Uchaguzi mkuu Malawi umekuja na funzo hili

08Jul 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Uchaguzi mkuu Malawi umekuja na funzo hili

MWAKA 1994 ulikuwa mwisho wa utawala wa miaka 30 wa chama kimoja cha Malawi Congress Party (MCP) cha Rais wa kwanza, Dk. Haustings Kamuzu Banda baada ya uchaguzi ndani ya mfumo wa vyama vingi.

Katika uchaguzi huo, Chama cha United Democratic (UDF) cha Bakili Muluzi, kiliibuka na ushindi, ambapo tangu wakati huo, MCP imeendelea kuwekwa pembeni hadi hivi karibuni ilipoibukia kwa kishindo.

Chama hicho kilicholeta uhuru wa Malawi mwaka 1964 kiliwekwa pembeni baada ya kutawala miaka 30. Kilitupwa nje kwa miaka 26 hadi uchaguzi wa hivi karibuni, ambao umekiwezesha kurudi madarakani kwa mara nyingine tangu walipokiondoa mwaka 1994.

Kimsingi wananchi wa Malawi walikuwa na sababu za kukiweka pembeni chama hicho, kutokana na uongozi wa mwanzilishi wake, Dk Banda, kwenda kinyume na matarajio yao.

Historia inaonyesha kuwa kiongozi huyo aligeuka kuwa kibaraka wa Wazungu na kuwaacha viongozi wenzake wa Afrika na pia kugawa wananchi wake na hivyo kusababisha matabaka na utengano.

Vitendo hivyo na vingine vingi vilisababisha yeye na chama chake kuchukiwa hadi kufikia kukiondoa madarakani kwa njia ya kura ingawa sasa kimerudi upya kutawala nchi hiyo kikiwa chini ya Rais Lazarus Chakwera.

Kitendo cha wananchi wa Malawi kukirudisha chama hicho madarakani, ni wazi kwamba, hata vyama vya upinzani barani Afrika vina la kujifunza kutokana kile wapigakura walichokifanya.

Jambo la kujifunza ni kwamba, kwa nyakati tofauti, vyama vya upinzani vimepewa ridhaa kuongoza nchi hiyo, lakini wananchi wameamua kukirudisha kinara wa uhuru.

Hivyo wapinzani nchini na Afrika wanatakiwa kujifunza kwa yale yalitokea Malawi ili wanapotafuta ridhaa ya kuongoza nchi, wasifanye makosa yatakayoleta kutimuliwa.

Hapa maana yake ni kwamba, chama kilicholeta uhuru kimejifunza kutokana na makosa na kujirekebisha, kisha kikaomba tena ridhaa kwa wananchi nao wakaamua kukipa kibali cha kuiongoza nchi.

Mbali na hilo, yawezekana kuna udhaifu uliofanywa na vyama ambavyo viliwahi kuitawala nchi hiyo na kusababisha MCP kupata upenyo wa kukiwezesha kujenga na hatimaye kupata ushindi.

Hivyo wakati upinzani ukimimina salamu za kumpongeza rais mpya wa nchi hiyo kwa ushindi, ni vyema pia wakawa na la kujifunza hasa kile kilichokirudisha chama tawala madarakani baada ya kukaa nje kwa miaka 26.

Yawezekana wananchi wa Malawi wameona ndani ya vyama vyote ambavyo vimewahi kuiongoza nchi hiyo tangu mwaka 1994, hakuna lolote, ndipo wakaamua kurudi kwenye chama chao cha zamani.

Baadhi ya watu wanaweza kudhani kwamba chama ambacho kimeshinda uchaguzi wa Malawi ni kipya, lakini ukweli ni kwamba ni kikongwe kilicholeta uhuru wa nchi hiyo.

Kwa kawaida chama kikishindwa katika uchaguzi, kinakuwa cha upinzani huku kilichoshinda kikiwa ni chama tawala, hivyo hata MCP kilikuwa tawala, kisha cha upinzani baada ya kushindwa na sasa ni chama tawala.

MCP inarudi madarakani kurekebisha changamoto zilizofanywa na viongozi waliowahi kuiongoza nchi hiyo tangu upinzani uliposhinda uchaguzi mkuu wa mwaka 1994.

Siyo vibaya kujifunza kwa vyama vingine ambavyo vilifanikiwa kupata ushindi na sasa vinaendelea kuongoza nchi, na wananchi wanaendelea kuviamini bila kujali kwamba kulikuwa na chama kilicholeta uhuru.

Kwa mfano tangu kuangushwa kwa chama cha kijamaa kilicholeta uhuru wa Zambia cha United National Independence Party (UNIP) tangu mwaka 1991 cha Baba wa Taifa Dk. Kenneth Kaunda, hadi leo kiko pembeni, kwa miaka takribani 30.

Kutofurukuta kwa chama cha Kaunda ni wazi vyama mbalimbali ambavyo vimekuwa vikishinda uchaguzi mkuu wa Zambia kwa nyakati tofauti vinafanya kile ambacho Wazambia wanakitaka.

Kwa hiyo wapinzani na vyama tawala Afrika wafahamu kuwa kitokea wakishika madaraka, kuna uwezekano wa kushindwa iwapo watakwenda kinyume na matarajio ya wapigakura.