Ushirikiano wa wafanyabiashara Mwenge unavyowakonga wateja

30Jul 2017
Beatrice Bandawe
Nipashe Jumapili
Tuzungumze kidogo
Ushirikiano wa wafanyabiashara Mwenge unavyowakonga wateja

UKIPITA eneo la stendi ya Mwenge jijini Dar es Salaam, lazima utasimamishwa na watu wasiopungua watano kila mmoja akikukaribisha katika biashara yake iwe ya kusuka nywele, kupaka rangi kucha, kubana nywele na nyingine kadhaa.

Hata hivyo, si wote wanaokusimamisha wanafanya biashara hiyo, la hasha. Wengi wanaowaita wateja mara nyingi ni madalali wa kupeleka wateja kwa wanaohusika wanaofanya shughuli hizo.

Udalali huo hufanywa na kinadada na kinakaka wakiwamo Wamasai, ambao wamezoeleka kuonekana wakilinda kwenye nyumba za
watu au maduka, ambao sasa wamejaa katika eneo hilo wakifanya shughuli ya ususi wa nywele na udalali wa kutafutia wateja saluni nzuri za ususi.

Mara nyingi mtu anapokwenda kusuka, ni kawaida kuwakuta kinadada kadhaa wamezunguka eneo hilo wakisubiri kupata tenda ya kuchambua rasta na kusaidia kusokota nywele na ujira huupata kwa makubaliano na msusi mkuu.

Kazi hizo hufanywa kwa ushirikiano ili kuhakikisha kila mtu aliyepo eneo hilo kwa siku anaingiza kipato chake.

Ushirikiano huo umewafanya wafanyabiashara hao kuwaunganisha na kuwa na umoja uliowawezesha kucheza michezo ya upatu inayowasaidia kujiinua kiuchumi.

Pamoja na eneo hilo kuwa maarufu kwa biashara ya nguo za mitumba, kinadada na kinamama huenda kujipendezesha kuanzia nywele hadi kucha.

Vijana wengi wa kiume wamejiingiza katika biashara ya urembo wa kuwapaka rangi za kucha na kusafisha miguu ya kinadada kazi ambayo imewapatia ajira na kujiepusha na makundi maovu.

Mtu anapokwenda kusukwa huulizwa kama anataka huduma nyingine ikiwamo ya kuchongwa nyusi, kusuguliwa miguu na kupakwa rangi na huunganishwa kwa wenzao wanaofanya kazi hiyo hasa kina kaka.

Kinakaka wengi wamejifunza kazi zinazofanywa na wanawake ikiwamo kusuka, kubana mitindo mbalimbali ya nywele inayowafanya kinadada kurudi kila mara kupendezesha nywele zao.

Licha ya kazi hizo, kuna wanaotembeza bidhaa mbalimbali zikiwamo za vyakula, urembo na nguo na kila mmoja hupata riziki yake kwa jinsi atakavyo changamka na biashara yake.

Ushirikiano wa wafanyabiashara hao umewafanya vijana wengi katika eneo hilo kila siku kupata kipato na kuepuka malalamiko ya kukosa ajira.

Baadhi ya vijana hao wamesoma hadi elimu ya juu, lakini wameamua kufanyakazi hiyo baada ya kukaa muda mrefu bila kupata ajira kutoka mashirika au kampuni mbalimbali.

Kwa hali ya sasa, vijana wengi wameamua kujiingiza katika biashara mbalimbali na kuondoa ile dhana ya kuwa unapokuwa msomi huwezi kufanyakazi za watu wasiokuwa na elimu kama ya kwao.

Wahenga walisema mtembea bure, si mkaa bure. Mtu yeyote anayejishughulisha na kitu chochote hawezi kukosa hela ya kumsaidia kuishi, tofauti na yule aliyekaa akisubiri kazi imfuate nyumbani.

Uchakarikaji unaofanywa na vijana wa stendi ya Mwenge, umeanza kuigwa pia katika maeneo mengine na kuwafanya vijana wengi kuboresha maisha yao.

Kuchagua kazi mara nyingi ndiko kunakowafanya vijana wengi kukaa wakilalamika kukosa ajira, lakini kazi za ujasiriamali zimewakomboa wengi na wengine waliofanikiwa wamekataa kabisa kusikia habari ya kuajiriwa.

Ubunifu pia ni njia moja ya kuwakomboa vijana kutoka kwenye tatizo la ukosefu wa ajira na kuwapeleka katika ulimwengu wa kujitegemea.

Vijana wanaonekana katika ujasiriamali wa aina tofuati, walibuni njia za kujipatia ajira na wenzao wakaiga na sasa wamesahau habari ya kulilia ajira.

Hata hivyo, ni muhimu mtu anapobuni njia yake, mwingine akafiria njia ya kuboresha badala ya kuigana na mwishowe watu kuanza kushikana uchawi.

[email protected]; Simu: 0774 466 571