Ucheleweshwaji adhabu TFF unapeperusha haki

18Feb 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ucheleweshwaji adhabu TFF unapeperusha haki

WANASHERIA wana msemo wao unaosema kuwa 'haki si tu itendeke, bali pia ionekane imetendeka.'

Ukiusoma kijuujuu unaonekana kama hauna maana sana na badala yake ni mbwembwe tu za wanasheria, lakini ukitulia utaelewa wana maana gani.

Na hata mtu anayepata adhabu ni lazima imuathiri, imuume ili siku nyingine asifanye tena.

Adhabu maana yake si kumkomoa mtu. Ni kwamba amefanya makosa ambayo anatakiwa apate uchungu ili ajutie na siku nyingine asirudie tena.

Kwa siku za karibuni naona kama Kamati za Shirikisho za Soka nchini (TFF), zilizowekwa kufanya kazi zake za kuadhibu wachezaji au kudhibiti wasifanye mambo yasiyo ya kistaarabu uwanjani, hazifanyi kazi zake vizuri.

Zinaonekana kujichanganya, kwa kuchelewa kutoa maamuzi, huku wengine maamuzi yao yakiwa ya papo kwa papo.

Kuna baadhi ya wachezaji wanapofanya makosa, basi haraka Kamati ya Saa 72 inafanya kazi yake bila kuchelewa, pamoja na Kamati yake ya Nidhamu, lakini kuna baadhi ya wachezaji wanapofanya makosa inashikwa na kigugumizi.

Nakumbuka misimu miwili iliyopita Kamati ya Saa 72 ilimsimamisha beki Abdi Banda wa Simba kwenye mechi dhidi ya Kagera Sugar siku moja tu baada ya mechi kumalizika.

Si hao tu, kuna baadhi ya wachezaji wengi ambao walikubwa na rungu la kusimamishwa muda mfupi baada ya kufanya makosa.

Hao ni Kelvin Yondani wa Yanga kwa kosa la kumtemea mate Asante Kwasi kwenye mechi ya watani wa jadi iliyochezwa Aprili 29, mwaka jana katika Uwanja wa Taifa ya msimu wa mwaka 2017/18.

Wengine ni James Kotei alipelekwa Kamati ya Saa 72 kwa kosa la kumpiga ngumi mchezaji wa Yanga, Gadiel Gabriel dakika ya 32 tukio ambalo mwamuzi hakuliona, pia Andrew Vincent wa Yanga alimpiga kichwa Mohamed Hussen 'Tshabalala' wa Simba na adhabu zao ilikuwa ni kufungiwa mechi tatu na faini ya milioni moja kwa kila mchezaji. Hata Erasto Nyoni na Hassan Dilunga imeshawahi kuwatokea. Hao ni baadhi tu.

Lakini inapokuja suala la mchezaji mwingine anafanya kosa, hasimamishwi bali anaendelea kucheza, tena hadi mechi mbili ndiyo anapelekwa, halafu inaonekana inaahirishwa-ahirishwa, haitendi haki.

Inaonekana kana kwamba hawa wachezaji wana matabaka. Kuna wachezaji wanagushwa na wengine hawaguswi, bali wananyenyekewa.

Beki wa Yanga, Abdallah Shaibu 'Ninja' alimpiga kiwiko mchezaji Ayoub Lyanga kwenye mechi dhidi ya Coastal Union na tukio hilo kutoonwa na mwamuzi, yeye hajasimamishwa na amecheza mechi nyingine dhidi ya Singida United, pia dhidi ya Simba.

Inawezekana akaadhibiwa baada ya mechi hizo. Hapo ndipo ninapojiuliza inakuwaje wachezaji wengine wasimamishwe baada ya tukio na wengine waendelee hadi kucheza mechi mbili? Hii si halali na wala 'fair play' ambayo Fifa wanataka.

Fifa waliweka adhabu hizi ili wachezaji wajutie na wasirudie tena makosa. Adhabu inatakiwa impe uchungu mchezaji na iiathiri klabu yake ili watafute namna ya kukaa na kufundisha nidhamu mchezoni ili kutorudia makosa wanayoyafanya.

Sasa kama Ninja alifanya kosa na akaendelea kucheza mechi zilizofuata, hakuna umuhimu wowote wa kumfungia ila kumuacha tu.

Duniani kote mchezaji anapofanya makosa na kuadhibiwa, anatakiwa kutocheza mechi zinazofuata na si kuachwa acheze mechi moja, mbili au tatu, ndiyo afungiwe, labda awe anachunguzwa na vyombo husika.

Sasa inakuwaje Kamati za Kibongo ziwe zinawafungia 'fasta' tu wanapofanya makosa, na wengine kuwaacha kwanza wacheze baadhi ya mechi wakati kanuni ni zile zile na ligi ni ile ile? TFF na kamati zake ilitafakari hilo.