Twaitakia Simba kila la heri

13Apr 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Twaitakia Simba kila la heri

LEO ni kufa au kupona kwa timu ya Simba dhidi ya TP Mazembe zitakaporudiana kule Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) baada ya kutoka suluhu katika mchezo wa kwanza uliochezwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.

Si rahisi kubashiri mshindi kwani mchezo wa mpira una matokeo ya ajabu. Wakati mwingine umdhaniye ndiye huwa siye na adhaniwaye siye huwa ndiye! Kwa kuwa mpira hudunda, kosa moja laweza kuiathiri timu yoyote. Msemaji wa Simba, Haji Manara ametamba kuwa hakuna timu yoyote itakayokuja kupambana na Simba kwenye uwanja wa Taifa iondoke na ushindi.

Wahenga walisema “Maneno fedha, majibu dhahabu” wakiwa na maana maneno tusemayo ni kama fedha lakini majibu ni kama dhahabu. Twashauriwa tuwe na tabia ya kutoa majibu yanayoweza kuonesha kuwa tunazitumia akili zetu. Yafaa kutafakari kabla ya kujibu jambo fulani.

Hakika Simba ina timu iliyoenea kila sehemu. Hapana shaka ina timu pana, kwa maana ya wachezaji wanaojua kusakata (fanya jambo kwa umahiri) kabumbu ipasavyo na la kuvutia. Hivyo hawapaswi kuwa na wasiwasi wala woga bali kila mmoja atimize wajibu wake. Wachezaji wasiwe wachoyo kupeana mpira bali wacheze kwa kushirikiana kwani umoja ni nguvu utengano ni udhaifu na penye nia pana njia.

Twajua kucheza ugenini kuna ugumu wake. Kuzomewa na wenyeji na kufanyiwa mambo yasiyopendeza. Wachezaji wa Simba hawatakiwi kusikiliza maneno yasemwayo nje ya uwanja. Muhimu ni kucheza kwa bidii na ari wakiwa na shauku (hamu ya kutaka kupata ushindi) ya ushindi bila kujali kelele na kuzomewa. Hii ni kawaida kwa timu ngeni inapocheza ugenini kwa hiyo hakuna sababu ya wachezaji wa Simba kutetema wala kukata tamaa wanapokuwa uwanjani.

Watanzania tunapaswa kuwaombea dua maalumu wachezaji wa Simba ili wafanye kile kinachodaiwa kutowezekana mbele ya TP Mazembe ingawa yasemwa ni vigumu kuwashinda kwao. Hayo ni maneno ya kuwakatisha Simba tamaa kwani “hakuna mume wa waume.” Maana yake hakuna mtu mmoja anayeweza kuwashinda wanaume wenzake wote.

Methali hii huweza kutumiwa kwa mtu anayejitia ubabe au anayejidai kuwa na nguvu (kwa muktadha huu TP Mazembe) kama njia ya kumnyamazisha. Simba wanapaswa kuwa makini kulinda lango lao na wakati huohuo washambuliaji wajitume ipasavyo na kutokuwa na uchoyo kwa maana ya kila mmoja kutaka kufunga hata pale asipoweza kufanya hivyo.

Nawanasihi wachezaji wa Simba kutocheza kwa woga wala papara na uchoyo bali wacheze kwa ushirikiano na bidii wakifuata maelekezo ya walimu wao. Watambue kuwa wanaiwakilisha Tanzania na wananchi wake.

Hebu! (tamko la kumtaka mtu asikilize). “Kaa mkuu ng’ombe wa maji akiinua gando mwelemeze nanda.” Kaa mkubwa ni mfano wa ng’ombe, akiinua mguu mwelemeze kigongo cha panda.

Methali hii yatufunza kuwa hatupaswi kumdharau mtu mwenye uwezo au nguvu fulani katika mazingira yake hata kama anaonekana dhaifu na mnyonge. Pia hutumiwa kutunasihi kuwa yeyote mwenye nguvu anaweza kushindwa mradi tuwe na maarifa na mbinu.

Nawakumbusha Simba kuwa “Mja hatindi rehema ali hai duniani.” Maana yake binadamu hapaswi kukata tamaa akiwa bado anaishi. Methali hii hutumiwa kutunasihi tusikate tamaa katika mambo yoyote tuyafanyayo hata kama ni magumu kiasi gani; tuvumilie tu hatimaye tutafanikiwa.

Msema kweli ni mpenzi wa Mungu. Naweka wazi kuwa hapa nyumbani siipendi Simba inapocheza na timu yoyote ya Tanzania lakini inapopambana na timu ngeni kutoka nnje ya Tanzania, huwa upande wao (Simba) kwani damu ni nzito kuliko maji.

Kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzanua Bara, kati ya timu 20 zinazoshiriki, ni Simba pekee iliyofungwa mabao machache (7) ikilinganishwa na Yanga iliyo kileleni ambayo imecheza michezo 31, kufungwa mabao 22 na kufunga mabao 51.

Wakati Yanga ikipoteza michezo mitatu na kwenda sare mara tano, Simba imecheza mechi 22, kushinda michezo 18, kupata sare tatu, imefunga mabao 45 na kupoteza mchezo mmoja tu. Ina mechi tisa za viporo.

Hii yaweza kuwapa nguvu wachezaji wa Simba na kuwashitua TP Mazembe kuwafanya wacheze kwa wasiwasi. Hata hivyo Simba wanatakiwa kuwa makini sana kwani wachezaji wa TP Mazembe watacheza mchezo wa kushambulia zaidi.

Watumie nafasi hiyo kujilinda kwa makini na kushambulia kwa kushitukiza bila kujali ngebe (maneno mengi yenye jeuri) za wenyeji watakaokuwa wakiishangilia timu yao ya nyumbani.

Aombaye atapewa: “Nami nawaambia: Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa. Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. (Luka 11:9-10). Inshallah (apendapo Mwenyezi Mungu).

[email protected]
0784 334 096