Usanifu wa lugha wapelekwa arijojo

10Jan 2017
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
Usanifu wa lugha wapelekwa arijojo

KWA mujibu wa Kamusi la Kiswahili Fasaha, Kiswahili kilianza kusemwa na kundi la watu waliojinasibu kwa sifa za kijamii zilizowaunganisha na kisha kusambaa katika makabila mbalimbali ya mwambao wa Afrika mashariki.

Nchini Tanzania, Kiswahili ndio lugha ya taifa na sasa yazungumzwa takriban nchi zote duniani. Pamoja na ukweli huu, twashindwa kutumia maneno sahihi (-siokuwa na makosa) ya Kiswahili! Ukisoma kwa makini magazeti yetu utagundua makosa mengi ya lugha na mtiririko m-baya wa sentensi.

Nazungumzia makosa ya magazeti ya kila siku. Sitoandika majina ya magazeti, ila kama watenda kazi wao, (hasa wanaodurusu kabla ya kupelekwa mitamboni), watasoma safu hii,watagundua kuwa makala haya yanawahusu.

Bismillahi! “Tangazo hilo ambalo lilimwamuru aondoke katika jengo hilo ndani ya masaa ishirini na nne ambapo licha ya mvutano huo kutokea, iliendelea ambapo gazeti hili lilishuhudia magari yakiingia na kutoka kuondoa mali hizo.”

Kwanza ‘saa’ haina wingi kwani neno hilo lipo kwenye umoja na wingi. ‘Saa’ ni moja na zaidi ya moja pia ni ‘saa’ kwa hiyo si sahihi kuipa saa kipashio ‘ma.’

Pili sentensi ya mwandishi imekorogwa sana kiasi cha kutoeleweka. “ …ambapo licha ya mvutano huo kutokea, iliendelea ambapo gazeti lilishuhudia magari yakiingia na kutoka kuondoa mali hizo.” Ilipitaje kwenye mikono ya watu wasiopungua watatu bila kugundulika makosa?

“Majanga: Black Chunas apigwa stop kutumia jina la kardashian.” Hili neno la mwisho ni jina la mtu hivyo herufi ya kwanza lazima iwe kubwa ‘K’ yaani Kardashian lakini limeandikwa kwa herufi ndogo -- kardashian!

Kadhalika neno ‘stop’ si Kiswahili lakini waandishi wetu hawafurahi bila kulitumia kwenye vichwa vya habari na makala zao kana kwamba hakuna neno la Kiswahili! Badala ya “ … apigwa stop kutumia jina la Kardashian” ingeandikwa “ … azuiwa kutumia jina la Kardashian” au “ … akatazwa kutumia jina la Kardashian.”

Vichwa vingine vya habari huandikwa kihuni kama hiki kifuatacho kwenye gazeti hili unalosoma sasa: “Mtunzi nyota asiyefagilia misifa.”

Tuanze na neno ‘fagilia.’ Maana ya neno hili ni ondoa uchafu kwenye sakafu au ardhi kwa ufagio; toa taka; ii) ondoa kila kitu: Wezi wamemwibia na kumfagia kila kitu.

Kuhusu ‘misifa’ sipati maana yake kwa Kiswahili. Nadhani mwandishi alikusudia neno ‘sifa’ lenye maana ya: i) mafuta yanayotengenezwa kwa matumbo ya samaki na hutumiwa kupakia n-nje ya chombo cha majini cha mbao ili kukikinga kuliwa na wadudu.

ii) hali ya kupendeza au kutopendeza kwa kitu au mtu. ‘Sifika’pia ‘sifikana’ ni kitendo cha kupata sifa juu ya jambo. ‘Sifu’ ni kitendo cha kueleza hali ya jambo, kitu au mtu kupendeza.

‘Sifa’ haina wingi hata isemwe ‘misifa’ au ‘masifa!’ Huu ni upotoshaji wa lugha.

“Yanga ni tizi la kufa mtu” ni kichwa cha hbari ya gazeti la michezo. Chini ya kichwa hicho kuna maelezo yafuatayo:

“Kocha wa Yanga Mzambia George Lwandamina, anatambua kwamba anayo majukumu makubwa mbele yake ya kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri katika michuano ya ndani na ile ya kimataifa hivyo ameamua kuwahenyesha wachezaji wake kwa kuwapigisha tizi la kufa mtu ili kuwajengea stamina na pumzi.”

Tatizo la waandishi wa habari za michezo ni matumizi ya maneno mengi yasiyo na umuhimu. Kwa mfano sentensi niliyoinukuu hapo juu ina maneno 43 katika sentensi moja inayochosha kuisoma.

“Kocha wa Yanga Mzambia George Lwandamina …” Tangu awasili nchini kuifundisha timu ya Yanga ameandikwa kwa mapana na marefu kwa hiyo hakukuwa na sababu za msingi kumtaja tena kuwa ni Mzambia.

Ni kocha gani asiyeelewa majukumu yake hata mwandishi aeleze “ … anatambua kwamba anayo majukumu makubwa mbele yake ya kuhakikisha timu inafanya vizuri katika michuano ya ndani na ile ya kimataifa…?” Hakuna kocha yeyote duniani asiyetaka timu yake ishinde.

Mwandishi kaandika: “ameamua kuwahenyesha wachezaji wake na kuwapigisha tizi la kufa mtu …” Hapa nitazungumzia maneno yafuatayo: ‘kuwahenyesha’, ‘tizi’ na ‘kufa mtu.’

Kwanza nina shaka kama neno ‘henyesha’ ni Kiswahili. Naomba nieleweshwe kwani silipati katika lugha ya Kiswahili.

Pili, ‘tizi’ pia si Kiswahili ingawa waandishi wa michezo hulitumia sana kwenye habari na makala zao. Kwa hakika neno hili limetoholewa kutoka Kiingereza cha ‘practice’ yaani mazoezi.

Isemwapo ‘zoezi’ maana yake ni utendaji wa jambo unaorudiwa ili kupata ufanisi; jaribio linalofanywa ili kuthibitisha ubora wa kitu.

Tatu, ‘kufa mtu’ maana yake ni mwanadamu (mtu) kupoteza uhai wake. Kwani wachezaji hufanyizwa ‘zoezi la kufa’ au la mpira?
Methali: Kuchamba kwingi mwisho …(ashaakum).

[email protected]