Ushirikiano unahitajika kuokoa hasara mamilioni kwenye mbolea 

11Jun 2021
Beatrice Moses
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ushirikiano unahitajika kuokoa hasara mamilioni kwenye mbolea 

MAMLAKA ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) imebainisha namna ya kuagiza mbolea kutoka nje ya nchi, hali iliyokuwa ikiigharimu nchi kutumia matrilioni ya fedha za kigeni.

Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Dk. Stephan Ngailo, amewaambia waandishi wa habari, kuelezea kuhusu maagizo ya Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Faustine Mkenda, kwenye ziara ya kikazi kwenye ofisi za mamlaka hiyo Jumatatu Juni 7, 2021.
 
Dk. Ngailo alisema, kwa mwaka jana pekee zilitumika zaidi ya Dola za Marekani milioni mbili (Sh. blioni 4.6) kuagiza mbolea nje ya nchi, ambako kwa hali ilivyo, asilimia 90 ya mbolea inayotumika nchini inaagizwa kutoka huko wakati asilimia 10 tu ndiyo inayozalishwa hapa nchini. 

Zimetumika zaidi ya Dola za Marekani trilioni 1.6  kuanzia mwaka 2017 hadi 2020, kiasi ambacho kinaweza kupunguzwa, iwapo tutafanikiwa kuzalisha mbolea kwa wingi nchini.
 
Maagizo ya Waziri Mkenda, ni pamoja na kuitaka TFRA kuongeza muda wa kufungua zabuni kwa mwezi mmoja mpaka Julai 8, 2021. Awali ilipaswa kuishia Juni 18 kwa lengo la kupata washiriki wengi zaidi ya 13 waliopo sasa, ambao ni kutoka ndani na nje ya nchi.
 
Hatua hiyo, inalenga kuongeza ushindani na hatimaye kupata bei shindani na nafuu kwa mkulima hivyo itasaidia wengi wamudu kuweka  mbolea ya kupandia na kukuzia mazao, hivyo kuweka uwezekano mzuri wa mazao kustawi  vizuri na kuwezesha mavuno, pia  mazuri.   
 
TFRA wameagizwa kuhakikisha tangazo la zabuni hiyo linapelekwe kwenye ofisi za balozi za Tanzania kwenye nchi zinazozalisha mbolea duniani, kupitia Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa nia ya kupata washiriki. Mfano; Russia, China, Saudi Arabia, Qatar, Morocco, Ukraine na Uturuki. 
 
Waziri ameagiza TFRA kupeleka tangazo la zabuni kwenye balozi za nchi zinazozalisha mbolea zilizopo hapa nchini, na iendelee na utaratibu wa kutangaza zabuni za BPS kwa kuwatumia wazubuni walioko kwenye kanzidata ya mamlaka, ili kuhakikisha mbolea zinawasili nchi kwa wakati kwa msimu wa kilimo 2021/2022.

Wahenga wanasema ‘umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu.’ Hivyo, ili maagizo hayo yote ya waziri ili yaweze kufanikiwa, kunahitajika ushirikiano mzuri kutoka kwa mabalozi na Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Kituo cha Uwekezaji.

TFRA imeagizwa kuandaa mkakati wa uanzishwaji wa viwanda vipya vya mbolea, ili kuongeza uzalishaji pembejeo hiyo nchini, ina jukumu kubwa kuhakikisha uzalishaji mbolea nchini unapewa kipaumbele.

Waziri anaamini kuwa, kwa kuongeza uanzishwaji wa viwanda vipya ni hatua itakayosaidia mbolea kupatikana kwa urahisi na kwa bei nafuu, hivyo kila mkulima atamudu kuinunua na kuitumia, hatua itakayoongeza uzalishaji mazao bora.

Hivyo, TFRA imetakuwa kubuni mkakati wa namna bora ya kuongeza uwekezaji nchini, kwa kuwa ndiyo itakuwa suluhisho la kuwahakikishia unafuu wa bei za pembejeo mbalimbali, ikiwamo mbolea.

Waziri wa Kilimo Profesa Mkenda, tangu alipokabidhiwa kuongoza wizara hiyo, alibainisha wazi kuwa atahakikisha sekta ya kilimo inaongeza kuchangia kukuza uchumi toka asilimia 28 iliyopo sasa, pia amekusudia sekta ya kilimo ikitoa mchango mkubwa kwenye upatikanaji malighafi ya viwanda.

Anaeleza wazi kusudi lake kuhakikisha sekta ya kilimo, akitaja mambo makuu manne, ambayo dira yake inajumuisha kuongeza tija kwenye uzalishaji mazao ya kilimo kwa kutumia eneo dogo kuvuna mazao mengi.

Pia, kuna mtazamo wa kusimamia na kuelimisha mbinu bora za uzalishaji, pamoja na kufanya umwagiliaji kwa njia ya matone ukue na kuchangia upatikanaji wa chakula kwa uhakika.

Profesa Mkenda, pia aliahidi kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya uhakika wa mazao ya wakulima na kusimamia masoko ya kimkakati ili wakulima wanufaike na upatikanaji wa mitaji na uwekezaji kwenye kilimo na upatikanaji wa mikopo kutoke taasisi za fedha nchini na zile za nje ya nchi yenye riba nafuu.

Kwa kuzingatia maoni hayo ya profesa, yanaweza kutoa nafasi kuanzishwa mpango mkakati unaotakiwa ili kuwawezesha hata wazawa wenye nia ya kujenga viwanda hivyo vya mbolea, kupata mitaji kwa kupitia mikopo yenye riba nafuu.