumika kuwachapa walimu walikuwa ni walinzi wa jadi (sungusungu).

Changamoto za walimu haziishii hapo tu, kuna matukio ya mambo ya kishirikina ambayo wamekuwa wakidai kukumbana nayo katika maeneo yao ya kazi hadi kufikia kuomba uhamisho.

Kwa mazingira kama hayo na mengine ambayo yamekuwa yakiripotiwa ni wazi kuwa yanawakatisha tamaa, na ndiyo maana nasema kazi ya ualimu ina changamoto nyingi.

Muungwana anaona kuwa ni vyema basi kwa jamii kuwaheshimu, ili kuwatia moyo wafanye kazi yao kwa bidii pamoja na changamoto nyingi wanazokutana nazo.

Jamii iache maneno ya kejeli kwa walimu hawa, kwani wana umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya nchi, ingawa baadhi ya wenzetu, huwaona kama hawana lolote.

Ualimu ni taaluma muhimu na ya kuheshimiwa! hebu fikiria kwamba mtoto anaanza shule akiwa hajui kusoma na kuandika, lakini mwalimu anamsaidia kwa kila hali ili kuhakikisha anajua kusoma na kuandika.

Uandaaji wa watoto kitabia, kimaadili na kitaaluma ni kazi ya wito na ni ngumu ambayo inahitaji kuungwa mkono na jamii ili iweze kutoa matunda bora ya ustawi wa jamii.

Hivyo, inasikitisha pale mtaalamu huyu anapodharauliwa! Siyo vizuri kabisa.

Wale wanaodharau walimu watambue kuwa viongozi na watu wenye nafasi mbalimbali za uongozi wametoka kwa walimu hao hao kuanzia wale wa shule za msingi, hivyo heshima kwao ni muhimu sana.

Na nidhamu hujengwa kati ya walimu na wanafunzi na ndio maana miaka ya nyuma mwanafunzi akikutana na mwalimu njiani alikuwa akimpokea mzigo na kuufikisha kule mwalimu anakokwenda.

Cha kushangaza siku hizi heshima kama hiyo haipo tena, si wanafunzi wala wazazi, baadhi yao wanaona walimu kama si lolote kwao ndio maana wanafikia hatua hata ya kuwatukana au kuwaadhibu hadharani.

Ni rai ya Muungwana kwamba kama njia ya kuwamotisha walimu, wadau na serikali waanzishe tuzo maalumu ya kuenzi kazi nzuri inayofanywa na kada hiyo kwa ustawi wa taifa letu.

Hiyo ni kutokana na uvumilivu wao kwa kazi wanayoifanya katika mazingira magumu kama bila ya kuchoka.

Inaweza ikawa ni tuzo ambayo walimu wataishindania lakini lengo kubwa liwe ni kutambua na kuthamini kazi kubwa wanayoifanya ingawa ni katika mazingira magumu.

Tuzo za aina hiyo zinaweza kuwaongezea ari ya kufanya kazi yao kwa bidii wakitambua kuwa nyuma yao kuna watu wanathamini mchango wao katika maendeleo ya elimu nchini.

Hatua hii inaweza kusaidia kubadili mawazo ya hata wale ambao wamekuwa wakiwadharau walimu ili watambue kazi kubwa zinazofanywa na kundi hilo ambalo ni nguzo ya maendeleo ya kielimu kwa kila Mtanzania.