Umma, wadau wahamasishe miezi sita ya mwanzo unyonyeshaji maziwa

03Aug 2017
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Umma, wadau wahamasishe miezi sita ya mwanzo unyonyeshaji maziwa

WIKI hii Tanzania imeungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Wiki ya Unyonyeshaji wa Maziwa ya Mama kwa Mtoto inayoadhimishwa kila mwaka kuanzia Agosti Mosi hadi 7.

Hii inafuatia Azimio la Innocent nchini Italia, lililosisitiza umuhimu wa kulinda, kuendeleza na kusaidia unyonyeshaji na ulishaji wa watoto.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa kitaifa wa maadhimisho hayo juzi jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema kuna uhusiano kati ya Unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa mtoto na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Mojawapo ya malengo yaliyo na uhusiano na unyonyeshaji wa maziwa kwa mtoto aliyoyataja waziri ni ya Lishe, Uhakika wa Chakula na Kupunguza Umaskini.

Akasema katika eneo la lishe na uhakika wa chakula, unyonyeshaji ni muhimu na njia inayoweza kupunguza tatizo la utapiamlo endapo taratibu za unyonyeshaji zitafuatwa.

Kwamba unyonyeshaji wa maziwa ya mama huchangia kwa kiasi kikubwa kuboresha afya, kulinda uhai na maisha ya mtoto.

Mwalimu akasema, kunyonyesha maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo ya maisha ya mtoto ndiyo njia bora na salama ya kumpatia virutubisho vyote muhimu kwa ukuaji na maendeleo yake.

Akafafanua, maziwa ya mama yana sifa ya kipekee ya kuwa na kinga za mwili ambazo humkinga mtoto dhidi ya magonjwa na kuchangia kupunguza vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano.

Muungwana ameona aangazie ufafanuzi huo wa waziri kwa kuwa lengo mojawapo la maendeleo endelevu ni hilo la kuhakikisha dunia ikiwamo Tanzania ina lishe bora na uhakika wa chakula ifikapo mwaka 2030.

Kimsingi mambo yote hayo bado ni changamoto kubwa kwa Watanzania.

Umaskini bado upo na Watanzania wengi hawana uhakika wa chakula, kwani bado kuna watu wanaopata mlo mmoja ama miwili kwa siku.

Aidha, lishe bado ni tatizo kubwa, hasa kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa mwaka 2015 na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) na SMART, udumavu ambao ni moja ya viashiria vikubwa vya utapiamlo kwa watoto chini ya miaka mitano hapa nchini uko kwa asilimia 35.

Kwa maana nyingine kati ya watoto 100 walio chini ya umri wa miaka mitano, watoto 35 wamedumaa.

Vyanzo mbalimbali vya lishe vinafafanua kwamba, mtoto mwenye utapiamlo huugua mara kwa mara na huwa na maendeleo dhaifu ya ukuaji wa kimwili na kiakili.

Kwa kuwa na uwezo mdogo wa kiakili, humsababishia ugumu wa kufikia elimu ya juu katika maisha yake, hivyo kuwa na mchango mdogo katika kukuza uchumi na pato la taifa.

Sasa, sababu kubwa inayosababisha watoto katika umri huo kudumaa ama kupata utapiamlo ni kutokana na ukosefu wa lishe bora.

Waziri alifafanua kuwa, unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa mtoto katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo bila ya kumpa maji au vinywaji vingine ni lishe na chakula cha uhakika kwake.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Takwimu za Utafiti wa Hali ya Kidemografia na Afya uliofanyika mwaka 2015, asilimia 41 ya watoto wenye umri chini ya miezi sita hawanyonyeshwi ipasavyo, hali inayowaweka katika hatari kubwa ya kupata utapiamlo.

Ni rai basi ya Muungwana kwa wadau wote wa afya na lishe na wananchi kwa ujumla kuhamasisha na kuelimisha umma ili kinamama hao 41 kati ya 100 ambao hawanyonyeshi ipasavyo maziwa watoto wao wafanye inavyopaswa.

Wahakikishe wanawanyonyesha maziwa pekee watoto wao katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo ya uhai wao ili kujenga kizazi chenye tija kwa taifa.