Ubakaji, ulawiti unaongezeka jamii, tuchukue hatua

11Dec 2022
Salome Kitomari
Nipashe Jumapili
Nawaza kwa Sauti
Ubakaji, ulawiti unaongezeka jamii, tuchukue hatua

LEO ni kilele cha siku 16 za kupinga ukatili duniani. Wadau wamekutana maeneo mbalimbali kupaza sauti dhidi ya vitendo vya ukatili ambavyo vinaumiza watu wote kwenye jamii.

Maadhimisho haya yanafanyika wakati matukio ya ulawiti na ubakaji wa watoto yanaongezeka kila uchao, kesi nyingi zinaelezwa kuishia polisi au mtuhumiwa anapopewa dhamana, familia zinakaa kuzungumza ili kuyamaliza kifamilia.

Aidha, baadhi ya vijana waendesha bodaboda wanadaiwa kuhusika na matukio hayo hasa wale wanaowabeba wanafunzi kuwapeleka shuleni, kiasi kwamba wako watoto wamefanyiwa ukatili na kuuzoea au kulazimishwa kuishi maisha ya mateso tangu wakiwa wadogo.

Kwenye shule za msingi na sekondari, matukio hayo yanaongezeka kwa watoto kufanyiwa hivyo na ndugu wa karibu ambao hulala nao wanapokaribishwa na mama, baba au mlezi anashtuka mtoto ameshaharibika.

Aidha, inadaiwa fedha inatumika kumaliza kesi hizo na wakati mwingine madawati ya jinsia yamelalamikiwa kuwa sehemu ya uharibifu, ambao sasa ni maumivu kwa jamii.

Unapokwenda maeneo ya starehe, utakutana na vijana wa kiume wa rika mbalimbali wanajiuza yaani wanaingiliwa kinyume cha maumbile na wanaume wenzao, huku wasichana wakiwa na uhusiano na wasichana au wanawake wenzao.

Vitendo hivi vinaua kizazi kwa kuwa idadi ya wanaume inaendelea kupungua kila siku, huku takwimu zilizopo zikionyesha wanaume ni wachache ikilinganishwa na wanawake, sasa linapotokea suala la ulawiti linapunguza idadi yao na kukiweka kizazi hatarini.

Inaelezwa kuwa mwanamume anapofanyiwa kitendo hicho, anatamani kuendelea kufanyiwa ndiyo maana wengi hujiuza ili kupata wa kumfanyia hivyo. Hili ni kosa kisheria na limekatazwa na kulaaniwa kwenye vitabu vitakatifu vya dini.

Utafiti mdogo uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Mashataka, ulibaini kuwa baadhi ya watuhumiwa wa makosa hayo wakiwa nje kwa dhamana, wanakimbia na wengine kuharibu ushahidi au kumalizana na wazazi ama ndugu wa mhanga wa vitendo hivyo.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Happy Msimbe, hivi karibuni alisema serikali imeanza mchakato wa kufanyia marekebisho Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, wanaanza mchakato wa makosa ya ubakaji na ulawiti kuondolewa dhamana.

Baadhi ya familia zinamaliza kesi hiyo nyumbani, inapotokea mzazi mmoja anashikilia kuendelea na kesi mahakamani anaitwa na kukalishwa na ukoo, ikiwamo kutengwa kama atakubali kuendelea na kesi.

Wengi wanaokumbwa na kesi hizi wanatoka familia maskini ambazo wakati mwingine kufuatilia kesi ni usumbufu na gharama, wakati mwingine wanakutana na usumbufu mkubwa polisi na hospitali na kuamua kubaki nalo moyoni.

Wanaoteseka ni watoto na wazazi wao ambao wametendewa ukatili huo, lakini hawana pa kukimbilia kwa kuwa kila eneo hakuna msaada na mwisho matukio huendelea kutokea.

Mabadiliko ya sheria hiyo kuongeza makali ni hatua nzuri sana kwa kuwa watu wataogopa na kesi zitashughulikuwa inavyotakiwa kwa kuwa ushahidi hautaharibiwa kama inavyofanyika sasa.

Ni muhimu kulinda taifa dhidi ya ongezeko la mashoga ambao wanakuwa hivyo siyo kwa msukumo wa maumbile, bali kwa kufanyiwa ukatili na wachache ambao wananufaika au ni tamaa za mwili.

Lakini ni muhimu kuendelea kutoa elimu na kuchukua hatua mapema taarifa zinapotolewa, kuboresha madawati ya jinsia ili yasiwe kichaka cha rushwa na kuumiza watu, viongozi wa dini walio waadilifu kuendelea kuwahubiri yaliyomema waumini wao na kuwaonya kwa kutumia maandiko matakatifu juu ya vitendo hivyo.

Sheria kufanyiwa mabadiliko ni jambo jema, lakini bila kudhibiti rushwa ni sawa na bure kwa kuwa watu wataendelea kufinyanga kesi za namna hiyo, ili kupata fedha kwa waliotenda pasipo kuona uharibifu huo ipo siku utabisha hodi kwenye nyumba yake.

Kwa sasa tuna Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum, ambayo imeunda kamati mbalimbali kukabili vitendo vya ukatili, lakini ni muhimu kufuatilia hadi ngazi ya chini hasa kwenye shule za msingi na sekondari, lakini kuimarisha idara ya ustawi wa jamii, polisi na hospitali ili wafanye kazi kwa hofu ya Mungu na kuogopa kuyaharibu matukio hayo.

Lazima jamii iwe wazi kwa kusema hapana kwa vitendo vya ukatili ambao unaelekea kuwa jambo la kawaida sana,mifumo ifanye kazi vyema,kamati za kupinga ukatili kuanzia ngazi ya mtaa zitekeleze wajibu wake.