Ulinzi wa kisheria kwa wajane

29Jun 2019
John Juma
Nipashe
Mionzi ya Sheria
Ulinzi wa kisheria kwa wajane

KUTOKANA na maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani, ambayo hufanywa Juni 23 kila mwaka, ni vema kujifunza zaidi kuhusu haki za wanawake hawa waliofiwa na wenza.

Sheria  ya  Ndoa  ya mwaka 1971, Sura  ya  29 iliyorekebishwa  mwaka  2010; sanjari na  Sheria  ya Usimamizi  na  Uendeshaji  wa  Mirathi Tanzania Sura  ya  352, marejeo ya mwisho 2002, zinaainisha haki hizo.

Kwa ujumla ziko  aina  mbili za  mali  anazostahili mke wa marehemu au mjane.

Mosi, ni  mali  inayotokana  na  mali za walizochuma  pamoja na mumewe wakati wa uhai wake.

Pili  ni  urithi  anaostashili  kupata   kama  mrithi  halali wa  marehemu mumewe.

Vifungu vya 2(1); 60 (b); na 114(1)-(3) vya Sheria  ya  Ndoa Sura  ya  29 ya mwaka 1971  iliyorekebishwa mwaka  2010.

Kwa  mfano,  mume amefariki. Lakini  kabla  hajafa   walijenga  nyumba    pamoja na mkewe. Au walinunua kiwanja au gari. Mume baada ya kufariki ameacha mali hizo.

Isitoshe pia, kwa kufuatia msingi huo huo, katika mali husika kuna “share” ya mume, kadhalika ya mke. Na zaidi sana, “share” ya kila mmoja inatokana na ukweli kuwa kila mwanandoa, wote kwa pamoja wamechangia nguvu katika kufanikisha kupatikana kwa mali hizo.

Shauri maarufu la Hawa Mohamed dhidi ya Ally Seif [1983] kwa kuzingatia uamuzi wa kimahakama uliofikiwa kupitia shauri hilo, itoshe kuongeza kwamba mchango huo siyo tu ule wa leta ni  lete, kwani hata kazi za nyumbani zinazofanywa na mke au mume kama kupika, kufua, kulea watoto ni mchango katika kupatikana kwa mali hizo.

Lakini, pia bado ni muhimu kwa wanandoa kufahamu na kuzingatia kwamba “mchango hasi”; kama vile matumizi mabaya ya fedha na rasilimali za familia vinaweza siyo tu kumpunguzia mhusika sehemu ya haki ya gawio, bali hata kumkosesha kabisa.

Tatu, endapo mume amekufa, mwanamke anastahili urithi kutoka mali za marehemu mumewe. Urithi huo utatokana na mali  zilizokuwa zikimilikiwa na mume na yeye pia.

Jambo hili ni kusema kwamba urithi huo utatokana na “share” au sehemu ya mali ya mume na siyo ile ya mke, ambayo tayari ni stahiki yake.

Tena, mjane anazo tena atakuwa na haki za aina mbili ya kupata sehemu yake aliyochangia katika kupatikana kwa mali husika, sambamba na haki ya kurithi mali ya marehemu mumewe.

Taratibu za Kufuata

Kinachotakiwa kufanyika, awali ya yote, ni kutambuliwa kwanza sehemu ya mali ambayo ni sehemu ya mchango wa mke katika kupatikana kwa mali husika na kutengwa na kuwekwa pembeni.

Mfano kama ni nyumba ya vyumba sita na pengine  mchango wa pamoja wa mke  na  mume  ni  nusu  kwa  nusu, bilashaka  vyumba  vitatu  vitawekwa  pembeni  kama sehemu   ya  mchango wa  mke huyo na vile  vyumba  vitatu  ambavyo vitabakia ndiyo vitatakiwa kugawanywa kama urithi halali  kwa kuwa warithi (wote) watakakuwepo.

Itajumuisha mke wa marehemu (mjane)  na watoto kama wapo. Ile hoja eti kuwa  alishapatiwa  vyumba  vitatu hapo  mwanzo haitakuwa na msingi.

Ieleweke kuwa urithi  siyo  jasho la nguvu kazi au rasilimali za mhusika, bali  hutokana na mapenzi ya  mtoa  wosia  na  matakwa  ya  lazima ya kisheria kwa maslahi ya wanufaika ambao ni lazima kupata stahiki zao akiwemo na mke wa marehemu .

Kufuatilia Mahakamani

Katika mazingira hayo kukusudia ni muhimu kwanza kwa msimamizi wa mirathi au wasii kuthibitishwa au kuidhinishwa na Mahakama.

Ambapo basi, anaweza kuwa alishateuliwa au kutajwa na marehemu  katika wosia au kama  hakuna  wosia  atateuliwa na kupendekezwa  na  ndugu kwenye  kikao cha familia.

Vifungu  2(1); 3; 9; 16(a)-(d); na 17  vya Sheria  ya Usimamizi  na  Uendeshaji  wa  Mirathi  Sura  ya  352 vinaeleza.

Baada ya  mahakama kumthibitisha msimamizi wa  mirathi au wasii, kwa mujibu wa taratibu,  mjane ataweza  kudai  haki yake ya kwanza inayojumuisha mali walizochuma pamoja na mumewe.

Katika mali zilizoachwa na marehemu, kabla  ya  mgao  wa  mirathi  kuanza kuchukua hatamu kwa kuzingatia haki za warithi wengine na haki hii ataidai  kwa  msimamizi  wa  mirathi.

Na kama  mjane ndiye msimamizi  wa  mirathi basi  haki  hii  ya mali walizochuma pamoja ataidai kwa  warithi.

Kwa lugha nyepesi zaidi, atapata  sehemu  yake baadaye urithi. Na mwisho, kama  kutakuwa na mgogoro au ubishi, utata mjane huyo ili kulinda maslahi yake, atatakiwa kufungua Shauri la Malalamiko Mahakamani na kuiomba itoe tamko kuhusu hatima ya kupata sehemu au share yake katika mali zilizochmwa pamoja na mumewe.