Ukicha kutajwa hutotenda jambo

18Jun 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
Ukicha kutajwa hutotenda jambo

UKIOGOPA kusemwa na watu ufanyapo jambo hulifanyi asilani. Methali hii hutumiwa kumhimiza mtu anayedhamiria kulifanya jambo fulani kisha akawa anaogopa wanavyosema watu wengine.

Kwa miaka 20 na ushei nimekuwa nikikosoa maneno yanayotumiwa vibaya na waandishi wa magazeti ya Kiswahili humu nchini. Lengo ni kuwaelimisha waandishi maana halisi (-enye dhati ya asili) ya maneno na jinsi ya kuyatumia katika uandishi. Niliamini watakapofanya hivyo, pia itakuwa funzo kwa wasomaji wasiojua maana ya baadhi ya maneno na jinsi ya kuyatumia.

Katika hilo, baadhi ya wasomaji wa makala zangu za ‘Tujifunze Kiswahili’ kutoka Kenya wamenitumia ujumbe wa simu na barua pepe (e-mail) wakishukuru kujua maana ya baadhi ya maneno na matumizi yake. Hii yadhihirisha “Penye miti hapana wajenzi” yaani panapokuwa na miti mingi aghalabu hapana wa kuitumia. Methali hii huweza kutumiwa kupigia mfano mahali ambapo pana vitu fulani lakini walioko mahali pale hawajui thamani yake!

Tatizo la baadhi ya waandishi wetu ni kutumia maneno ya mitaani kwa dhana kuwa ni maneno ‘mapya’ ya Kiswahili. Kweli ni mapya kwa wanaofuatilia uhalisia na chimbuko la lugha ya Kiswahili lakini si halisi, hivyo si sahihi kuyatumia. Hali hiyo hufanya waandishi kutoandika mtiririko mzuri wa Kiswahili!

Mfano: “Hii ni mara ya pili kwa mtendaji huyo mkuu wa CCM kuwaonya wanachama wanaovizia kumridhi Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein ambaye anatarajia kumaliza mihula miwili ya urais mwakani.”

Nazungumzia maneno mawili ya sentensi hiyo hapo juu, yaani ‘wanaovizia kumridhi.’ Maana ya ‘vizia’ ni jificha mahali kwa nia ya kushambulia ghafla; kitendo cha kusubiri kwa siri ili kumkamata mtu au mnyama; otea. ‘Ridhi’ ni kitendo cha mtu kukubali jambo kwa hiari; ridhia.

Hao wanaosemwa ‘wanavizia kumridhi’ Rais wa Zanzibar, ‘hawamvizii’ wala ‘kumridhi’ kwani maneno hayo mawili hayaendani na maana halisi ya ‘vizia’ kama lilivyo neno ‘ridhi’ lisivyoendana na habari ya mwandishi. Kila moja lina maana tofauti na aliyoandika mwandishi kama nilivyoyatolea ufafanuzi hapo juu.

Sentensi ingeandikwa: “Hii ni mara ya pili kiongozi huyo wa CCM anawaonya wanaojiandaa (sio wanaomvizia) kugombea (sio kumridhi) nafasi ya Rais Shein baada ya muhula wake wa pili.”

Hata kupanga sentensi kwa mtiririko mzuri unaoeleweka, siku hizi ni tatizo kwa baadhi ya waandishi: “Maandamano hayo ambayo yaliyoanzia Tazara yalikuwa pia ni kwa ajili ya kuombea taifa amani.” Mwandishi hakuwa na sababu ya kutumia neno ‘ambayo. Kwa jumla sentensi haikupangwa vizuri.’

Ingeandikwa: “Maandamano hayo yaliyoanzia (nimeacha neno ‘ambayo’) Tazara pia yalihusu kuliombea taifa amani.”

“Akizungumza na … (jina la gazeti) jana Kamishna wa Polisi, Athuman, alisema baada ya agizo walilopewa na Rais Magufuli kuhusiana na tukio hilo, utekelezaji wake ulianza mara moja.”

‘Husiana’ ni kuwa na uhusiano wa damu, kuwa na fungamano la kirafiki. ‘Husika’ ni mtu kuwa na mamlaka kwenye jambo; shiriki katika kitendo fulani. ‘Husisha’ ni kumwingiza au kumshirikisha mtu katika jambo ili aonekane naye anahusika; fungamanisha. ‘Husu’ ni husiana au fungamana na jambo; toa hisa kwa, toa fungu kwa; lazimika kufanya jambo; lazimu.

Kwa hiyo sentensi inayomtaja Kamishna wa Polisi na Rais Magufuli, neno ‘kuhusiana’ halikutumika kwa usahihi. Mwandishi alipaswa kutumia neno ‘husu’ na kuandika: “ … Kamishna wa Polisi, Athumani alisema baada ya agizo la Rais Magufuli kuhusu tukio hilo, utekelezaji wake ulianza mara” (yaani bila kukawia).

“Mkali wa Bocco mzuka kama wote” ni kichwa cha habari kwenye moja ya magazeti yetu ya michezo. ‘Mzuka’ ni neno nililoelezea maana yake mara nyingi lakini ni kama kumpigia mbuzi gitaa! ‘Mzuka’ ni kiumbe kisichoonekana ila hudhaniwa kuwa kinaishi na huweza kumtokea mtu; pepo. “Mkali wa Bocco mzuka kama wote” msomaji anaelewa nini?

Chini ya kichwa hicho iliandikwa: “Meddie Kagere ndiye aliyeibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu baada ya kutupia kambani mabao 23, lakini straika anayemfuata na kinara kwa wazawa ni Salim Aiyee wa Mwadui, unaambiwa jamaa kwa sasa ana mzuka kama wote huko mgodini.”

Maana ya ‘tupia’ ni kitendo cha kuweka kitu juu ya kingine kwa kurushiarushia mahali mbalimbali kama vile ufuta juu ya mkate. Kitendo cha kuweka nguo begani au kichwani. ‘Kamba’ ni neno lenye maana mbili: Ukambaa mnene unaotengenezwa kwa kupindwa na kuziunga nyuzi pamoja. Hapa twapata methali isemayo ‘Ukuukuu wa kamba si upya wa ukambaa.’ Pili ni mnyama mdogo wa baharini mwenye magamba laini na miguu mingi ambaye huliwa.

‘Goli’ kwa muktadha huu, ni nguzo maalumu aghalabu zenye nyavu zinazochomekwa kwenye viwanja vya michezo kama vile kandanda, kuwa ni sehemu ya kuingizwa mpira unaohesabiwa ushindi. Pia ni pambo la kike linalofanana na bangili, livaliwalo mkononi au mguuni.

Katika kandanda, mpira ‘hautupiwi kambani’ kama iandikwavyo mara nyingi na waandishi wa michezo, bali hupigwa kwa mguu na kuingia golini au kimiani yaani ndani ya wavu wenye tundu ndogo ndogo. Kwa hiyo ‘kamba’ na ‘wavu’ ni vitu viwili tofauti. Waandishi wanaopenda kuchanganya maneno hayo wanapaswa kuzingatia hili.

“Unaambiwa jamaa kwa sasa ana mzuka kama wote huko mgodini” ina maana gani? Mwandishi huandika kuwajuza wasomaji matukio au huwaandikia maneno ya mitaani yasiyoeleweka ila kwa wahuni? Kwa mfano, siku hizi mtaa huandikwa ‘kitaa’ na mtaani huandikwa ‘kitaani!’ Watanzania ndiwo tunaotakiwa kwenda kufundisha lugha ya Kiswahili nchi za nnje! Kwa maneno ya vijiweni?

Mtoto msikivu ndiye abarikiwaye.

[email protected]

0784 334 096