Ubingwa Ligi Kuu uko wazi

09Mar 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ubingwa Ligi Kuu uko wazi

LIGI Kuu inakaribia tamati huku timu za Yanga, Azam na Simba zikiwa zimekaliana mguu-kausha kila moja ikiukodolea ubingwa wa msimu wa mwaka 2018/19. Ipi itatwaa ubingwa, ni swali lililo kwenye fikra za makocha, wachezaji, viongozi na wanachama wao bila kuwasahau mashabiki.

Ni vigumu kubashiri kwa uhakika timu itakayotwaa ubingwa msimu huu. Timu tatu zinazoongoza kwa wingi wa alama (pointi), yoyote yaweza kutwaa ubingwa endapo itakuwa makini katika mechi zilizosalia. Kabla ya mechi za Jumamosi hii, Yanga SC inayoishi kwa kudura (uwezo wa Mwenyezi Mungu) ndio inayoongoza. Imecheza mechi 26 ikishinda 20, sare 4 na kupoteza 2. Imefunga mabao 43 imefungwa 17 na kujikusanyia alama 64.

Azam FC inafuata katika nafasi ya pili ikiwa imecheza michezo 26 kama Yanga. Imeshinda michezo 15, sare 8 na kupoteza 3 ikifunga mabao 36 na kufungwa 17 kama Yanga. Ina alama 53 kwa maana ya alama 11 nyuma ya Yanga.

Simba iliyo kwenye nafasi ya tatu baada ya Yanga na Azam, leo inapambana na JS Saoura wa Algeria kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika. Watanzania tuache chuki zetu na kuitakia ushindi. Ligi ya nyumbani Simba imecheza mechi 20, imeshinda 16, sare 3 na kupoteza mchezo mmoja tu. Imefunga mabao 43, kufungwa 7 na kuwa na alama 51.

Simba imepitwa na Yanga na Azam kwa michezo sita. Kama ikishinda michezo hiyo ili kulingana na timu hizo mbili za juu, itakuwa na alama 61 ikibaki mechi moja (alama 3) tu kuikamata Yanga yenye alama 64. Ikishinda, itakuwa nafasi ya pili baada ya Yanga na kuishusha Azam kwenye nafasi ya tatu kwa alama 9.

Katika timu hizi tatu, kama Simba itakuwa makini na kucheza kwa bidii bila kutekwa na sifa zinazotolewa na mashabiki wake, na Yanga kupoteza mchezo mmoja, hapana shaka itarejesha ubingwa ilioutwaa msimu uliopita na kuwaacha Yanga wakikodoa!

Wakati Yanga imepoteza mechi mbili, Simba imepoteza mechi moja tu ilipofungwa na Mbao FC jijini Mwanza. Yanga imefunga mabao 43 katika michezo 26, Simba ina mabao kama ya Yanga (43) kwa michezo 20. Yanga imefungwa mabao 17 kati ya michezo 26 iliyocheza lakini Simba imefungwa mabao 7 tu katika michezo 20. Hii yadhihirisha ubora wa safu ya ulinzi ya Simba akiwamo mlinda mlango wao makini, Aishi Manula.

Kandanda ni mchezo wa kubahatisha. Timu yaweza kucheza vizuri sana lakini ikafungwa na timu isiyotarajiwa! Simba ilifungwa na Mbao FC jijini Mwanza hata kocha wao akatupiwa chupa za maji. Hao Mbao walioifunga Simba Kirumba, walifungwa mara mbili na Yanga. Kwanza uwanja wa Taifa Dar es Salaam kwa mabao 2-0 kisha uwanjani kwao Kirumba jijini Mwanza kwa bao 1-0.

Timu zilizoingia kwenye Ligi Kuu msimu huu nazo hazipo nyuma kwa kuzitikisa timu zoefu. Kwa mfano timu ngeni kwenye Ligi Kuu ya Bara, ya Manispaa ya Kinondoni (KMC) kabla ya mechi za leo ilikuwa nafasi ya nne baada ya Yanga, Azam na Simba. Timu ingine ngeni iitwayo Alliance ipo nafasi ya 6 kutoka juu. Timu hizo mbili – KMC na Alliance – zinacheza mchezo wa kuvutia na hunisikitisha sana zinapopoteza michezo yao. Mpira unadunda!

Nazisikitikia timu za African Lyon na Biashara United zinazoshiriki Ligi Kuu kwa mara kwanza msimu huu kwa kuwa nafasi mbili za mwisho pamoja na uchezaji wao mzuri. Katika jumla ya timu 20 zinazoshiriki Ligi Kuu msimu huu, Singida United nayo imepoteza makali yake na kuwa nafasi ya 18 kutoka juu na 3 kutoka chini!

Yapo madai kuwa sababu za uchezaji wa Singida United kushuka ni wachezaji na makocha wao kutolipwa mishahara yao na kufanya ulaji wao uwe wa shida kiasi cha kushindia ndizi mbivu! Kwamba hata siku timu hiyo ilipopambana na Tanzania Prisons ilishinda mabao 2-1 kwa tabu kwani wachezaji walicheza bila kunywa chai wala chakula cha mchana!

Baadhi ya wachezaji wengi wa kigeni wameikimbia timu huku kocha Goram Popadic na msaidizi wake, Dusan Momcilovic wakiupa uongozi wa Singida United mpaka tarehe 15 mwezi huu wawe wamewalipa mishahara na marupurupu ya mwezi Februari.

Popadic anasema mkataba wao ni pamoja na kupewa gari, mpishi na mhudumu wa usafi lakini hakuna kilichofanyika mpaka sasa. Anasema hata fedha za kulipia Bajaji kwenda uwanjani hawapewi! Hili ni tatizo sugu kwa timu za Tanzania kutaka ufahari na mambo makubwa wasiyoweza kuyatekeleza.

Wahenga walisema: “Ukimpa mtu kazi pataneni ujira kwanza.” Maana yake unapompa mtu kazi ya kufanya, lazima kwanza mpatane malipo na marupurupu mengine. Methali hii yatukumbusha kwamba twapaswa kuyazingatia mambo katika upana wake. Mathalan kabla hatujafanya jambo lolote twapaswa kufikiria matokeo yake kwanza.
[email protected]
0784 334 096