Ulevi wa asubuhi kero Mwananyamala

07Dec 2017
Adam Fungamwango
Nipashe
Mjadala
Ulevi wa asubuhi kero Mwananyamala

TANGU kuingia madarakani Serikali ya Awali ya Tano chini ya Rais, Dk. John Magufuli, kumekuwa kukihimizwa zaidi suala la uchapaji kazi na kuachana na masuala ya uzembe na ulevi.

 

 

Akitekeleza kaulimbiu yake iliyokuwa maarufu sana wakati wa kampeni 'Hapa Kazi Tu', Rais Dk. Magufuli amekuwa akifanya kwa vitendo na si maneno, pia akitaka kila Mtanzania achape kazi na kuachana na maisha ya kubangaiza na ya ‘kimjini - mjini’ yaliyokuwa yamezoeleka huko nyuma.

Kila mmoja sasa ameanza kuishi na kula kwa jasho lake halali na serikali ilishapiga marufuku unywaji pombe mojawapo kali iliyokuwa imezoeleka sana.

Serikali kwa kutilia mkazo wa kila mtu afanye kazi, ilipiga marufuku watu kunywa pombe nyakati za asubuhi na mchana.Katazo hilo limesaidia sana si tu kuondoa uhalifu, pia limesaidia kupunguza ajali za barabarani na hasa bodaboda na mengine yanayofanana na hayo.

Hata hivyo, bado zipo chembe chembe au mabaki yaliyobaki yakiachiwa, yanaweza kusababisha hata wale walioacha kurejea tena na kuifanya kazi iliyofanyika mwanzo yote kuonekana ni kazi bure.

Bado kuna maeneo hasa jijini Dar es Salaam yameonekana yakiendelea na biashara ya kuuza pombe kali nyakati za asubuhi mpaka mchana, tena siku ambazo ni za kazi.

Cha ajabu ni kwamba, sehemu hizo si kwenye baa au grosari, bali ni kwenye maduka ya kawaida tu ya wazi.

Sehemu zilizokithiri kwa kiwango cha hali ya juu ni Mwanyamala Kisiwani. Kuna maduka kadhaa yanayouza pombe nyakati za asubuhi hasa  Mwananyamala Kisiwani, likiwepo moja jirani na kanisa hapo hapo Mwananyamala Kisiwani.

Hilo na mengine, huuza pombe kali zinazopimwa kwenye glasi ndogo za plastiki na wanakunywa bila ya woga. Wamekuwa wakijazana kwenye viti nje ya maduka hayo kuanzia alfajiri hadi jioni. Najiuliza kwanza, wanafanya kazi saa ngapi? 

Hali hii si tu kwamba inawafundisha tabia mbaya watoto na jamii kwa jumla, pia watumiaji vinywaji hivyo wanatumia matusi bila ya kujali watu wanaopita hapo, watoto wa nyumba jirani wanaofikiwa na lugha hizo za matusi na kuanza kuiga kutukana, yote yakiishia katika mporomoko wa maadili.

Kibaya zaidi, huwakwaza na kuwanyanyasa kinamama wanaopita njiani hata baadhi wanalalamika kwa kauli “hawana tabia nzuri, wanatutukana, wanatunyanyasa sisi wanawake na hata baadhi ya wanaume wanakutana na adha hiyo wanapopita. “Tunaomba kituo kidogo cha Polisi cha Mwinjuma, ambacho kipo jirani waliangalie suala hili kwa sababu ninachojua serikali imeshakataza, halafu pia ni duka linalouza  mahitaji ya kawaida tu, itakuwaje tena wanauza pombe?"

Kutokana na kuchoshwa huko na tabia hiyo ya  kilevi, pia tunaiomba Polisi Mwinjuma iliangalie hili na kumuunga mkono Rais wetu, kwani kwa kawaida pombe huuzwa katika sehemu maalumu ili watoto na wanafunzi wasijiingize kwenye tabia hiyo.

Pia, ni kitu kinachofanyika kwa wakati maalum, huku ulevi wa asubuhi si sahihi kwa kusababisha watu wasifanye kazi, bali uhalifu na kero kwa wapita njia na majirani kwa jumla.