Ujumbe wa MO uwafikie wasiojitambua Simba

11Feb 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ujumbe wa MO uwafikie wasiojitambua Simba

WAKATI mwingine Mwenyezi Mungu anaweza kukupa neema, halafu ukaichezea mwenyewe na kujikuta ikikuponyoka.
Inapoondoka, mtu anaanza kupiga kelele kuwa kuna watu wabaya wamemsababishia matatizo, kumbe yote ameyataka mwenyewe.

Baada ya mechi ya Kombe la SportPesa kati ya Simba dhidi ya Bandari Kenya, zikazuka habari kuwa baadhi ya wachezaji wa Simba walitoroka kambini usiku na kwenda kwenye starehe kabla ya mechi hiyo.

Kwenye mechi hiyo, karibuni nusu nzima ya wachezaji wake walicheza chini ya kiwango na kusababisha kufungwa mabao 2-1.
Wanachama na mashabiki wa Simba walionekana kuchukizwa na kilichotokea, ingawa hakuna kiongozi yeyote wa klabu hiyo aliyejitokeza na kukiri kuwa jambo hilo lipo.

Hata hivyo, kitendo cha kumteua meneja mpya, Patrick Rweyemamu, ambaye alianza kazi mara moja, inaonyesha kuwa lililosemwa lipo.

Rweyemamu aliyewahi kuwa meneja wa timu hiyo, amepewa umeneja huo akimrithi Richard Robert aliyesimamishwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwa kile kilichoelezwa kuwazuia wachezaji wa Simba kuingia kwenye kambi ya Taifa Stars.

Kabla ya kuteuliwa, Mratibu wa Simba, Abbas Ally, ndiye aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo na inaelezwa kuwa hakuwa na meno yoyote ya kuwazuia wachezaji wa timu hiyo kutoroka usiku kwa raha zao.

Zipo taarifa zinadai kuwa mpaka Simba imeshtuka, tayari wachezaji wa timu hiyo walikuwa wameshatoroka zaidi ya mara tano.

Mchezaji yeyote awe Mtanzania au wa kigeni, kitendo cha kutoroka kambini wakati timu yake inajiandaa na mechi au mashindano ni cha kutojitambua. Soka lina miiko na maadili yake kama kazi zingine zozote.

Kitendo cha kutoroka kambini na kwenda kwenye kumbi za starehe na kurejea alfajiri, si tu kwamba zinasababisha mchezaji asiweze kufanya kazi yake kwa ufasaha uwanjani, lakini pia kinaweza kumsababishia majeraha, vile vile mchezaji anaweza kupata matatizo alikokwenda bila taarifa.

Soka ni mchezo wa kutumia nguvu, hivyo mchezaji ambaye hajapumzika vizuri, kunywa pombe na kufanya mambo mengine yasiyo na maana ni lazima atacheza chini ya kiwango.

Nakubaliana na Mwekezaji wa Klabu ya Simba, Mohamed "Mo" Dewji, ambaye amesema hawatokuwa na msamaha wowote wa wachezaji wasiojituma na wasiokuwa na nidhamu, zaidi ya kusubiri tu mikataba yao imalizike ili waachane nao kwa amani.
Kilichobaki sasa kwa wachezaji wote wa Simba ni kujitathmini upya na kujitambua.

Kwa sasa Klabu ya Simba ndiyo yenye malisho manono nchini, na cha kujiuliza kama mchezaji atatemwa kwa sababu za utovu na nidhamu anaweza kupata klabu nyingine nchini inayolipa mishahara kwa wakati na huduma bora kama hiyo? Na kama ipo haizidi moja ambayo ni Azam, ambayo nayo haisajili kwa pesa nyingi kwa sasa.

Wachezaji wa Simba inabidi sasa wajitazame mara mbili mbili na wapo kwenye mtego, kwa kuwa mwekezaji aliyewekeza pesa zake kiasi cha Sh. bilioni 20, hawezi kukubali ujinga wa wachezaji ambao badala ya kupigania nembo ya klabu, wanatoroka usiku na kwenda kujirusha kana kwamba wanaisaidia klabu, kumbe wao ndiyo wapo kazini, wanaishi kwa shughuli hiyo ya mpira.