Umbea wa Simba, Yanga

21Nov 2020
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Umbea wa Simba, Yanga

‘UMBEA’ ni tabia ya kutoa habari bila kutumwa au kuulizwa; udaku, udakuzi. Tabia ya kufuatilia au kusikiliza habari za watu wengine bila kutumwa.

'Siri’ ni jambo lililo moyoni mwa mtu ambalo mwingine halioni ila yeye mwenyewe. Ni jambo au tukio ambalo bado halijatakiwa kudhihirishwa. Jambo ambalo watu wengi hawalijui, jambo lililofichika.

Mtu anayetarajia kuposa*, hapigi mbiu (pembe inayopulizwa ili kuwaarifu watu jambo fulani; ujumbe au taarifa inayotolewa na mpuliza pembe hiyo).

*Posa ni maombi ya kutaka kuoa yanayopelekwa kwa wazazi wa binti anayehitajika kuolewa; taarifa au ombi la kutaka kumwoa binti kwa wazazi wake; chumbia.

Usajili wa wachezaji, hasa kwa Simba na Yanga, hufanywa bila kificho na kusababisha kile kiitwacho “mwenye kisu kikali ndiye alaye nyama.” Kwamba anayekishika kisu kikali ndiye anayeweza kuikata nyama vizuri.

Simba na Yanga hawana siri ila umbea ndio unaotawala wakati wanapohaha kupata wachezaji wa kuwasajili.

Ndo maana ilisemwa: “Siri ya mtungi iulize kata.” Maana yake siri ya mtungi wa maji inajulikana na kata ya maji, maana vitu hivi vinatumika pamoja, haviachani.

Methali hii hutumika kwa maana ya kuwa ukitaka kuijua, kwa mfano, siri ya marafiki wawili, mpate mmoja kati yao umwulize, ndiyo ataijua, maana wako pamoja kama vile mtungi na kata.

Linapokuja suala la usajili wa wachezaji, lazima Simba na Yanga zitaingiliana, ama kwa dhati (umakini wa moyo) au kuchafuana ili mojawapo, au zote zimkose mchezaji anayegombewa!

Tabia hii imekuwapo kwa miaka mingi kila upande ukiutega mwingine. Huandika mara kwa mara kwamba kisemwacho kuwa Simba na Yanga ni ‘watani wa jadi’ si kweli kwani watani wa jadi husaidiana katika mambo mbalimbali mmoja anapokuwa kwenye matatizo.

‘Nyang’anya’ ni kitendo cha kuchukua kitu bila ridhaa ya mwenyewe; pora, nyakua.
‘Nyang’anyiana’ ni kitendo cha kugawana kitu bila ya mpango kwa namna ambayo kila mmoja anataka apate zaidi kuliko mwingine; nyanyia, yaani pata kitu kwa ujanjaujanja, laghai ili kupata kitu.

‘Uongozi’ ni dhamana ya kusimamia jambo kwenye taasisi au penginepo. Madaraka anayopewa mtu ya kusimamia au kuongoza shughuli.

Hutunduwaa (shangaa, baki kimya bila kutenda jambo au kwa ajili ya kufikiria jambo linalostaajabisha; duwaa) nisikiapo viongozi wa Simba na Yanga wakivutana kuhusu mchezaji fulani anayetakiwa na kila upande!

Kwa nini viongozi wa vilabu hivyo kongwe hawafanyi usajili wao kimya kimya bila kueleza hadharani mchezaji wanaomkusudia au wanaofanya mazungumzo naye ili wamsajili?

Kwa nini huingiliana na hata kuibiana wachezaji kama upande mmoja ukipata tetesi kuwa mchezaji huyo anatakiwa Msimbazi au Jangwani? Huo si ‘utani wa jadi’ bali ni ‘chuki za jadi.’ Anayebisha abishe, lakini ukweli ni huo ingawa unaumiza.

Ukichunguza sana utagundua kuwa viongozi wa Simba na Yanga hutaka kuoneshana nguvu ya fedha ilhali hawana uwezo huo!

Wakati Simba wakimtegemea sana MO Dewji kwa kila jambo, Yanga nao wanaitegemea mno Kampuni ya GSM kwa kila kitu baada ya aliyekuwa mfadhili wao wa zamani mambo yake kwenda msobemsobe.

Yanga na Simba zilikuwa moja mwaka 1935 lakini mwaka uliofuatia, (1936) kukawa na mfarakano (hali ya kutoelewana) baina yao. Simba ya sasa ikaitwa Sunderland ambayo ndio hii inayoitwa Simba leo.

Tangu wakati huo, si Yanga wala Simba inayojitegemea yenyewe. Simba ilikuwa ikiwategemea Waarabu ilhali Yanga ikiwategemea Wahindi. Hebu fikiri kwa miaka 85 vilabu hivyo vinavyoitwa ‘watani wa jadi’ havijaweza kujitegemea ila vinaendelea kuwa tegemezi (-enye kutumainia kiumbe kingine kwa mahitaji yake)!

Je, ni ‘watani wa jadi’ kweli au ‘wajinga wa jadi’? Wana dhamira (nia ya kufanya jambo; azma, kusudio) ya kuviendeleza vilabu hivyo au ni kile kisemwacho ‘kupiga pesa’?

Leo, kwa mfano, Mo Dewji (Simba) na GSM (Yanga) wakijitoa, timu hizi zitakuwaje? Viongozi wa vilabu wanaweza kueleza walivyozisaidia timu zao na kuwaletea maendeleo yoyote? Ni yale wasemayo Waingereza: “be coining/minting money” yaani kutajirika haraka haraka!

Kama Simba na Yanga zikiendelea kubebwa kwa mbeleko (kitu au nguo itumiwayo kum-bebea mtoto mgongoni au kifuani) na hao wafadhili wao, yaani MO Dewji na kampuni ya GSM wanaozisaidia kwa hali na mali wakiondoka, viongozi waliopo madarakani wanaweza kuviendesha vilabu hivyo? Allahu ya aalam (Mungu ndiye mwenye kujua zaidi)!

‘Uongozi’ ni dhamana ya kusimamia jambo kwenye taasisi au penginepo; madaraka anayopewa mtu kusimamia au kuongoza shughuli. Je, viongozi wa Yanga na Simba wanajua maana ya uongozi na umuhimu wake?

Ile nyumba ya Yanga pale Jangwani na Simba pale Msimbazi hata kupakwa rangi ni mpaka wadhamini wajitolee! Ukibebwa usilevyelevye miguu, chambilecho wahenga.

[email protected]
0784 334 096