Uchafuzi huu makusudi wa mazingira unakera

10Jan 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Uchafuzi huu makusudi wa mazingira unakera

KATIKA baadhi ya maeneo ya jijini Dar es Salaam, imekuwa kama jambo la kawaida kukutana na harufu kali itokanayo na rundo la taka au majitaka yanayotiririka kutoka katika chemba za vyoo.

Mtu ukitembelea maeneo yanayoitwa ‘uswahilini’ ni kawaida kukumbana na hicho ninachokitaja na imezoeleka kwa wenyeji wa maeneo hayo, kana kwamba ndio tabia au utamaduni wao wa kila siku.

Lakini ukweli ni kwamba, ni hatari kuishi katika mazingira ya aina hiyo. Usahihi unaotakiwa ni kwamba, hata kama wahusika ni maskini, bado wanatakiwa kuboresha mazingira wanayoishi kwa ajili ya usalama wa afya zao.

Hali ya aina hiyo, ipo kando ya barabara ambazo baadhi ya watu wamekuwa wakitoa taka katika nyumba zao na kuziweka huko au kuzitupa kwenye mito, ili zizolewe na maji ya mvua.

Wakati hao wakifanya hivyo, baadhi ya watembea kwa miguu na abiria wa daladala, nao unakuta wakitupa taka ovyo tena bila wasiwasi kwamba watakamatwa.

Kwa mfano, mtu anatafuna mhindi au anakunywa maji, akimaliza anatupa bunzi lake, hata kama yumo ndani ya daladala, ambako hivi sasa kila moja ina vifaa vya kutunzia taka.

Yaani kwa ujumla, ni kwamba kila mtu anafanya anavyojua ndio maana taka zimekuwa zikitupwa ovyo, ikiwamo mifuko laini ya plastiki, inayotumiwa na kutupwa ovyo mitaani, kusababisha kero ya aina yake.

Sasa kama ndivyo hivyo, wakazi wa Dar es Salaam, katika hilo linalohusu usafi wao, wanapaswa kujifunza ustaraabu, wasigeuze kutupa uchafu kuwa utamaduni au tabia yao.

Ninatambua jinsi ambavyo serikali imekuwa ikifanya jitihada kubwa za kuboresha miundombinu ya barabara, lakini inaharibiwa na watu wachache ambao, kwao kuendekeza uchafu, wanageuza utamaduni wao.

Kwanini watu wasijitahidi kuliweka jiji katika hali ya usafi ili kuendana na hadhi yake ya kupendeza? Ina maana hata kufanya usafi, watu wafundishwe?

Unakuta baadhi ya watu wakitoa uchafu katika nyumba zao nyakati za usiku na kwenda kuutupa kwenye daraja la waenda kwa miguu au barabarani.

Yapo baadhi ya maeneo ambako kumewekwa vibao vyenye maandishi mahususi au onyo kwamba, ni marufuku kutupa taka maeneo hayo, faini yake ni Shilingi 50,000, lakini ajabu kinachofanyika ni kama onyo hilo limewapa ruhusa.

Ninasema hivyo, kwasababu nimewahi kushuhudia kibao chenye onyo kama hilo kimezingirwa na rundo la taka, huku watu wakiendelea kurundika zaidi bila ya hofu ya kutozwa faini.

Tabia ya kutozingatia usafi wa mazingira, inawafanya watu wengine kujisaidia haja ndogo kwenye mitaro pasipo aibu, tena mchana kweupe, wenafanya hivyo katika chupa za plastiki na kuzitupa.

Pia, kuna wanaojisaidia katika mifuko ya plasitiki wanayotupa vichochoroni. Hayo yote, kama nilivyosema awali, ni mazingira ya kupitwa na ustaarabu.

Ninachojua ni kwamba, suala la kujisaidia ni faragha na ndio maana. mtu anafanya hivyo iwe haja kubwa au ndogo, katika faragha rasmi ambayo ni chooni,. anakofunga mlango asionekane au kusikika, wakati huo.

Lakini sasa, wanapotokea watu wanaoamua kuweka ustaarabu kando na kufanya mambo wanavyotaka, basi kuna haja ya kuwaelimisha wawe wastaarabu.

Mtu anayejisaidia katika chupa au ndani ya mfuko wa plasitiki na kisha kuitupa mitaani, hawezi kuona aibu kuchukua taka nyumbani kwake na kwenda kuzitupa vichochoroni, kwenye mto au barabarani.

Kwa hali ilivyo, ni vyema halmashauri husika zikatumia sheria ndogo ilizo nazo za afya na mazingira, kwa ajili ya kukabiliana na watu wa aina hiyo, ambao suala la uchafuzi wa mazingira kwao wanalirahisisha sana.

Pia, ni muhimu kutenga maeneo rasmi kwa ajili ya wamachinga ili waweze kufanyia shughuli zao, kuliko kuendelea na utaratibu wa sasa, ambao kwa namna moja au nyingine unachangia katika uchafuzi wa mazingira.

Hiyo ndio hali halisi ya Dar es Salaam, huenda na kwingineko ambako kimsingi, serikali inatumia fedha nyingi kuboresha mazingira yanayoharibiwa na watu wasiozingatia usafi wa mazingira.