Twajifunza nini tuhuma hizi za ujasusi ?

03Apr 2016
Ibrahim Mkamba
Nipashe Jumapili
NAWAZA KWA SAUTI
Twajifunza nini tuhuma hizi za ujasusi ?

HII ni hadithi ya kweli iliyotokea miaka 40 iliyopita huko KIlosa mkoani Morogoro. Machi na Aprili mwaka 1976, familia yetu iliyokuwa na marehemu wazazi wangu baba Mwalimu Jaffar Mkambda na mama yangu pamoja na ndugu zangu, ilitikiswa kwenye tukio la kihistoria lililogusa maisha yangu.

Nimeleta hadithi hii ya kweli kwa lengo la kueleza umakini uliokuwapo miaka hiyo ambao, kwa kiasi kikubwa umeondoka. Kadhalika nahoji? Kwa nini leo hatuko makini kama zama hizo tunapozingirwa na matatizo mengi yanayohusisha usalama ukiwamo ugaidi na wizi?

Baba yangu mzazi, marehemu Jaffar Mkamba, alikuwa mmoja wa waalimu wa Shule ya Msingi Ulaya wilayani Kilosa. Machi 1976 alifika shuleni hapo raia wa Uingereza Leeman inatamkwa Liiman, ugeni huo ukaleta sekeseke.

Liiman alitokea Zimbabwe zama hizo ikiitwa Southern Rhodesia, akipitia Zambia na kuingia Tanzania kwa basi. Alifika Mikumi na kutafuta usafiri wa kuelekea Kilosa uliomfikisha Shule ya Ulaya.

Mwalimu Mkuu wa Muhenda wakati huo, Mwalimu Maro, alimueleza kuwa Mwalimu Tesha, alikuwa mbali na hapo. Akashauriwa alale kwani hakukuwa na usafiri wa kumfikisha Ulaya muda huo.

Yule Mzungu alikakataa na kusema angetembea kwa miguu Aliambiwa njiani kulikuwa na hatari nyingi hasa wanyama wakali kama simba. Akaomba apewe silaha aendelee na safari Mwalimu Maro akampa mkuki na kuanza safari kwa miguu.
Alitembea usiku kucha na kufika Ulaya karibu na alfajiri na kupiga hodi nyumbani kwetu. Hapo shuleni kulikuwa na nyumba tatu za waalimu ya Mwalimu Mkuu Paschal Mlenga au Pam, ya waalimu Byabato na Tesha na ya kwetu .

Baba alipofungua mlango na kuwasiliana na mgeni huyo aliyesema anamtfuta Tesha, alimsindikiza kwa Tesha akimwambia kuwa hakuwapo kwani alikuwa Morogoro kuchukua mshahara wake. Akamkabidhi kwa Mwalimu Byabato ili aendelee kumkarimu mgeni akisubiri Tesha arejee.

Nakumbuka marehemu mama yangu alikuwa akimshauri baba kwenda kutoa taarifa ya ugeni huo kwenye ofisi za serikali lakini baba alikataa kwa maelezo kuwa hakupaswa kutolea taarifa mambo binafsi ya wengine na akasema Tesha ndiye mwenye mgeni na kwamba endapo itahitajika kuiarifu serikali kuhusu Liiman , Mwalimu Byabato ndiye wakufanya kazi hiyo.

Aliogopa kuonekana kama kamshtaki Mwalimu Tesha. Aliporudi safarini,Tesha akajulishwa kwamba yule Mzungu alikuwa mwalimu wake aliyemfundisha sekondari mkoani Kilimanjaro. Mwalimu huyo hakumripoti mgeni wake.

Mgeni huyo, aliyekuwa akiongea Kiingereza tu alipogundulika kuwapo bila serikali kuwa na taarifa zake, sekeseke lilianza. Waalimu wote wanne waliokuwa wakiishi shuleni hapo walihojiwa na polisi waliovaa sare, wasio na sare na maofisa wa serikali wa Kilosa, Morogoro na kutoka Dar es Salaam.Tuhuma ikiwa kumficha jasusi.

Shuleni Ulaya palikuwa panatikisika miezi kama hii miaka 40 nyuma. Hawa wanaingia, wale wanatoka. Nyumbani kwetu, tukitoka nje usiku kujisaidia tuliwaona waalimu wakihojiwa na mazungumzo yakiandikwa zikitumika taa za kandili na karabai kufanikisha kazi hiyo.

Wakati huo Liiman alishapelekwa Kilosa,baadaye Morogoro hadi Dares Salaam ambako sikujua hatma yake.
Kilichotokea wakati huo ni kwamba ulikuwa ni msimu wa harakati za ukombozi wa Afrika ulioongozwa na Tanzania.

Pili, Mzungu alikuwa ametokea Zimbabwe zama hizo ikiitwa Southen Rhodesia iliyokuwa kwenye agenda ya ukombozi na alikuja Tanzania, iliyokuwa mkombozi na kushukia Morogoro kulikokuwa na kambi ya Wapigania Uhuru wa ANC chama cha ukombozi wa Afrika Kusini iliyokuwa Mazimbu, ikifahamika kama Solomon Mhalango Freedom College. .Liiman alikuwa Mwingereza na nchi yake iliendelea kuing’ang’ania Rhodesia au Zimbabwe.

Uchunguzi wa kina uliendelezwa na maofisa wa serikali kutoka Dar es Salaam waliokuwa wakibadilika kila siku.
Waalimu waliotuhumiwa walisambazwa sehemu mbalimbali kwa uhamisho wa kujigharamia. Waliohamishwa walikuwa Mlenga aliyekuwa Mwalimu Mkuu, Tesha mwenyeji wa Niiman, Maro aliyetoa mkuki kwa Mzungu, baba yangu (Mkamba), Byabato aliyeishi na mgeni kwa wiki nzima.

Mpaka leo ikitimia miaka 40 sijui sababu ya seke seke hilo. Serikali ndiyo inalifahamu.
Baadaye, Ikulu ya Mwalimu Julius Nyerere ikawaona watuhumiwa wote kuwa hawana hatia na walirudishiwa tena shuleni kwa gharama za serikali, wakalipwa fidia kwa usumbufu na wakapewa uhuru wa kuhamishwa kwa malipo kwenda walikotaka Tanzania Bara.

Baba alibaki alipohamishiwa lakini kilichonisisimua kwa miaka yote hii 40 ni barua ya kumfutia tuhuma na wenzake kuandikwa na Ofisi ya Rais, Ikulu na si ofisi nyingine . Mwaka uliofuata wa 1977, ikazuka kesi ya mwenzetu Juma Zangira ya mambo hayo hayo ya ukombozi wa Afrika.
Tuwe pamoja wiki ijayo kujiuliza.