Ulinzi mabinti uanze kudhibiti utumikishwaji wa nyumbani

04Aug 2020
Na Waandishi Wetu
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ulinzi mabinti uanze kudhibiti utumikishwaji wa nyumbani

WATOTO wengi wa kike sehemu nyingi duniani wanakabiliwa na vikwazo kama kutothaminiwa katika jamii pale wanapoanzisha safari yao ya kuelekea utu uzima.

Kutokana na vikwanzo hivyo wanavyokutana navyo ambavyo ni pamoja na mimba na ndoa za utotoni, unyanyasaji,ubakaji pamoja na kutokuwa na usalama wa kutosha katika jamii., wengi hawajui hatima yao.

Mabinti wanakabiliwa na changamoto nyingi. Kiini chake ni kukosekana kwa usawa wa kijinsia pamoja na usalama katika jamii nyingi hasa za Kiafrika yakiwamo makabila mengi ya Tanzania.

Hali hiyo huwakuza na kuwainua watoto wa kiume na kuwadhalilisha wa kike kuanzia ngazi ya familia hadi taifa.

Ipo dhana potofu katika jamii ya wengi kuamini kuwa mtoto wa kike hawezi kufanya jambo la muhimu ikilinganishwa na watoto wa kiume. Dhana hiyo hutokana na mfumo dume uliotawala katika jamii nyingi ambazo zinaamini kuwa watoto wa kiume ni muhimu zaidi na hivyo hupewa kipaumbele na fursa katika nyanja zote ikiwamo kipaumbele katika kupata elimu.

Ubaguzi huo huchangia mabinti kulazimishwa kuacha masomo na kukatisha ndoto zao.

Hivyo umewadia wakati wa dunia kuchukua hatua na kuwapa fursa ya maisha bora wasichana hawa pamoja na kuwawezesha kutimiza ndoto zao katika jamii wanazoishi.

Hata hivyo changamoto zinazowakabili wasichana zinatatulika kwa kuimarisha uwezo wao wa kujiamini.

Baadhi ya njia ambazo zinaweza kutatua changamoto hizo ni pamoja na elimu kupewa kipaumbele hasa kwa mtoto wa kike.

Serikali, wazazi , walezi na walimu wanatakiwa kufanya bidii ili kuleta usawa baina ya wavulana na wasichana kwenye elimu.

Aidha, kuwahamaisha kupenda elimu na kuwapa moyo katika masomo yao ni mojawapo ya mbinu za kumuimarisha mtoto wa kike, kwani atajiona yuko sawa na wenzake wa kiume.

Halikadhalika elimu ya utambuzi ni muhimu kwa wasichana, wanatakiwa kukumbushwa kuwa ni sehemu ya jamii na hivyo kazi yao sio kuzaa pekee.

Hivyo hamasa hiyo inatakiwa kufikishwa kwa nguvu zote kwa jamii zote zisizothamini kuwasomesha, kuwaoza.

Mtoto wa kike anatakiwa aelimishwe kuwa anawajibika kuijenga jamii yake kwa namna nyingi si kuzaa pekee. Aidha, atambue mchango wake kwa jamii kiuchumi na kisiasa.

Kampeni zinaweza kusaidia wanajamii kuondokana na dhana potofu ya kuwa mtoto wa kike hana thamani sawa na mtoto wa kiume.

Asasi mbalimbali za kiserikali na kiraia zinaweza kutoa elimu kwa jamii kuhusu thamani ya watoto wote, wa kike na wa kiume.
Vilevile, wazifahamishe jamii namna ya kuripoti matukio yanayohusu unyanyasaji wa mtoto wa kike.

Aidha, ili kudhibiti utumikishwaji wasichana, ajira ya wasichana wa ndani iangaliwe upya na

Ni muhimu pia taifa likaweka sheria inayoelekeza au kutoa mwongozo wa ajira za wasichana wa ndani.

Kwamba sheria itamke wazi kuwa msichana aliye chini ya miaka 18 asiajiriwe kufanya kazi za ndani. Hii itachangia jamii nzima kumthamini mtoto wa kike na kumuongezea nafasi mtoto wa kike kufikia ndoto zake.

Pengine wakati umefika kwa kila mmoja kutumia nafasi aliyonayo iwe nyumbani, shuleni, kazini, ama katika jamii; kuondoa changamoto zinazomkabili msichana kutokana na ubaguzi.

Walimu na walezi maana wao hutumia muda mwingi na watoto na wanaweza kuwajengea dhana chanya ya usawa wa kijinsia wakiwa na umri mdogo.

Fatma Mtutuma na Faudhia Sultan (UDOM)