Uchaguzi wa marudio usiwe hatma ya `kusaka’ utulivu Zanzibar

23Mar 2016
Mashaka Mgeta
Nipashe
Mtazamo Yakinifu
Uchaguzi wa marudio usiwe hatma ya `kusaka’ utulivu Zanzibar

UCHAGUZI wa marudio Visiwani vya Zanzibar, ulifanyika Machi 20, mwaka huu ili kuwapata Rais, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani.

Ni uchaguzi uliowagawa Wazanzibari, kiasi cha kuhatarisha amani, umoja na mshikamo miongoni mwa Watanzania wa Zanzibar.

Ingawa iko hivyo, wapo wanaoweza kuamini kwamba, tamko hilo hapo juu ni sehemu ya uchochezi, la hasha! Kwa hali ilivyo sasa, Zanzibar haihitaji uchochezi, Wazanzibari hawapaswi kuchochewa ili washiriki kutenda yaliyo maovu.

Hali ilivyo sasa, inahitaji umma kushiriki katika kuwarejesha Wazanzibar pamoja. Wajitambue katika udugu uliopo, utu na haki sawa kwa kila mmoja. Hivyo, ninavyoelezea kuhusu hatari dhidi ya amani, umoja na mshikamano ni kutokana na viashiria kadhaa vilivyopo.

Mosi, ni mzozo uliodumu tangu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (Zanzibar (ZEC), Salum Jecha kutangaza kufutwa kwa matokeo na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana.

Jecha alifikia hatua hiyo iliyokosolewa na baadhi ya kada, wakiwamo wanasheria, lakini tamko lake likaendelea ‘kuishi’ hadi uchaguzi wa marudio ulipofanyika.

Pili, kujiondoa kwa chama kikuu cha upinzani, Chama Cha Wananchi (CUF) kutoshiriki uchaguzi wa marudio kukabomoa daraja lililowaunganisha wapinzani na watawala visiwani humo.

Ikumbukwe kwamba, kwa miongo kadhaa sasa, siasa za Zanzibar zinazojikita pia katika uasili wa raia, zimeghubikwa na tofauti zenye kuibua vurugu za kabla, wakati na baada ya Uhuru. Historia ya uhalisia huo ni ndefu.

Sasa inapotokea chama kikuu cha upinzani kama CUF kujiondoa katika mchakato wa kidemokrasia pasipo kutokana na ridhaa yao, isipokuwa kupinga kile kinachoaminika kuwa ni ‘kusigina’ misingi ya utawala bora, si jambo jema.

Inawezekana walio kwenye vyama vingine visiwani Zanzibar hususan Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakashangilia, wakafurahia, wakajipongeza na kuamini kwamba ‘wameuweza’ upinzani. Si kweli.

CUF ina wanachama wengi katika Zanzibar. CUF ina wafuasi wengi katika Zanzibar. CUF ina mizizi thabiti katika siasa za Tanzania na ndio maana hata katika Bunge la Jmahuri ya Muungano, lina wanachama walioshinda nafasi za uwakilishi wa umma.

Chama hicho kinapojiondoa kwa ‘shinikizo’ lisilo rasmi, kikajiweka kando dhidi ya uchaguzi wa marudio, si dalili nzuri kwa ustawi wa Wazanzibari na maendeleo ya visiwa hivyo.

Sasa ni dhahiri kwamba baada ya matokeo ya uchaguzi wa marudio kutangazwa, sehemu kubwa ya washindi itatoka CCM na pengine, vyama vingine vikiwamo vilivyoshindwa hata kumudu kumiliki ofisi ya chama!

Zipo dalili nyingi zinazoashiria kutokuwapo mazingira bora yanayochagiza amani, umoja na mshikamano Zanzibar. Yakiandikwa kwa ujumla wake, gazeti hili haliwezi kutosha kwa nafasi.

Lakini itoshe kueleza kwamba misingi bora ya kikatiba na sheria za nchi, vinatoa fursa kwa raia halisi wa Tanzania kuwania nafasi za uongozi na uwakilishi wa watu, ili mradi anakidhi matakwa ya sheria.

Miongoni mwa matakwa yaliyo makuu katika hilo ni kuwa raia halisi wa Tanzania. Kwamba katika sifa zote zinazoanishwa kwa mtu kuongoza au kuwawakilisha wananchi, lazima awe raia wa Tanzania.

Kwa hiyo, Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wake haiwezi kuongozwa na raia wa nje, awe anatokea Burundi, Rwanda, Kenya, Ujerumani, Pakistan au kwingineko katika pande zote za dunia, bali Mtanzania halisi.

Kama hali ipo hivyo, tofauti pekee iliyo kubwa kwa wanaotafuta uongozi ama uwakilishi wa wananchi ni njia wanayoitumia kufikia lengo hilo.

Njia hiyo ni kupitia vyama tofauti vya siasa ambavyo sasa, vinaonekana kuthaminiwa, kutukuzwa, kuheshimiwa kuliko hata utaifa.

Watanzania wakiwamo Wazanzibari, kama ilivyo sehemu nyingine za Afrika wapo tayari kumuathiri ‘ndugu wa damu’ ili mradi tu awe anaaminika katika itikafi ya chama kingine .

Tunapoiangazia Zanzibar na kama nilivyoeleza awali, makovu yaliyosababishwa na tofauti za kisiasa visiwani humo, yanapaswa kufutwa. Kukamilika kwa uchaguzi wa marudio kusiwe sababu ya kubweteka na kuwaacha Wazanzibari wakisambaratika.

Kukamilika kwa uchaguzi wa marudio kunapaswa kuwa sehemu muhimu kwa wadau husika kuisaka amani na utulivu wa Zanzibar, vinginevyo chuki, uhasama na aina nyingine za mafarakano haviwezi kuwa vyenye tija kwa nchi na watu wake.

Kwa maana hiyo, ni wazi kwamba, mathalan Mtazania anayeishi Pemba akiwa mwanachama wa CCM, hana tofauti na Mtanzania wa eneo hilo aliye katika CUF.

Mfumo wa maisha, mahitaji yao, eneo la kijiografia wanalolitegemea na rasilimali zilizomo havitofautiani.

Pamoja na ukweli kwamba kila chama cha siasa kinatafuta mamlaka ya kuongoza na kuwakilisha, msingi wake unapaswa kuwa katika utaifa.

Kwamba mwenye nia na utashi wa kuifikia hatua hiyo awe mzalendo mwenye fikra na utayari wa kulifanya kusudio hilo kuwa na endelevu kwa yeyote mwenye sifa na akakubalika kwa wananchi.

Fitina, chuki, uchochezi ama aina yoyote inayojenga taswira ya kupora haki za baadhi, ama kuhamasisha ukiukwaji wa sheria na taratibu stahili, haviwezi kuwa mambo yenye tija kwa nchi na watu wake.

Huko ni kuliangamiza taifa na kuweka mianya kwa wasiokuwa na nia njema kuihujumu nchi.

Uchaguzi wa marudio umefanyika, mamlaka na wadau husika wasiyachukue matokeo yake kuwa ni hatima ya mafarakano yaliyopo Zanzibar. Amani na utulivu vinapaswa kutafutwa kwa hekima na busara ili kulifanya eneo hilo lililo ndani ya Jamhuri ya Muungano kuwa mahali salama pa kuishi.

Kutumia uwezo wa aina yoyote, uwe unaotokana na ushawishi kwa nguvu za umma ama matumizi ya dola haviwezi kuiokoa Zanzibar na Tanzania kwa jumla.

Nchi isibwete. Watu waje pamoja, wazungumze ili amani na utulivu viwepo kwa uhalisia wake visiwani Zanzibar.

Mashaka Mgeta ni mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii. Anapatikana kupitia simu namba +255 754691540, 0716645612 ama barua pepe:[email protected] au [email protected].