Usafirishaji makontena changamoto kwa watumiaji barabara

17Mar 2017
Jenifer Julius
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Usafirishaji makontena changamoto kwa watumiaji barabara

USAFIRISHAJI makontena makubwa jijini Dar es Salaam kwenda nchi jirani au mikoani ni jambo la kawaida kabisa. Yaani kukutana na kupishana nayo barabarani ni utaratibu uliozoeleka.

Miongoni mwa mizigo hiyo husafirishwa kwenda nchi za nje kwa ajili ya matumizi wanayoyafahamu wao.

Baadhi yake husafirishwa kwenda kwenye masoko ya kimataifa kama vile Kenya, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Marekani.

Mizigo mingi hufungiwa katika makontena kwa ajili ya usalama wake. Makontena huwasaidia wafanyabiashara kusafirisha mizigo mikubwa wakiwa na uhakika wa usalama wa mali zilizomo.

Hata hivyo, kuna jambo ambalo naona kuwa halikukaa vyema katika mchakato huo. Yaani ni kuhusu namna yanavyofungwa au kudhibitiwa ili yasianguke hata kuhatarisha usalama wake na watumiaji wengine wa barabara.

Baadhi ya wasafirishaji wa makontena hayo wanayafunga katika namna ambayo ni hatarishi kwa waendesha magari yanayobeba makontena hayo. Hali halisi ilivyo ni kwamba, hawayafungi vyema. Yaani huyashikiza tu kwenye magari na kujikuta maisha ya watu wengineo yanawekwa rehani.

Kwa kawaida, makontena hayo hutakiwa kufungwa kwa nati maalum pande zote nne, hasa kwenye kona zake na ikiwezekana kushikizwa na minyororo kutegemeana na ukubwa wa mzigo uliopakiwa.

Unaweza kukutana na gari imebeba kontena ikiwa imepachikwa tu bila kufungwa na minyororo, hali ambayo ni hatari kwa maisha ya watu, kutokana na ukweli kuwa, kontena inaweza kuanguka muda wowote hata kusababisha maafa.

Baadhi yao hawafungi kwa kigezo kuwa makontena hayo yanapelekwa eneo la karibu hivyo kuona usumbufu kufunga na kufungua kwa muda mfupi. Hayo hufanywa na watu ambao kuna kila dalili kuwa, hujali uharaka kuliko athari itakayotokea kama kontena hilo likiteleza na kudondoka.

Mara kadhaa zimetokea ajali za makontena kuanguka na kusababisha maafa hasa eneo ambalo gari hulazimika kukata kona. Mathalani maeneo ya Tazara imewahi kutokea gari kuangusha kontena hilo wakati ikikata kona kuelekea Gongo la Mboto.

Ukichunguza kwa makini, utabaini kuwa kontena hilo lilikuwa halijafungwa na kushikiliwa kwenye gari inavyostahili.

Hii ni kutokana na ukweli kuwa, si rahisi kontena kuanguka kama litakuwa limeshikiliwa vizuri kwenye magari.

Ufike wakati madereva na wamiliki wa magari yanayobeba makontena haya, wazingatie sheria za usalama barabarani na ubebaji wa mizigo hasa mizigo mikubwa. Kwa kufanya hivyo, hawalindi maisha ya kwao tu pia ya watu wote ambayo yanawekwa hatarini bila ya sababu za msingi.

Ni muhimu Jeshi la Polisi kufuatilia suala hili kwa makini na kuwachukulia hatua kali wote wasiofunga makontena hayo kwenye magari ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika.Wanapaswa kufuatilia makontena haya kwa ukaribu zaidi, kwani kwa mbali sio rahisi kugundua ukweli ulivyo.

Wamiliki na wanaokodisha magari haya hawana budi kuhakikisha kuwa, makontena yanayobebwa yamefungwa, sio tu kulinda usalama wa wananchi pia kukuepushia hasara inayozuilika ikitokea kontena likaanguka kwa sababu halijafungwa vyema .

Pia wananchi tunao wajibu wa kukemea jambo hili kwa kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi, iwapo utakutana na gari lenye kontena ambalo halijafungwa ipasavyo.

Tushirikiane kuepusha janga hili kwani lisipokukuta wewe linaweza kumkuta mwenzako. Chukua hatua sasa.