Uporaji wa ardhi ama fursa za uwekezaji?

04Mar 2016
Restuta James
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Uporaji wa ardhi ama fursa za uwekezaji?

KUMEKUWA na uwekezaji mkubwa unaofanywa barani Afrika na wawekezaji wa nje ya bara hili ambao wanamilikishwa maeneo makubwa ya ardhi kwa miaka 99 tena wakiendesha kilimo cha mazao ya biashara kama jatrofa.

Ripoti za tafiti mbalimbali za kimataifa za hivi karibuni zinaeleza kwamba zaidi ya hekta milioni 203 barani Afrika zinamilikiwa na matajiri wakubwa waliomilikishwa kwa kisingizio cha uwekezaji.

Ripoti hizo zinaeleza kwamba ‘biashara’ ya ardhi barani Afrika, Tanzania ikiwamo inawakandamiza wakulima wadogo, maskini ambao wanapoteza rasilimali ndogo pekee waliyonayo na kubaki wakiwa hawana hata eneo la makazi.

Inaeleza kwamba kila sekunde, wananchi maskini wanapoteza ardhi yao kwa kulazimishwa kuitoa kwa wawekezaji wakubwa na kwa fidia ndogo ama bila malipo yoyote.

Nimesoma ripoti hizo japokuwa Tanzania haikutajwa sana lakini yaliyozungumzwa yanatokea pia hapa nchini. Tafiti mbalimbali zinaonyesha kwamba zaidi ya hekta milioni tatu zinashikiliwa matajiri kutoka nje kwa miaka 99.

Najua zipo kelele nyingi zimepigwa na wanaharakati wa masuala ya ardhi nchini na hata mimi niliwahi kuandika juu ya hili; leo tena ninauliza hivi hawa ni wawekezaji wa kweli ama waporaji wa ardhi?

Tunafahamu kwamba wakulima wadogo wanachangia sana katika uzalishaji wa chakula kinachoweza kutosheleza kulisha kaya. Ili kujua kipimo cha umasikini wa mtu au kaya lazima pia ujue uwezo wake wa kujilisha; lakini cha kushangaza, wakulima wadogo wanaonekana leo ni maskini wa kutupa, vipi wakikosa hata hiyo ardhi ndogo waliyonayo?

Binafsi sipingi uwekezaji, lakini lazima kama Taifa tujiulize kipaumbele chetu. Tunawanyang’anya wananchi ardhi tukitegemea watanunua chakula kwa wazalishaji wakubwa! Hii inakuwa ni biashara kubwa kwa gharama ya maisha ya mamilioni ya maskini; hakuna anayejali haki zao. Haikubaliki.

Lazima Tanzania iamke sasa, ijiulize Afrika ambayo inaongoza kwa kuuza mamilioni ya hekta za ardhi yenye rutuba ndiyo hiyo hiyo inayoongoza kwa njaa. Uwekezaji uliofanywa kwa miaka 10 iliyopita haujaleta nafuu yoyote ya maana kwa wananchi wa Afrika, tunahitaji miaka mingine mingapi kujifunza juu ya hili?

Ripoti ya Shirika la Kimataifa la Oxfam inaeleza kwamba asilimia 60 ya uwekezaji wa kilimo kikubwa ulifanyika katika nchi zinazoendelea ambazo zinakabiliwa na matatizo makubwa ya chakula. Inaeleza zaidi kwamba robotatu ya kilichozalishwa kilisafirishwa nje ya nchi hizo.

Ripoti hiyo inaonya kwamba uwekezaji huo hausimamiwi na sera wala kanuni zitakazoweza kuzuia uporaji wa ardhi na kwamba uwekezaji uzingatie usalama wa chakula wa jamii inayozunguka mradi na nchi husika.

Uwekezaji unaoendelea nchini unazingatia uwazi? Je, kunakuwa na majadiliano ya kina kuhusu faida na hasara za mradi, je, haki za wakulima wadogo zinalindwa na kubwa zaidi, usalama wa chakula unazingatiwa?

Pamoja na jitihada zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano kurejesha mashamba pori yaliyotelekezwa, ni vyema ikapitia pia mikataba ya mashamba yanayoendelezwa na kurekebisha dosari zinazoweza kutuletea madhara hapo baadaye.

Ni wiki iliyopita tu wakazi wa Kijiji cha Moa, Kata ya Moa wilayani Mkinga walitisha kikao cha dharura kwa ajili ya kumkataa Mwenyekiti wa kijiji hicho, Rambazo Abdi, pamoja na Kamati ya utendaji, wakiwatuhumu kuingia makubaliano na mwekezaji kwa kumpatia kinyemela eneo lenye ukubwa wa ekari 2,491 kwa ajili ya kuchimba chumvi.

Mwekezaji anadaiwa kupewa eneo hilo kwa miaka 33 wakati wananchi wa kijiji hicho wakiwa hawana eneo la makazi wala kilimo.

Mifano ni mingi na ninadhani hili jambo linapaswa kutazamwa upya.
Mungu Ibariki Tanzania.