Usiri wa TFF unavubaza soka

14May 2016
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Usiri wa TFF unavubaza soka

‘USIRI’ ni ajizi aliyonayo mtu katika kufanya jambo. Ndio maana wahenga walisema: “Ajizi nyumba ya njaa.”
Ajizi ni uzembe au ucheleweshaji wa kufanya jambo. Maana yake usiri wa kuamua au hata uzembe ni ufunguo wa ufukara au umasikini.

Hivi karibuni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), liliipokonya Azam FC alama (pointi) tatu na mabao matatu iliyopata dhidi ya Mbeya City Februari mwaka huu na kuinufaisha timu hiyo ya Mbeya kwa mabao matatu na alama tatu sawia.

Kwa mujibu wa kanuni namba 37(4) ya Ligi Kuu ya Bara ya mwaka 2015 na kanuni ya 14(37) , mchezaji anayeoneshwa kadi tatu za njano katika mechi tatu hataruhusiwa kucheza mchezo unaofuata.

Adhabu ya Azam FC imesababishwa na mchezaji wake, Erasto Nyoni kuchezeshwa dhidi ya Mbeya City ilhali alikwishaoneshwa kadi tatu za njano katika michezo iliyopita.

Simba ilipata kuadhibiwa kwa kosa kama hilo ilipomchezesha Mussa Hassan ‘Mgosi.’ Vilevile Yanga ilipomchezesha nahodha wake, Nadir Haroub ‘Canavaro’ katika mechi dhidi ya Costal Union ya Tanga msimu wa mwaka 2011/2012.

Mpaka adhabu ya wachezaji waliooneshwa kadi tatu za njano kusimamishwa kucheza mchezo mmoja ilipopitishwa na TFF, kilabu zote za Ligi Kuu inayodhaminiwa na Vodacom (VPL) vilishirikishwa. Kwa hiyo suala kwamba vilabu havijui sheria hiyo halina mjadala.

Kinachoshangaza ni usiri (ajizi katika kufanya jambo) wa klabu na TFF yenyewe. Ilikuwaje shirikisho hilo licheleweshe hukumu dhidi ya Azam FC kwa zaidi ya miezi miwili?

Au ni kufuata mtindo wa Jeshi la Polisi la “ushahidi haujakamilika” hata kwa miezi kadhaa, huku watuhumiwa wakiendelea kuwa mahabusu?

Ina maana, TFF haina kamati inayofuatilia michezo ya timu shiriki? Je, ‘mabenchi ya ufundi’ hujazana eneo wanalokaa wachezaji kuangalia soka tu bila kuweka kumbukumbu ya mambo yanayotendeka viwanjani?

Kazi za mabenchi ya ufundi ni pamoja na kuweka kumbukumbu muhimu za mechi, ikiwemo kuorodhesha matukio ya wachezaji wasio na nidhamu au uungwana mchezoni na wanaooneshwa kadi za njano au nyekundu.

Je, kadi hizo hutolewa kwa haki, bahati mbaya au uonevu? Aidha kuwaonya wachezaji kutofanya mambo yaliyo kinyume cha kanuni za mchezo wa soka.

Tukirejea kwenye mada yetu, kitendo cha kuipoka Azam FC ushindi dhidi ya Mbeya City dakika za m wisho wa msimu wa Ligi Kuu kimeisononesha (huzunisha) na kuifanya iyumbe.

Jambo hili lanikumbusha ile methali ya “Chendacho mavani hakina marejeo.” ‘Mava’ ni makaburi. Methali hii yatufunza kuwa kitu kilichotwaliwa na anayetuzidi nguvu hatuwezi kukipata tena. Pia yatuhimiza kuvitunza vizuri vitu tulivyo navyo.

Kwa muktadha ninaoujadili, ‘vitu’ nina maana ya klabu za soka kuelewa kanuni, sheria na haki zao. Zapaswa kuchukua hatua sahihi na kwa wakati muafaka dhidi ya kasoro zitokeazo viwanjani.

Suala la Azam FC kupokwa ushindi wa mabao matatu na alama (pointi) tatu limeacha maswali mengi miongoni mwa wapenzi wa soka nchini.

Kosa la Azam FC kumchezesha Erasto Nyoni aliyeoneshwa kadi tatu za njano mara tatu kwa mchezo usio wa kiungwana lililalamikiwa na timu ya Mbeya City? Kama jibu ni ndio, mbona TFF lilichukua muda mrefu kuamua?

Je, shirikisho hilo halikujua mapema kosa la Azam FC ili lilijua baada ya Mbeya City kulalamika (kama ililalamika)? Kama halikuwa na kumbukumbu hiyo, wajibu wake viwanjani ni kitu gani?

Mpaka nilipokuwa naandaa makala haya, zilipatikana habari kuwa Azam FC ilikuwa imekata rufaa dhidi ya adhabu hiyo.
Imeelezwa kuwa rufani ya Azam FC kwa TFF itatolewa uamuzi kabla Ligi Kuu haijafikia tamati.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Shirikisho TFF, Alfred Lucas, kikao cha kamati husika inayoongozwa na Abbas Tarimba hakijapangwa kwa sababu Azam FC haikukata rufani kwa hati ya dharura.

Afisa Habari Alfred Lucas alisema: “Rufani hukatwa kwa hati ya dharura kama jambo ni la dharura sana. Tulipokea rufani ya Azam kwa hati ya kawaida na tunaifanyia kazi. Tumempa mwenyekiti wa kamati ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kuitisha kikao.”

Wakati wapenzi wa soka, na hasa wale wa Azam FC wakisubiri uamuzi wa rufaa yao, kocha Stewart Hall wa timu hiyo amewaaga wachezaji wake akitaja mambo yaliyomfanya aondoke.

Moja ni kukiri kuwa hakuna lolote analoweza kuifanyia timu hiyo kupata mafanikio zaidi. Pia anasema tatizo lingine ni ubovu wa uendeshaji wa soka nchini unaofanywa na TFF.

Aidha alisema Tanzania haina viongozi wa mpira na waliopo wanawaza zaidi jinsi ya kupata hela tu kupitia mchezo huo! Kweli bwana. Kimya kingi kina mshindo mkuu.

[email protected]
0715/0784 33 40 96