Ugeni wa Rais Magufuli Nanenane Simiyu uchagize ununuzi wa pamba

30Jul 2019
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ugeni wa Rais Magufuli Nanenane Simiyu uchagize ununuzi wa pamba

TAARIFA za hivi karibuni kutoka kwa vyombo vya habari kwamba Rais John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima (Nanenane) mkoani Simiyu, zimemvutia Muungwana pia.

Kwa mujibu wa Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, maadhimisho ya sikukuu hiyo yanayoanza Agosti Mosi katika kanda zote nane nchini yakiwa ni maadhimisho ya 26 tangu kuanzishwa kwake, yatafunguliwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Aidha, kwa mujibu wa taarifa hiyo, maadhimisho hayo yanayofanyika katika viwanja vya Nyakabindi, Bariadi, vilevile yatatembelewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Agosti 3, ambaye atapata fursa ya kuona shughuli mbalimbali za wadau.

Muungwana anasema amevutiwa na taarifa hizo kwa sababu Rais Magufuli anakuwa mgeni rasmi katika kilele cha sikukuu hiyo ya wakulima mkoani Simiyu, katika kipindi ambacho wakulima wa zao la pamba bado wana kilio.

Wana kilio kwa sababu wengi wao wanaendelea kukabiliwa na  changamoto ya kutonunuliwa kwa pamba yao takribani miezi mitatu sasa tangu msimu wa ununuzi wa zao hilo ulipozinduliwa Mei 2 mwaka huu.

Taarifa kutoka maeneo kunakolimwa pamba na hasa Kanda ya Ziwa, ukiwamo mkoa wa Simiyu ambako Rais Magufuli atakuwa mgeni rasmi katika kilele cha Nanenane zinaonyesha kwamba wanunuzi wa pamba ni kama ‘wanapiga chenga.’

Kwamba pamoja na serikali kutoa kauli rasmi kupitia kwa Waziri Mkuu katikati ya mwezi huu kwamba kufikia Julai 30 pamba yote iliyoko katika mikoa inayolima zao hilo itakuwa imenunuliwa na wakulima wote kulipwa fedha zao, bado uhalisia wake hauko hivyo.

Muungwana anasema hivyo kwa sababu kwa mujibu wa taarifa kutoka maeneo mbalimbali, pamba bado imejaa kwenye bohari za Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS), kiasi kwamba nyingine ilikuwa inahifadhiwa nje.

Hata hivyo, pamba hiyo iliyoko kwenye bohari za AMCOS ni chache ikilinganishwa na ile ambayo bado iko majumbani kwa wakulima.

Ni kweli kwamba baada ya kauli ya serikali, baadhi ya kampuni zinazonunua zao hilo zimekuwa zikipeleka fedha kwenye vyama vya msingi, lakini kiasi kinachopelekwa ni kidogo, ikilinganishwa na pamba iliyokusanywa ambayo bado haijalipiwa.

Baadhi ya viongozi wa AMCOS wamemtaarifu Muungwana kwamba wanunuzi wanapeleka fedha kulingana na kiasi cha pamba ambayo tayari wameisafirisha kuipeleka kwenye viwanda vya kuchambua pamba kutoka AMCOS.

Na ndiyo maana hadi sasa vyama vingi vya msingi vinadaiwa na wakulima waliopeleka pamba yao kwenye bohari za vyama hivyo, huku wanunuzi wakiendelea kupeleka kiasi kidogo cha fedha kwa sababu ambazo hajazibainika.

Hili linatokea wakati ambapo Mwenyekiti wa Chama cha Wanunuzi Binafsi wa Pamba akiwa ameahidi mbele ya Waziri Mkuu kwamba baada ya serikali kukubali kuwadhamini wanunuzi ili wapate mikopo kutoka benki, wangenunua pamba yote ya wakulima.

Aidha, kuna taarifa kwamba kwenye baadhi ya vijiji, wanunuzi hawajafika kabisa hadi sasa na hivyo kufanya wakulima waendelee kubaki na pamba yao majumbani hadi sasa.

Na kutokana na kwamba siku zimeendelea kukatika bila ufumbuzi hadi sasa, baadhi ya wakulima walikuwa wameamua kupeleka pamba yao kwenye bohari za AMCOS, walau ikakae huko hadi pale fedha zitakapopelekwa.

Hatua hiyo ndiyo iliyosababisha baadhi ya bohari kujaa, na hivyo pamba nyingine kuhifadhiwa nje.

Ni vizuri kwamba baadhi ya wakuu wa wilaya akiwamo wa Maswa, waliingilia na kuzuia wakulima kupeleka pamba kwenye bohari za Amcos, wakati hakuna fedha za kuwalipa.

Wakati Rais Magufuli akiwa mgeni rasmi kwenye kilele cha Maadhimisho ya Sikukuu hii ya Wakulima, Muungwana anatoa rai kwake kutatua sintofahamu hii, ili pamba yote ya wakulima inunuliwe.

Anatoa rai kwake akichukulia ukweli kwamba yeye ni mtu wa vitendo na mtetezi wa wanyonge wakiwamo wakulima wa pamba, kama alivyo kwisha jibainisha.