Umefika wakati kutambua viongozi wanaofaa na feki

15Mar 2019
Mary Geofrey
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Umefika wakati kutambua viongozi wanaofaa na feki

KUELEKEA Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, wabunge na madiwani wameanza kujirudi kwa wananchi kuanza kutoa misaada mbalimbali.

Kila ukiangalia vyombo vya habari mwaka huu, utaona habari za mbunge huyu na diwani yule, wametoa msaada wa vitu kadha wa kadha kwa wananchi wa maeneo yao.

Sawa, ni wajibu wenu kutimiza vile mlivyoahidi kwa wananchi waliowapigia kura, kwa sababu lengo la kuomba kura lilikuwa ni kuwaongoza, kuwasemea na kuwapa misaada inayotakiwa.

Lakini, kipindi hiki kisitumike kama fursa kwenu viongozi ambao mlishindwa kutimiza wajibu wenu katika kipindi cha miaka minne mliyopewa, nafasi ya kutumika katika maeneo husika, mkatumia muda huu kuwalaghai wananchi.

Isiwe tangu mmechaguliwa mlitulia kula maisha, mkaacha kujishughulisha na matatizo ya wananchi kwa madai mko ‘bize.’ wakati huu ndio mnarudi mkijifanya kazi mliyopewa mnaimudu.

Ni vyema na haki kwa kiongozi aliyekuwa anatimiza wajibu wake wakati wote wa uongozi tangu alipochaguliwa, akaendelea kutimiza wajibu hata sasa, tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Lakini isiwe umerudi jimboni kwa sababu umejua uchaguzi mkuu unakaribia na wewe bado unataka kupewa nafasi ya kuendelea kuongeza eneo ulilopo.

Msiwafanye wananchi hawana akili za kupambanua mambo, mkadhani hawajui vyema kuwa mlishindwa kutimiza wajibu wenu, leo ndio mrudi kwa zawadi za hapa na pale.

Wakati huu wa kurudi jimboni au kwa wananchi wakati miaka mingine ulikuwa ‘bize’ na mambo yako, inatia shaka machoni mwa wananchi ambao naamini ni weelewa wazuri wa kupambanua mambo katika nyakati tofauti.

Inashangaza sana kuona kiongozi anarudi jimboni na kuanza kuchangia mifuko ya saruji ya Sh. 500,000 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa yaliyokuwa yameinama tangu anaomba kuchaguliwa 2015.

Inashangaza na kutia hasira zaidi pale anapochukua waandishi wa habari, ili watoe habari hiyo kwa lengo la kuuaminisha umma wa Watanzania, kuwa ni kiongozi wa kuigwa.

Utakuwa wa maana, kama ulikuwa unafanya hivyo miaka yote bila ya kujali, ulikuwa unatangaza au la, kwa sababu Watanzania wanaona na wanafahamu ni nani anawafaa.

Nayaeleza hayo, kwa sababu wapo madiwani na wabunge ambao baada tu ya kuchaguliwa, walihama kabisa maeneo yao nao wakaenda kuishi mjini kula maisha kwanza.

Wapo na wengine ambao mara baada ya uchaguzi mkuu wa 2015, walikata mawasiliano na wananchi katika namna ya hawana tena muda wa kupoteza, kwa ajili ya kuzungumza na wakadhani miaka mitano ni mingi sana.

Kuna wale waliokuwa wanaonana na wananchi, lakini hawakutumia nafasi zao kutatua changamoto zinazowakabili. Ieleweke, kutatua changamoto za wananchi, si kuwapa hela, bali ni kuwawakilisha kutafuta msaada wa kile wanachokitaka.

Pia, wapo ambao waliokuwa bize kuwazungumzia bungeni, lakini kurudi jimboni ilikuwa shida, hawakuwa na muda, kutwa wako katika vikao visivyo na mwisho, Nao wajue, wakati wa kurudi kwa wananchi nao umefika.

Uongozi unautaka, majukumu unayakwepa. Ni wakati wa kuvuna ulichopanda na ukumbuke kuwa ‘ng’ombe hanenepeshwi siku ya mnada.’

Wananchi je? Ni wajibu wenu sasa kutambua nani anawafaa kuendelea kuwa kiongozi wa eneo lako, kulingana na hulka ya uwajibikaji wake, lakini si kwa sababu ya maarufu.

Wananchi wasikubali kupumbazwa na ‘vizawadi’ vya muda mfupi na vyenye lengo la kuombea kura.

Kama kiongozi anatoa msaada, ni vyema na ni wajibu wake kufanya hivyo. Lakini, isiwe kigezo cha ushawishi wa kuomba kura.

Kipindi cha uchaguzi hakijafika na kitakapofika, mnapaswa kuchagua wawakalishi ambao mnaamini watawawakilisha vyema, katika kuwaongoza, badala ya wale wanaotaka madaraka kwa ajili ya shughuli zao binafsi.

Msiwaonee haya viongozi wa namna hii. Wealezeni ukweli na kama kuwakataa muwakatae, kwa kuwa walishindwa kufanya kile mlichowaagiza au walichoahidi.

Msikubali kutumika kuwa madaraja ya kupandisha watu kufikia malengo yao, maisha yao yakiendelea kupaa na nyie mnabaki kuwa watu wale wale, msio na shule nzuri, majisafi na salama.

Hakikisheni kama kiongozi alitoa ahadi zake, alizitimiza na kama hakuzitimiza, basi muwe mliona juhudi zake za kuzitatua, lakini akakwama kwa sababu mnazozijua. Daima isiwe alienda kula maisha mjini, akawaacha na shida zenu, leo anarudi akitaka kuchaguliwa tena.

Madhara ya kuchagua wasiyofaa na waroho wa madaraka, nadhani yanafahamika, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi na jamii kupima.