Ustawi, polisi jamii wasaidieni wanafunzi wasisote vituoni

18May 2022
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ustawi, polisi jamii wasaidieni wanafunzi wasisote vituoni

WAZAZI na walezi wamekuwa na mwitikio mkubwa wa kuwapeleka shuleni watoto wao, ili wapate elimu bila kujali kuwa wanaposoma ni mbali au karibu.

Pamoja na kuitikia wito huo, watoto kusoma mbali na nyumbani ni sawa kuwapa adhabu hasa wanafunzi wengi wa mijini.

Inapotajwa  adhabu ni kutokana na wanafunzi wengine kusota vituoni wakiwa na njaa na wakati mwingine wakishindwa hata kwenda vyooni kujisaidia kwasababu vyoo ni vya kulipia na wenyewe hawana pesa zaidi ya nauli na kiasi kidogo cha kununua karanga au andazi walichopewa na wazazi au walezi.

Wanafunzi wengi wanaosoma sekondari za kutwa wanateseka kuamka alfajiri na kurejea nyumbani usiku hata wakati mwingine zaidi ya saa 3:00.

Ni kutokana na kukosa magari ya shule au usafiri wa shule na kutegemea daladala. Tatizo ni kubwa kwa watoto wa madarasa ya chini mfano darasa la kwanza.

Watoto hao wadogo wanasota vituoni wakisubiri magari, lakini hawawezi kugombea usafiri huo na matokeo yake wanabakia vituo muda mrefu bila kuwahi shuleni au kurudi nyumbani.

Hatukatai watoto kusoma shule za mbali lakini, ni vyema sasa serikali ikawa na mpango wa kuwasaidia ikibidi polisi jamii au maofisa wa ustawi wa jamii kwenye kata wakashirikiana kuwasaidia kwa kusimamia watoto ili wapandishwe kwenye mabasi wakati wa kwenda shule na kurudi nyumbani.

Wanafunzi wanafikia vituoni saa 11 alfajili wakisubiri usafiri ambao wanalazimika kuugombea na watu wazima. Wazazi, walezi, serikali na wadau wajiulize hali hii itaendelea mpaka lini?

Mtoto au watoto hao ni wadogo muda huo walitakiwa kulala lakini elimu ni ufunguo wa maisha wanatakuwa kuwa darasani.

Kinachotakiwa kutatua suala hili ni wazazi na walezi pamoja na jamii kuanza kushughulikia changamoto hiyo kwa kushirikiana na serikali za mitaa hasa ofisi za kata ili kupata maofisa ustawi watakaoshirikiana na polisi jamii kuwafikisha shule.

 

Inatisha kuona mtoto mdogo unakwama  kituoni na sasa yanaanza kuwa mazoea katika miji mingi ya Tanzania, ndiyo maana ni wakati wa kuchukua hatua.

Ni wazi akifika shule amechoka hawezi kusoma akirudi nyumba amechoka je si kumuadhibu mtoto huyo?

Ni vyema wazazi na jamii kuangalia kuanzia sasa suala hilo hata kama shule haziko mbali bado watoto wanahitaji usalama kulindwa na kuepushwa na hatari na suala la usafiri salama halikwepeki.

Suala la kuwapa watoto usafiri kuenda pamoja na kuwapatia chakula cha mchana ili wanapotoka shuleni wawe na nguvu na kuwapunguzia uchovu na njaa.

Njaa inasababisha watoto kuchoka na kusinzia zaidi katika magari na muda mwingine kondakta anapata tena kazi ya kuwauliza wanashuka wapi ili wawashushe vinginevyo watapitilizwa.

Kuna wazazi au walezi ambao wanaona kuliko kuwaamsha watoto usiku na kukumbana na changamoto za usafiri wanaona ni vyema kuwapeleka watoto wao vijijini wakaishi na babu na bibi zao vijijini na kusoma shule za mbali.

Hii inasadikiwa itampunguzia mtoto usumbufu hasa wa usafiri ndani ya  daladala bila kujua kuwa watoto wanakosa uangalizi na wanaweza kutumbukia kwenye maangamizo hata tabia za kihalifu.

Wazazi na walezi wanatakiwa kuliangalia sana suala la watoto na kuwasaidia kutengeneza na kutegemeza maisha yao.

Wakati huu serikali na Wizara ya Elimu zinapofanya juhudi za kuboresha elimu ni vyema pia wadau wakashirikishwa kutoa moani yao ya namna ya kuboresha elimu kwenye eneo la usafiri hasa kwa wanafunzi wa mijini.