Twawaremba walemavu ili iweje?

10May 2016
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
Twawaremba walemavu ili iweje?

“KULIMA ni bangu, kazi ni tunga yataka mwengwangu wa kwenda na kuja. ‘Bangu’ ni faida au vita na ‘mwengwangu’ ni mwepesi. Maana yake kulima ni faida, kazi yataka mtu mwepesi wa kwenda na kurudi.

Ni methali yatukumbusha kuwa tutafaidika ikiwa tuko tayari kufanya kazi kwa bidii na juhudi.

“Elimu bila amali ni kama nta bila asali.” ‘Amali’ ni matendo au kazi. Maana yake elimu isiyo matendo ni kama nta ambayo haina asali.

Kuna tabia iliyozuka ya kuwadharau waandishi wa habari kwa kuwaita waongo, wambea, wachochezi, waganga njaa n.k. Ndo maana baadhi ya watu wakitakiwa kujibu tuhuma zinazowahusu huwa wakali na kukataa kujibu maswali wanayoulizwa.

Wengine hutukana matusi mazito na kuwafukuza waandishi! Kumbe wanapoulizwa hupewa nafasi ya kueleza upande wao ndipo mwandishi aweze kuandika habari sahihi kuhusu tuhuma zao.

Kwa upande mwingine, mwandishi mahiri apaswa kujua historia ya mambo mbalimbali si nchini mwake tu, bali hata nchi za n-nje. Bila hivyo, mwandishi huwapotosha wasomaji wasiojua historia au mambo yanayoendelea duniani.

Ndo maana waandishi hutakiwa kusoma magazeti na vitabu kadiri wawezavyo ili kujua matukio ya kila siku.

Nakumbuka miaka ile ya ukoloni, wanafunzi wa darasa la tano walijua majina ya viongozi wa nchi mbalimbali duniani na miji mikuu ya nchi zao. Kwa hiyo kipindi cha ‘quiz’ (jaribio la maswali au chemsha bongo), wanafunzi walijibu bila kumunyamunya (kutikisa midomo kama mtu anayetaka kusema au kucheka).

Soma sentensi hii: “Wadadisi wa mambo wanasema huenda leo Hillary akawa amejihakikishia ushindi wa tiketi ya chama chake cha Republican.”

Hillary Clinton ni mke wa Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton. Pia alikuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za N-nje wa Marekani katika kipindi cha kwanza cha Rais Barack Obama atakayemaliza muhula wake mwishoni mwa mwaka huu.

Hillary Rodham Clinton, kama walivyo Bill Clinton na Barack Obama, ni makada wa chama cha Democratic lakini mwandishi atwambia chama cha Hillary ni Republican! Haraka yote hii ya nini?

“Jijini Dar es Salaam, Yanga kinara wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 59 inasaka pointi tatu za kuzidi kujichimbia kileleni mwa ligi hizo (!). Kwani Ligi Kuu ziko ngapi mpaka mwandishi aandike ‘ligi hizo?’ U’wapi umakinifu?

“Pia anafahamu kuwa nyumba zilizotwaliwa si mbavu za mbwa wala vibanda, bali mahekalu ya umma.”

Jamani ‘hekalu’ si nyumba ya kulala bali ni jengo maalumu linalotumiwa na Mayahudi au Mabaniani kutekeleza ibada zao. Kwa ufupi ni nyumba za ibada ingawa waandishi wamezoea kuita majumba makubwa ‘mahekalu!’ Si sahihi.

“Tangu aingie madarakani na kauli yake mbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ na mbwembwe za ‘kutumbua majipu,’ Rais John Magufuli amevutia wengi, hasa wanyonge.”

Sina ubishi kwa hilo ila tatizo langu ni jinsi sentensi ilivyoandikwa. Ingekuwa: “Tangu Rais John Magufuli aingie madarakani na kauli mbiu yake ya ‘Hapa Kazi Tu’ na kutumbua majipu, amevutia wengi, hususan wanyonge.

Pia sidhani kama Magufuli ‘anapotumbua majipu’ ni ‘mbwembwe’ (mikogo, madaha) bali anatekeleza moja ya ahadi alizoahidi wakati wa kampeni.

“Ukimataifa wampasua kichwa Majabvi” ni kichwa cha maneno ya habari kwamba “Kiungo wa Simba, Mzimbabwe Justice Majabvi amesema kiu yao ya kutaka kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao inawapa hamasa ya kujituma zaidi ili waweze kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara.”

Kuhusu ‘kimataifa’ na sasa ‘umataifa,’ kuna msomaji aliyenitumia ujumbe ufuatao:

“Hongera kwa kutupa somo. Kuna maneno yanatumika ndivyo sivyo yaani ‘habari za kitaifa’ na ‘kimataifa.’ Huu ni upotoshwaji wa dhahiri. Taifa haliwezi kuwa ‘kitaifa.’

“Waelimishe wadau wa habari watafute maneno stahiki ya habari za ndani ya nchi na sio kuita taifa ‘kitaifa.’ --- 0718 074 139” Nakaribisha mchango wa wadau wa Kiswahili.

Kichwa cha habari katika gazeti hili kiliandikwa: “PPF yafunza wasiosikia 50.” Ni kawaida kusikia vipofu wakiitwa ‘wasioona,’ mabubu waitwa ‘wasiosema’ na viziwi kuitwa ‘wasiosikia.’ Kwa ujumla wao huitwa ‘wenye ulemavu’ badala ya walemavu!

Twajua ‘kiguru’ ni mlemavu wa mguu mmoja ambao humfanya atembee kwa shida. ‘Kikono’ ni mtu aliyelemaa mkono; mtu mwenye mkono uliokatika.
‘Mlemavu’ ni mtu ambaye ana kiungo cha mwili kisichofanya kazi yake sawasawa. Kwa nini wote wenye athari ya miili yao wasiitwe ‘walemavu’?

Karibuni kwenye mjadala huu.

Methali: Akutanguliaye chanoni hukuzidi tonge.
[email protected]
0715/0784 33 40 96