Ukiambiwa kitenge wakitia moto

25Jun 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
Ukiambiwa kitenge wakitia moto

“UKIAMBIWA kitenge au kiepushe na moto wewe wakitia motoni” ni methali ya kutumiwa kwa mtu anayepewa ushauri fulani wa kumfaa lakini akaupuuza na kuishia kujitosa katika taabu.

Wahenga wametuachia methali nyingi za kutuzindua na kutuelimisha. Kwa mfano, “Asiyeangalia huishia ningalijua.” Mtu asiyeangalia aendako huishia kusema ‘laiti ningalijua’baada ya kufikwa na jambo. Twashauriwa tuwe watu wa kukanyika au tunaofuata ushauri tunaopewa na waliotutangulia kwa maarifa au ujuzi kama vile wazee.

Magazeti ya michezo hutumia maneno ya Kiingereza kana kwamba hakuna ya Kiswahili! Maneno yanayotumika mara kwa mara ni ‘ishu’ yaani ‘issue’ kwa Kiingereza ambalo maana yake kwa Kiswahili ni suala au hoja. Gazeti la Kiswahili limeandika: “Ishu ya Msuva Ulaya iko hivi buana.”

Msomaji anayeitwa Mwamini aliandika yafuatayo kwenye gazeti la Mwananchi: “Kiswahili ni tunu* yetu. Kutofungamanisha Kiswahili na maendeleo ni kuukataa uzalendo wetu, utu wetu na utamaduni wetu bila sababu za msingi. Matokeo yake ni kuwa watumwa wa utamaduni wa watu wa Magharibi. Maendeleo huletwa na watu walio huru kifikra na kujituma katika kufanya kazi. Lugha inabaki kuwa chombo cha mawasiliano ambacho kikiwa peke yake bila watu walio huru kifikra, katu maendeleo ya kweli hayatoweza kufikiwa.”

*Tunu ni kitu ambacho mtu humpa mwingine kuwa ishara ya upendo; hidaya, tuzo; kitu ambacho hupatikana kwa nadra, kitu cha thamani kubwa. Kongole (shukrani, asante) Mwamini kwa kuliona hilo.

Pia waandishi hupenda sana kutumia maneno tofauti na maudhui (wazo linaloelezwa katika maandishi au katika kusema). Nimekuwa nikisahihisha Kiswahili lakini ni kama natwanga maji kwenye kinu. Kila ninavyojitahidi ndivyo wenzangu wanavyozidi kutumia maneno kinyume na maana halisi!

Baadhi ya maneno yanayotumiwa vibaya ni ‘balaa’, ‘bana’ au ‘buana’, ‘mzuka’ n.k. Uhalisi wa neno ‘balaa’ ni jambo, kitu au mtu anayefikiriwa kuleta maafa, mkosi au hasara; kisirani, nuksi. Pia jambo lenye kuleta hali ya kutoelewana; kizaazaa, mtafaruku; janga lililoenea katika jamii au kwa mtu binafsi.

Neno bwana siku hizi limepewa majina mawili: ‘buana’ au ‘bana.’ ‘Buana’ halimo kabisa kwenye msamiati wa Kiswahili ila limebuniwa na waandishi wa habari za michezo. ‘Bana’ ni kitendo cha kuweka kitu katikati ya nguvu mbili zinazoishia kwenye kitu chenyewe.

“Mkali wa Bocco mzuka kama wote” ni kichwa cha habari kinachomduwaza msomaji kwa kutojua maana yake, kikifuatiwa na maelezo yafuatayo:

“Meddie Kagere ndiye aliyeibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu baada ya kutupia kambani mabao 23, lakini straika anayemfuata na kinara kwa wazawa ni Salim Aiyee wa Mwadui, unaambiwa kwa sasa ana mzuka kama wote huko mgodini.”

Nimeeleza mara nyingi kuwa maana ya ‘tupia’ ni kuweka kitu juu ya kingine kwa kurushia rushia mahali mbalimbali kama vile ufuta juu ya mkate. Kitendo cha kuweka nguo begani au kichwani; pia tupia macho.

‘Kamba’ ni nyuzinyuzi kama vile za usumba (uzi unaotokana na ganda la nnje la nazi ambalo hufaa kusokotea kamba) au katani, zinazosokotwa kwa urefu, aghalabu hutumika kufungia mizigo; ugwe. Pia ni kiumbe wa baharini mwenye miguu mingi mirefu, magamba na nyama laini.

Ingeandikwa: “Meddie Kagere ndiye mfungaji bora wa Ligi Kuu nchini kwa kufunga mabao 23, akifuatiwa na mzawa Salim Aiyee wa Mwadui.” Hayo ya “sasa ana mzuka kama wote” anajua aliyeandika. Mwandishi anapaswa kuhakikisha wanaosoma habari/makala zake wanaelewa maana ya maneno anayoandika.

Ajabu ni kuwa hata gazeti hili ninalolitumia kukosoa maneno ya ovyo magazetini, yaelekea waandishi wake hawasomi makala za “Tujifunze Kiswahili” na ushahidi ni huu: “Aliongeza kuwa halmashauri imekinunua kifaa hicho kwa ajili ya matumizi ya kupimia kutokana na kuchukuliwa kipimo hicho, wanafanya kazi katika mazingira magumu, ikiwamo kukodisha kifaa hicho.”

Sentensi imeandikwa ovyo kwani ingepaswa kuwa mbili. “Alisema Halmashauri ilinunua kifaa hicho (GPS) ili kupimia ramani. Kutokana na kifaa hicho kuchukuliwa, watu wanafanya kazi katika mazingira magumu kwa kukodi kifaa hicho.”

‘Kukodisha’ limetumiwa vibaya na kuharibu maana. Kiswahili fasaha, ‘kodisha’ ni pangisha kitu kama chumba/vyumba, nyumba n.k. kwa malipo fulani. Wenye nyumba hukodisha chumba/vyumba au nyumba zao na wanaokodi huitwa wapangaji. Vivyo hivyo wenye vyombo vya usafiri hukodisha vyombo vyao vya usafiri na wanaokodi, yaani watumiaji, huitwa wakodishaji.

Neno ‘kodi’ lina maana mbili: Kwanza ni malipo kwa ajili ya kitu kilichotumiwa kwa muda. Pili ni fedha inayotozwa na serikali kwenye pato la mtu; kitendo cha kutumia kitu cha mtu mwingine kwa muda kwa malipo.

“Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limetoa orodha ya waamuzi watakaochezesha michuano ya Kombe la Afrika nchini Misri lakini hakuna hata mwamuzi moja kutoka Tanzania … Misri na Tunisia ndiyo wanaoongoza kuwa na idadi kubwa ya waamuzi kwenye AFCON ya mwaka huu ... wakifuatiwa na Morocco ambao wana waamuzi nne huku CAF ikishindwa kumteua hata mwamuzi moja kutoka Nigeria.” (Maneno yaliyokolezwa rangi ndio yenye matatizo). Kha! (tamko la kuonesha kukasirika au dharau) ‘mwamuzi moja,’ ‘waamuzi nne.’

Sisi ndiwo twatakiwa kwenda kufundisha lugha ya Kiswahili kwa wenzetu. Pukachaka! (Neno lenye kuashiria kutema mate ambalo humaanisha kukidharau kitu kilichotajwa).

Methali: Kila mlango una ufunguo wake.

[email protected]

0784 334 096