Umahiri na ukakamavu wa JWTZ ni miujiza ?

11Dec 2016
Owden Kyambile
Nipashe Jumapili
Muungwana Lazima Nilonge
Umahiri na ukakamavu wa JWTZ ni miujiza ?

JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambalo mwaka huu lilitimiza miaka 52 tangu kuasisiwa kwake Septemba Mosi 1964, limetajwa kuwa miongoni mwa majeshi bora na yenye weledi, uzoefu na ujuzi mkubwa wa mapambano katika Bara la Afrika na nje ya Bara hilo.

Taarifa zilizowahi kutolewa kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu jijini Dar es Salaam mwaka 2014, ilikitaja Kikosi cha Majeshi Maalum (Specil Forces) cha JWTZ kinacholinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuwa ni miongoni mwa vikosi bora 30 vya majeshi maalum duniani kwa mafunzo, uwezo na weledi.

JWTZ katika uhai wake wa miaka 52, limepitia harakati nyingi za majukumu makubwa na kufanikiwa kutoa michango lukuki ya kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi pamoja na majukumu mengine yaliyofanyika nje ya nchi.

Jeshi hilo lilishiriki kikamilifu kufanikisha harakati za ukombozi barani Afrika kwa kufundisha majeshi ya vyama vya ukombozi Kusini mwa Afrika na likachangia kupatikana kwa uhuru wa nchi za Angola, Msumbiji, Zimbabwe, Namibia na hata Afrika Kusini.

Vita ina gharama zake, lakini gharama kubwa ni wakati wapiganaji wanapopoteza maisha yao. Kama ilivyokuwa wakati wa vita dhidi ya Amin wa Uganda, vita vya ukombozi pia viligharimu maisha ya baadhi ya askari wa JWTZ, ambao mabaki ya miili yao imehifadhiwa katika makaburi yaliyoko Naliendele mkoani Mtwara.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Amirijeshi Mkuu huko Ikulu, ilisema si tu kwamba JWTZ limetekeleza ipasavyo malengo na shabaha zake za msingi kikwelikweli, lakini pia limebakia kuwa jeshi imara, lenye uzalendo, lenye utii na nidhamu ya hali ya juu.

Taarifa ilisema hizo ni sifa ambazo mataifa mengi hususani katika Afrika zimeshindwa kufanikiwa, na kwamba ni dhahiri kuwa amani, utulivu na usalama wa nchi yetu katika miaka yote 52 sasa umechangiwa sana na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.

Jeshi hilo limeendelea kushiririki katika shughuli za ulinzi wa amani duniani na kupata mafanikio makubwa kwenye operesheni za kulinda amani katika nchi mbalimbali kama Liberia, Darfur, Lebanon, Ivory Coast, Visiwa vya Shelisheli, visiwa vya Comoro, na sasa huko DRC ambako majeshi ya JWTZ yalifanikiwa kukiangamiza kabisa kikundi cha waasi wa M23.

Jeshi hilo halikuishia kutekeleza mbinu za medani ya kivita peke yake, bali wanajeshi wake wameshiriki kikamilifu kwa kushirikiana na mamlaka za kiraia katika uokoaji na maafa hususan kwenye majanga yakiwemo ajali ya MV Bukoba, ajali ya meli Zanzibar, mafuriko ya Kilosa, Morogoro ambako jeshi hilo lilijenga reli iliyokuwa imesombwa na maji, na hata huko Mwakaleli mkoani Mbeya ambako jeshi liliwajengea wananchi daraja la mto Lufilyo baada ya mvua kung'oa miundombinu hiyo.

Kwa kipindi chote cha miaka 52, JWTZ halijapata kashfa za utovu wa nidhamu wala kuhusishwa na hujuma za jumla katika nyanja mbalimbali nchini, limekuwa mfano katika utendaji uliotukuka na hata wakati wa dharura za migomo kama ilivyowahi kutokea kwa madaktari kugoma nchini, madaktari wa Jeshi hilo walikuwa mbadala wa kutoa huduma za tiba.

Wanajeshi hawa hufikia wakati wakastaafu kazi na kujiunga na raia wengine mijini na hata huko vijijini, wakiendelea kuwa raia wenye nidhamu.

Wakati Jeshi letu linapopata sifa kubwa kiutendaji, ni budi kukumbuka kuwa makamanda na wapiganaji wengi waliostaafu, na ambao wengi wao wapo vijijini ndio walioweka misingi imara inayolifanya jeshi sasa lionekane bora Barani Afrika, aidha ni jambo la kijivunia sana kwa jeshi la nchi kuwa miongoni mwa majeshi 30 bora duniani!

Wanajeshi wastaafu wanaishi katika maisha ambayo ni tatanishi kiuchumi, mafao yao ambayo kwa kipindi kirefu hayajaboreshwa yamewafanya waishi katika hali ya kimaskini bila mfano, na hao hao ndio walioliwekea JWTZ rekodi nzuri inayowavutia wengi duniani.

Naelewa kila kipindi kina changamoto na mambo yake, kizazi kilichopo leo ni tofauti na kile cha miaka 20 iliyopita, na hata teknolojia imebadilika, lakini gharama za maisha hazimchagui mstaafu wala aliyeko kazini, sasa ni kwanini wastaafu hawa wasiangaliwe kama ni sehemu 'potential' ya mafanikio ya Jeshi hili?

Na kuwaenzi kwao iwe ni kwa kuwajali kiuchumi, najua serikali imelalamikiwa mara nyingi, lakini labda haijui uchungu wa wastaafu wapiganaji ulivyo!

Hamasa na msisimko waliouonyesha wanajeshi wakati wa gwaride la sherehe za miaka 55 ya Uhuru juzi, ni mwendelezo wa umahiri na nidhamu ya JWTZ, tukumbuke vijana hao pia siku moja watastaafu, lakini jeshi litaendelea tu! Serikali isiwafumbie macho wastaafu.

Maoni 0715-047304