Umoja DataVision, TAFCA utaibeba sanaa za mikono

17Jul 2017
Adam Fungamwango
Nipashe
Mjadala
Umoja DataVision, TAFCA utaibeba sanaa za mikono

HAKUNA njia ya mkatato kwa wasanii wa kazi za mikono kuweza kujijenga kiuchumi na kukuza kazi zao kwa soko la ndani na nje ya nchi zaidi ya kuunda umoja wao utakaotoa fursa pana zaidi kuweza kufika mbali na kuongeza kipato chao.

Hiyo ni kutokana na ukweli kwamba wasanii wa kazi za mikono wamekuwa katika mazingira magumu ya kazi zao na kushindwa kupenya kwenye hadhi ya kimataifa kwa sababu mbalimbali moja ikiwa ni fani hiyo kutokuwa na umoja ambao unaweza kuwakutanisha pamoja na kupanga jinsi ya kupanua soko la bidhaa zao, hivyo kujitanua kiuchumi kuliko wanavyoonekana katika sura ya umaskini kwa sasa.

Kwa kutambua hilo, Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania (TAFCA)na Kampuni ya DataVision International (DVI), limewataka wasanii wa sanaa za mikono kuunda umoja wao utakaowaunganisha kuwa kitu kimoja ili kujijenga kiuchumi hususan katika kutafuta masoko ya ndani na nje ya nchi.

TAFCA na DataVision International mwishoni mwa wiki iliyopita walikutana na wana sanii mbalimbali wakiwamo waasisi wa asasi mbalimbali za sanaa kupanga jinsi ya kuwakwamua kiuchumi kwa kuwajenga na kuwawezesha kuendeleza vipaji vyao.

Rais wa TAFCA, Adrian Nyangamalle anasema sanaa ya kazi za mikono ina changamoto kubwa, na kwamba hatua ya kuwakutanisha na DataVision International itawezesha kupanga jinsi ya kusonga mbele kwa kutumia teknolojia ya kisasa zaidi.

Nyangamalle anasema kati ya ugumu wanaokutana nao kwenye sanaa hiyo ni kazi hizo kutozungumza kama ulivyo muziki au filamu ambazo ni rahisi kwa mtu kujua ni nani aliyeigiza au kuimba.

Anafafanua: “Sanaa yetu ina changamoto kubwa na kati ya changamoto zenyewe ni hizi kazi zetu kutokuimba kama wasanii wanaoimba au kuigiza ambako ni rahisi watu kujua aliyeimba au aliyeigiza ni nani.

“Ni wazi unaweza kupata jibu kwenye hili ninalosema katika mfano wa karibuni zaidi pale watu kadhaa walipojitokeza kudai ni wachoraji/wachongaji wa Nembo ya Taifa. Kama kinyago kile kingekuwa kinaimba au kuigiza, ingekuwa rahisi kujua ni nani aliyeimba, maana tungesikia sauti ya mwimbaji.”

Rais huyo alisema kwa sasa hali hiyo inakwenda kubadilika kwa vile wameingia katika makubaliano maalumu na DataVision International ambayo itachukua jukumu la kutafiti idadi halisi na kuwatambua wasanii wa sanaa za mikono nchini na kupanga jinsi ya kuwasaidia kwa kutumia mifumo ya kiteknolojia.

Nyangamalle alisema:“Tunaamini kupitia kwa hawa wenzetu wa DataVision International, ambao wamekuwa kwenye wigo wa kufanya shughuli zao kwa kutumia njia mbalimbali za teknolojia, tutaweza kuwatambua wasanii wote nchini na kuwawezesha nao kupata faida mbalimbali ikiwamo kazi zao kutambulika ndani na nje ya nchi. Suala letu la kujua idadi ya wasanii litakuwa rahisi na hapo wasanii wanaweza kupata thamani ya jasho lao wanalovuja juu ya kazi hizi.

“Hii itafanya tuwafikie wasanii wote wa ndani ya Dar es Salaam na nje kuweza kufikiwa kwa urahisi, kuliko tukiendelea kukaa katika hali tuliyokaa huko nyuma.”

Nyangamalle akiongeza kwamba sanaa ya uchongaji haiko Dar es Salaam pekee, bali iko nchi nzima, hivyo ushirikiano wao na DataVision International kuwatambua wasanii wote kwa majina, makazi na kazi zao ambazo zote zitaweza kuonekana kwenye tovuti (Web Portal) ambayo itakuwa mahsusi kwa sanaa tu, hivyo kuwezesha watu na asasi mbalimbali duniani kote kujua uwezo wa wasanii wetu.

Kadhalika, Nyangamalle anasema hivi karibuni alikutana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, aliyehoji kwa nini sanaa za kazi za mikono hazipati kipaumbele stahiki.

“Hii ni sanaa inayohitaji vitu vidogo vidogo ili kuweza kuwa ajira rasmi kwa wasanii wenyewe." Nilipomwambia Waziri Mwakyembe mipango yetu alishangaa na kusikitika ni kwa nini sanaa yetu haipewi sifa stahiki kama zilivyo sanaa nyingine.

“Kampuni ya DataVision International ipo sokoni kwa miaka 18 sasa na imefanya kazi na taasisi mbalimbali za serikali na binafsi kuwezesha ufanyaji kazi kwa ufanisi kwa kutumia mbinu mbalimbali za teknolojia. Muungano huu kati ya DataVision International na TAFCA utawezesha sanaa yetu ifike mbali zaidi,” alisema rais huyo wa TAFCA.

Akizungumza kwa niaba ya DataVison International, kiongozi wa Kitengo cha Biashara, MacLean Geofrey, alisema wanafahamu TAFCA, ina kundi kubwa ambalo halijaunganishwa pamoja na hivyo kwa pamoja TAFCA na DataVision Inernational, itawaleta karibu kwa kuwatambua na kutengeneza 'database' ya wasanii wote nchini kisha kuwawezesha na kuwaelimisha juu ya nguvu ya teknolojia katika kupenya kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi ili waweze kusonga mbele.

MacLean anasema watamfikia kila msanii wa kazi za mikono, kujua aliko, watawasajili wote na kuwapa utambulisho ili waweze kutambulika popote waendako.

“Wasanii wa sanaa za mikono wana fursa za hali ya juu. Lakini hawajakaa katika nafasi nzuri, hivyo kuwapo kwetu ndani yao ni kuhakikisha kwanza tunawakusanya pamoja, na kuwasajili. Tukishawasajili tutafanya watambulike na hapo ndipo itakuwa rahisi kufanya kila kitu, lakini kwanza tuwasajili,” alisema MacLean akidokeza ya kuwa kati ya mikakati yao ni kufanya kazi na TAFCA kwa karibu zaidi.

Mtendaji Mkuu wa Tamthilia ya Kisasi, Edwin Musiba, alisema sanaa yao ina changamoto kubwa kama kukatishwa tamaa na watu, lakini wao kama wasanii wanatakiwa kuamini kile wanachokisimamia.

Edwin alisema kazi za sanaa za mikono ni kama kazi za kujitolea, hivyo wasanii wanapaswa kujua ni jinsi gani wanaweza kujipanga vyema na kupeleka kitu kizuri sokoni kwa mlaji.

“Niliwahi kutengeneza kazi moja nikaipeleka kwenye vituo mbalimbali vya televisheni.

Majibu niliyokuwa nikipewa yalikuwa ya kukakatisha tamaa. Lakini mara zote nilizokuwa nikikatishwa tamaa niliamini kuna siku mambo yatakuwa mazuri kupitia sanaa hii hii ambayo watu wanaibeza” alisema Edwin, mmoja wa vijana waliovutia kwa utoaji wa mchango kwenye mdahalo huo.