Uingereza ratiba hadharani, TFF isisubiri kabla ya wiki

17Jun 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Uingereza ratiba hadharani, TFF isisubiri kabla ya wiki

KIZURI huigwa, hata kama kinafanywa na adui yako, au mtu ambaye humkubali. Na kwa Tanzania hatutaki ama tunazembea kujifunza kutoka kwa wenzetu wa nje walioendelea hususan katika sekta ya michezo.

Hasa kwenye nyanja za soka, tunapaswa kuangalia na kufuata mifano na mifumo ya klabu na vyama vikubwa vilivyoendelea barani Ulaya.

Nchini England msimu wa Ligi Kuu 2018/19, ulimalizika Mei mwaka huu, kama ilivyokuwa kwa Ligi Kuu nchini Tanzania. Tofauti ilikuwa ndogo tu kuwa Bongo ilimalizika mwishoni mwa mwezi huo.

Katika hali inayoonyesha kuwa jamaa hao wa England hawana masihara, tayari wameshatoa ratiba yao ya msimu ujao.

Ijumaa ya Agosti 9, mwaka huu, shughuli itaanza upya kwa Liverpool itakapokuwa nyumbani dhidi ya Norwich City.

Jumamosi ya Agosti 10, West Ham itacheza na Manchester City, AFC Bournemouth itapambana na Sheffield United, Barnley itacheza dhidi ya Southamton, Crystal Palace itaanza na Everton, Leicester City dhidi ya Wolverhampton, Watford dhidi ya Brighton, Tottenham itacheza na Aston Villa na Jumapili ya Agosti 11, Newcastle United itakumbana na Arsenal, huku Manchester United ikiiva Chelsea.

Ratiba hii imetoka mwezi mmoja na kitu kabla ya ligi yenyewe kuanza na hata kabla klabu hazijaita wachezaji wao kwa ajili ya kuanza maandalizi ya msimu mpya.

Cha kufurahisha zaidi ni kwamba wameweka mpaka saa za kuanza mechi hizo. Hili na mengine, ndiyo yanayowafanya wenzetu kuwa mbele na kufanya ligi yao ipendwe kiasi cha kufuatiliwa na watu wengi, pamoja na kupata wadhamini kibao.

Hili ni jambo la mfano wa kuigwa kwa Shirikisho la Soka nchini (TFF), ambalo mara nyingi limekuwa likilalamikiwa kwa kushindwa kupanga baadhi ya mipango yake sawasawa. Mara nyingi tumeshuhudia TFF ikishindwa kutoa ratiba kulingana na wakati. Wakati mwingine imekuwa ikitoa ratiba vipande vipande na mambo mengine mengi.

Kwa sasa siwalaumu sana kwa sababu viongozi wao na hata baadhi ya watendaji wakuu watakuwa bize na Afcon, lakini itakapomalizika hakutokuwa tena na hoja ya kujitetea badala yake kujifungia ndani na kutengeneza ratiba.

Tena ratiba yenyewe ili nzuri itakayozingatia mambo mengi ikiwamo ushiriki wa timu nne kwenye mechi za kimataifa msimu ujao ili kusiwe na utitiri wa viporo, kama vile haitoshi iwe ya usawa na si timu moja kuanza mechi nne mpaka tano nyumbani au ugenini tupu.

Faida ya ratiba kutoka mapema kama kwa wenzetu ni kwamba, tayari kila mmoja anakuwa anajua anakwenda kucheza na nani. Hii inawapa makocha kutengeneza mbinu ya kwenda kumkabili mpinzani wake, kwa sababu kila mmoja anakuwa na aina ya mfumo wa timu anayokwenda kucheza nayo.

TFF si vibaya kuiga hili. Hatutaki kuona hadi timu zinaanza maandalizi ya msimu mpya hazijui ni lini ligi itaanza, achilia mbali ratiba.

Tumechoka kuona ratiba inatolewa kwa kushtukiza, yaani wiki moja au mbili kabla, na kuzifanya timu kukurupuka na kuanza safari kwa zile zinazotakiwa zikacheze mbali ya vituo vyao.

Wakati mwingine kipindi hicho baadhi ya timu zinakuwa nje ya nchi kwa ajili ya maandalizi ya msimu, zinalazimika kukatisha na kurejea haraka.

Ratiba za aina hiyo za Kibongo zinakuwa haziwapi makocha wakati muafaka wa kuwaandaa wachezaji wao kwa mfumo ambao itakwenda kucheza na timu pinzani.

Mfano, Polisi Tanzania inapangiwa na Yanga, ratiba inatoka wiki moja kabla, kocha hatoweza kuwatengeneza wachezaji kukabiliana na timu hiyo, pia Namungo ukiishtukiza kucheza na Simba wiki moja kabla huku kocha wao akiwa bado hajaweka mfumo wa kuizuia timu hiyo ni matatizo matupu.

Ratiba ikitoka mapema na kuwa nzuri inasababisha vitu vingi kwenda kama inavyotakiwa, kila mmoja akitimiza majukumu yake na hata TFF yenyewe itakwepa zile lawama inazotupiwa ambapo wakati mwingine si za kwao, lakini zingine ni za kujitakia wenyewe.