Usishue dau na maji yajaa

08Jun 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Usishue dau na maji yajaa

IBRAHIM Ajibu, usiteremshe au kuvuta dau majini ikiwa maji yamejaa. Methali hii ni muhimu kwako kukufunza umuhimu wa kutenda jambo wakati ufaao ili usije kujihatarisha au kujiletea maangamizo.

Ajibu, wahenga walisema “Bahati ikibisha hodi sharti ufungue mlango mwenyewe.” Yaani jambo la kheri likikufika wapaswa kulifurahia. Hii ni methali ya kuwanasihi au kuwashauri watu (wewe ukiwa mmoja wao) wanaopata nafasi nzuri ya kujifaidi lakini wakacheleachelea au kutoitaka!

    Husemwa “Mcha bahari hapendi safari” maana yake mtu anayeogopa bahari hapendi kusafiri.Twanasihiwa kwamba tudhamiriapo kulifanya jambo tusiwe na uchelewevu, ajizi ya kulikabili au tusiwe na woga.    

    Zipo habari kwamba Ajibu anawaniwa na Simba, timu aliyoiacha na kujiunga na Yanga msimu uliopita na sasa mkataba wake umefikia ukomo. Yasemekana kapewa kiasi fulani cha fedha na bilionea wa Simba, Mohammed Dewji "MO" ili kumrejesha ‘kundini’ katika klabu hiyo iliyotwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu wa pili mfululizo.

    Wakati huo huo, timu maarufu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), pia ilitangaza nia ya kumwania kijana huyo kutokana na uwezo wake wa kulichezea gozi la ng’ombe kama utakavyo na kuwaburudisha watazamaji wa timu yoyote unayoichezea. TP Mazembe ni moja ya timu maarufu zaidi Afrika inayomilikiwa na bilionea mwenye machimbo ya madini nchini humo.

TP Mazembe ndio iliyomfungulia mlango Mbwana Samatta anayechezea timu ya KRC Genk ya Ubelgiji na kusababisha wenyeji wamwite ‘Samagoal’ kwa jinsi anavyofunga mabao hata kuiwezesha timu yake kutwaa ubingwa wa ligi nchini humo.

Samatta ni zao la Simba kisha TP Mazembe na sasa KRC Genk ya Ubelgiji aliyoiwezesha kutwaa ubingwa huku akiibuka mchezaji bora wa mwaka mwenye asili ya Afrika kati ya wachezaji wote wanaocheza kandanda nchini Ubelgiji.

 Thamani ya Samatta imevuka nje ya Ubelgiji kwa kutajwa kutakiwa na timu za Watford, Leicester City na Burnley za Englanda. Kuna habari kuwa timu ya Aston Villa inamhitaji Mtanzania huyo kwa udi na uvumba na imemtengea pauni milioni 12 za Uingereza, sawa na Shilingi bilioni 40 za Tanzania! Mbali ya timu za Uingereza zinazomhitaji Samatta, pia kuna timu za FC Roma ya Italia na Lyon ya Ufaransa.

Simpingi Ajibu kujiunga na timu yoyote aipendayo kwani “kipenda roho hula nyama mbichi.” Roho ikipenda huweza kula hata nyama mbichi. Pia kitu anachokipenda mtu au inachokipenda roho ya mtu huwa ni kama dawa yake. Methali hii hutumiwa kumpigia mfano mtu anayeelekea kukipenda kitu sana ingawa wengine wanakiona kuwa kibaya.

    Masikini na umasikini wake hulala fofofo akimwachia Mungu matatizo yake yote. Siku zote Mungu yuko moyoni mwake akisema: “Kupata kuna Mungu ukikosa shukuru.” Maana yake kukipata kitu au kukikosa ni mapenzi ya Mungu. Twapaswa kumshukuru japo hatukupata.

Ajibu anapaswa kutambua kuwa mchezaji anayecheza kandanda Ulaya ana faida mbili kubwa, kwanza anapata ujuzi na ufundi zaidi wa mchezo huo unaopendwa sana duniani. Pili, mshahara anaolipwa hauwezi kulinganishwa na mshahara anaolipwa mchezaji yeyote humu nchini hata wale wanaotoka nnje ya Tanzania.

Ni rahisi tu kuangalia maendeleo ya Samatta tangu ajiunge na klabu ya KRC Genk. Amejenga jumba lake la maana kule Kigamboni jijini Dar es Salaam, pia anajenga Msikiti utakaowasaidia waumini wa dini ya Kiislamu kufanya ibada zao.

Kama hiyo haitoshi, sasa Samatta anashirikiana na msanii Ali Kiba kukusanya fedha ili kuwasaidia watu wasiojiweza. Huu ni mwaka wa pili timu za wachezaji hao zikicheza jijini Dar es Salaam na mara zote timu ya Samatta imeondoka na ushindi mnono dhidi ya timu ya Ali Kiba. Mwaka ujao mchezo wao utahamishiwa mkoa utakaotajwa baadaye.

‘Auni’ ni kitendo cha kumsaidia mtu mwingine ili aondokane na matatizo; msaada, muawana. Sikuamini kama Watanzania ndivyo tulivyo linapokuja suala la kuwasaidia wenzetu wasiojimudu! Mchezo ule haukuwa wa kuwanufaisha Samatta na  Kiba, bali kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye uhitaji.

“Katika mambo yote nimewaonesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, ‘Ni heri kutoa kuliko kupokea!’” (Matendo 20:35).

Sichukii Ajibu kwenda Simba wala sifurahii kuendelea na Yanga, kinachonisikitisha ni yeye kutojitambua. Hakuna anayependa kuishi maisha yale yale mpaka mwisho wa dahari (milele) bali hutaka kuwa na maisha bora zaidi.

Ajibu, achana na ushabiki wa Simba na Yanga, kajiunge haraka na TP Mazembe ili ujifungulie njia ya kwenda ng’ambo utakakopata maendeleo na maisha mazuri zaidi kuliko kuzing’ang’ania Simba au Yanga. Kokote utakapokwenda ugenini, acha lelemama na uvivu.

[email protected]

0784  334 096