Unapomficha mtoto mlemavu unalenga nini, kama si ukatili?

14Mar 2019
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Unapomficha mtoto mlemavu unalenga nini, kama si ukatili?

HUWA mara zote nasema, mtoto mlemavu hakupenda kuzaliwa hivyo. Ulemavu unaweza ukatokana na mambo mbalimbali kwa mtoto, na hata sisi tulio katika hali nzurui ni walemavu watarajiwa.

Wapo wanaozaliwa na wakaugua, hivyo wakaishia katika ulemavu. Wengine, huenda wazazi wao hawakula vizuri katika ujauzito na wengine kutumia dawa bila ya ushauri wa kidaktari, nao wakaishia kuzaliwa walemavu.

Tujiulize, mtoto huyo kosa lake ni nini, mpaka mzazi unaamua kumficha na kuona kama umepata laana? Mtoto huyo ana haki kama wenzake na hatakiwi kufichwa ndani.

Anatakiwa kupelekwa shule kupata elimu itakayomsaidia katika maisha yake na wataalamu wa afya. Wanasema kuwa watoto walemavu wanapofikishwa hospitali, wanapatiwa mazoezi ya viungo, hata kutegemea na hali, lakini wanarudia taratibu hali zao.

Pia, watoto hao wanapopelekwa shule wanajitahidi kusoma na wamekuwa wakifanya vizuri masomoni.
Tumeona baadhi ya watoto walemavu,wana kipaji ikiwamo hata wengine kuchora kwa kutumia miguu.

Basi, kwa mtaji huo wa kifikra, wazazi wasififishe ndoto za watoto wao wenye ulemavu, bali wawapeleke shule wakajiendeleze na baadae kufikia hatua ya kuwa huru katika maisha yao na kuacha kuwa tegemezi.

Serikali daima imekuwa ikiwajali walemavu nchini na kuna baadhi ya majengo yamewekewa miundombinu, ili kuweza kuisaidia kada hiyo. Kimsingi, hivi sasa hicho ni kigezo muhimu katika ujenzi mpya nchini.

Kuna baadhi ya shule japo si nyingi, ambazo ama zina huduma maalum au shule nzima imeandaliwa kuwahudumia watoto walemavu.

Najiuliza, kama imefikia hatua hiyo, sasa inakuwaje mzazi aliyezaa mtoto mlemavu, akajihisi kukosa wajibu wa kuwapatia elimu vijana hao.

Inatakiwa wazazi wenye watoto waelemavu, kuwapeleka shule kupata elimu. Pia, wasifungiwe ndani, bali wachanganywe kucheza na wenzao, ili wachangamshe akili zao.

Pia watoto hao wasitengwe katika familia zao, kutokana na ulemavu walio nao. Inapobidi, mzazi anapompeleka mtoto katika kituo cha walemavu, hata yeye anaweza kujiingizia kipato kwa kufanya kazi.

Kama, mtoto ataendelea kufungiwa, ni vigumu mzazi kwa mzazi kujiongezea kipato, kutokana na sehemu kubwa ya muda utautumia kukaa na mtoto huyo nyumbani na kufanya ashindwe kujiongezea kipato.