Ustaarabu unahitajika kwa mashabiki Ligi Kuu ikirejea

01Jun 2020
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ustaarabu unahitajika kwa mashabiki Ligi Kuu ikirejea

JUNI 13, Ligi Kuu Tanzania Bara, Ligi Daraja la kwanza na Ligi Daraja la Pili Tanzania Bara zitarejea tena ili kupata bingwa, timu zitakazoshuka daraja na timu zitakazopanda msimu wa 2019/20.

Tangu Machi 17, serikali ilipositisha shughuli zote za michezo kutokana na dunia kukumbwa na ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona, kulikuwa na tishio la Ligi za Tanzania kufutwa kama ilivyokuwa baadhi ya nchi duniani.

Shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli alipotangaza mara mbili kwa vipindi tofauti, azma yake ya kutaka kufungulia shughuli za michezo na hatimaye mara ya tatu, kutamka rasmi kuruhusu michezo ikiwamo tarehe ambayo ni leo Juni Mosi.

Ina maana kuanzia leo, Watanzania ni ruhusa kujimwaga tena viwanjani kushuhudia kandanda, mchezo ambao mashabiki wengi waliukumbuka mno na kuwa kama wagonjwa.

Nchi ilikuwa kimya na hakukuwa na shamrashamra kama ambavyo huwa inakuwa wakati ligi inaendelea nchini Tanzania, watu kutambiana na kutaniana hapa na pale, ili mradi tu kufanya watu wawe na furaha, faraja na amani.

Sasa ni rasmi tayari kila kitu kimeshafunguliwa, lakini Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo zimeweka utaratibu maalum jinsi gani michezo hiyo ya ligi itafanyika kwa kuzingatia taratibu zote za kiafya.

Kutokana na hali hiyo, wizara zote mbili zimeshaanza kutoa miongozo na bado zitaendelea kutoa mingine ili kufanikisha mambo yote mawili, ligi zichezwe, lakini kurejea kwa michezo hiyo kusilete tena maambukizo mapya ya ugonjwa wa Covid-19.

Kwa maana hiyo mashabiki wote wa soka, wanapaswa kuifuata miongozo hiyo, pamoja na masharti yatakayotolewa na wizara hizo.

Kama itatolewa ruhusa ya baadhi ya mashabiki kuingia na ngoma zao, basi inapaswa iwe hivyo na hata jinsi watakavyokaa majukwaani, basi wafuate taratibu zote za kiafya zilizowekwa na wataalamu.

Kama mwongozo ni kwamba mashabiki waingie uwanjani, lakini kuwe na idadi maalum, basi mashabiki wanapashwa kukaa kwenye viti kwa kuachiana mita moja moja.

Ina maana kuwa shabiki akikaa kiti kimoja, cha pili kinaachwa tupu na mwingine anakaa cha tatu.

Lakini hii kidogo inatakiwa pia iwe kwa msaada wa wanausalama, lakini kuwe na umakini na uangalizi wa hali ya juu kwa wakata tiketi mlangoni, kwani inaweza kushuhudia mashabiki wengine wakiingia kwa njia za panya na uwanja ukajaa kuliko ilivyopangwa kiafya.

Mashabiki pia wanatakiwa wawe wamevaa barakoa kama itatokea wakiruhusiwa kuingia uwanjani.

Kama hali itakuwa ni tofauti, basi mashabiki wanatakiwa waheshimu maagizo ya kutokwenda uwanjani na wala wasianze kutaka kulazimisha kwenda kujazana nje ya uwanja ambao mechi zinachezwa kwa sababu huo pia utakuwa ni mkusanyiko na unaweza pia kusababisha maambukizo.

Kinachotakiwa kwa mashabiki ni kuwa wastaarabu na hii ni kwa ajili ya afya zao, na si Shirikisho la Soka nchini (TFF), Jeshi la Polisi au Serikali.

Hata kwa wale mashabiki watakaokuwa wanaangalia kwenye vibanda umiza, wanatakiwa pia wawe makini maeneo ambayo wanaangalia.

Kwanza wahakikishe muonyeshaji ana vifaa kama maji, dawa na sabuni mlangoni, ili kila mmoja anawe kabla ya kuingia. Pili kila shabiki ahakikishe anaingia humo akiwa amevaa barakoa na hata jinsi ya kukaa, wasikubali kujazana hadi kuegemeana.

Mashabiki hawatakiwi kufanya mambo au vituko ambavyo vitasababisha serikali ighairi na kuchukua hatua nyingine kama vile kusimamisha tena michezo ili kuokoa maisha ya mashabiki ambao wameshindwa kulinda afya zao wenyewe.