Ushirika unapokiuka malengo yake, kudumu ni kitendawili

15May 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ushirika unapokiuka malengo yake, kudumu ni kitendawili

KATIKA harakati za kujikomboa kiuchumi, vyama vya ushirika vimekuwa na mchango mkubwa kutetea hali ya uchumi kwa wanachama na wanajamii kwa ujumla.

Hilo limo katika majukumu muhimu yanayofanywa na vyama hivyo vya ushirika katika kupunguza umaskini na kukuza huduma za kiuchumi, kibiashara na masoko kwa wakulima wadogo.

Vilevile, inawapa sauti wadau wanyonge, kuwaletea ustawi wa jamii, kutengeneza ajira, kurahisisha upatikanaji huduma za kifedha na kuwezesha wakulima na jamii kwa ujumla.

Aidha, vyama hivyo ambavyo ni nguzo muhimu katika jamii, vina mchango mkubwa katika kuinua hali za kiuchumi za wanachama, kuwaunganisha wananchi wa hali ya chini, ili waweze kujitambua na kuunganisha nguvu zao katika kujiletea maendeleo.

Pia, vyama vya ushirika vinatajwa kuwa na uwezo wa kuwaunganisha wanyonge, ili waweze kutetea haki zao na kuwapa uwezo wa kujadiliana na kupambana na walanguzi ili kupata bei bora ya mazao yao.

Hata hivyo, kuna baadhi ya vyama hivyo vimekuwa vikikabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwamo zinazosababisha na viongozi na kusababisha wanachama kuvikimbia.

Miongoni mwa changamoto zilizopo ni tabia ya uendeshaji wa vyama hivyo, bila ya kufuata taratibu na kuna wakati wakulima ambao ni wanachama walidhulumiwa fedha za mauzo ya zao yao, kupitia vyama vyao.

Ni hivi karibuni, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, aliainika katika faragha yake na Nipashe kwamba, Ripoti ya Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika ya Mwaka 2018/2019 kwa Kamishna Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru), Brigedia Jenerali John Mbung’o, ilikuwa na 'madudu' mengi.

Ukaguzi huo ulibaini ubadhirifu wa zaidi ya Sh. bilioni 124.5 uliofanywa na vyama vikuu vya ushirikia vya akiba na mikopo maarufu ‘saccos’ na vyama vya msingi vya mazao vinavyojulikana kama ‘amcos.’

Kupitia taarifa hiyo, ilibaini kuwapo vyama vya ushirika vilivyokiuka misingi ya uendeshaji na vikaumbuka na yaliyo kinyume na misingi ya kisheria na kanuni za uendeshaji ushirika nchini.

Ni siku kadhaa zilizopita, Waziri Hasunga alitangaza kufuta usajili wa vyama vya ushirika 3, 348 vilivyokuwapo rasmi kisheria, baada ya kupatiwa notisi ya kusudio hilo, sababu kuu inatajwa vilikuwa havitekelezi majukumu yake ya msingi kwa mujibu wa usajili uliotolewa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini.

Kuna msemo wa Kiswahili ‘ukiona mwenzio ananyolewa na wewe tia maji.' Binafsi nasema, hilo linapaswa kuwa fundisho kwa vyama vingine vya ushirika vilivyobaki, vibaki katika mstari wa kisheria, katika uendesha shughuli zake kwa namna inavyotakiwa.

Ikumbukwe kwamba waziri huyo mwenye dhamana, ameshaweka wazi kwamba, hatua ya kuvifuta vyama vinavyokiuka misingi na kanuni za usajili wake, utakuwa endelevu dhidi ya vyama vya ushirika vitakavyoshindwa kutekeleza malengo ya uanzishwa wake, kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika iliyopo.

Kinachosisitizwa na waziri, ni uadilifu katika utendaji ili vyama vya ushirika viendelee kuwa nguzo imara ya kuwakomboa wananchi kutoka kwenye umaskini, kwani vina mchango mkubwa katika kuboresha maendeleo ya nchi.

Iwapo vyama vya ushirika wa mazao, akiba na mikopo na aina nyingine vitajiendesha vizuri, kuna uhakika wa kutoa ajira kwa wanachama wake na ndio ngazi mojawapo muhimu ya kupiga hatua kimaendeleo.

Hivyo suala la kujiendesha kwa kuzingatia misingi ya uanzishaji wake ni njia ambayo kwa namna moja au nyingine inaweza kusaidia vyama kutimiza hayo na vikaaminika kwa wanachama.

Hapa sibahatishi kutumia mfano wa Chama cha Ushirika cha Umoja, kilichopo mjini Liwale mkoani Lindi, kwa kufanikiwa kuwasomesha wanachama wake na waliopata utaalamu wa mambo ya fedha na kisha wakawaajiri.

Ni hatua nzuri, kwani badala ya kuajiri wataalamu kutoka nje, kikaona umuhimu wa kuwaendeleza wanachama wake na kisha kutumikia kuiweka sawa hesabu zao za fedha, wakiwa ni wataalamu wa ndani waliiopiga hatua za ujuzi na maarifa.