Usugu wa foleni Dar lini utakwisha?

16Mar 2017
Christina Mwakangale
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Usugu wa foleni Dar lini utakwisha?

Foleni za magari katika jiji la Dar es Salaam si jambo geni. Usugu wake unaendelea kuongezeka siku hadi siku hata kuwa sehemu ya maisha ya wakazi wa jiji siku hadi siku.

Licha ya juhudi za serikali katika kupunguza kero hiyo, ikiwamo kuanzisha mradi wa mabasi yaendayo haraka Dar es Salaam (Dart), kujenga na kuziboresha barabara mbadala za ndani katika maeneo tofauti jijini ili kuzipunguzia wingi magari yanayotumia barabara kuu.

Naipongeza serikali kwa juhudi inazozifanya, lakini mtazamo au msisitizo wa kutatua foleni jijini nashauri ni muhimu kuzingatia hali halisi iliyopo katika makutano ya barabara na kusababisha tatizo kuwa kubwa zaidi katika maeneo mengineyo ya barabara.

Katika makutano yenye taa za kuongozea magari, ikiwamo Ubungo, Tazara, Moroco, Mwenge, Ilala Boma, njia panda ya kuelekea Keko jirani na Veta na kwingineko ni miongoni mwa maeneo sugu kwa foleni.

Askari wa usalama barabarani yaani trafiki ni lazima wahakikishe kuwa wanakuwapo katika maeneo hayo ili kutoa muongozo stahili licha ya kuwapo taa hizo.

Kwa mtazamo wangu, maeneo haya yangeweza kupanuliwa ni kurahisisha magari yaendayo uelekeo wa pembeni kupita na kupishana kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani.

Pia barabara za juu 'fly over' zenye urefu wa kilomita chache ili kurahisisha magari yanayopishana maeneo hayo yapite kwa urahisi na kufanikisha kuondoa foleni sugu katika barabara zetu.

Tatizo ambalo nimelishuhudia binafsi ni katika kupeana nafasi ya kila mtu kuelekea aendako, eneo la Ubungo na Tazara mataa yanaongoza kwa kuanzisha foleni hususan majira ya asubuhi na jioni.

Ni jambo la kawaida, kusimama kwa muda wa saa tatu hadi nne katika makutano ya barabara ni jambo la kawaida na wanaopatwa na adha zaidi ni watumiaji wa usafiri wa umma, kutokana na hali ya joto na mbanano kupindukia ndani ya vyombo hivyo.

Katika maeneo haya, kuna ujenzi wa majengo yaliyo karibu na barabara kinyume cha sheria hata kusababisha adha zisizo za lazima.

Tofauti na miaka ya nyuma linaendelea kukua na matumizi ya barabara kuongezeka kutokana na ongezeko la magari na pikipiki ni usafiri wa umma. Ufanyike utaratibu angalau wa kuzipanua barabara katika makutano ili kupunguza usugu wa foleni katika maeneo haya jambo ambalo linawezekana.

Ni matumaini yangu, mamlaka husika za ujenzi wa barabara ndani ya miji ziangalie mikakati ya muda mfupi ili kupunguza foleni kwenye makutano. Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kuhakikisha zinawekewa lami ili kupunguza foleni kwa asilimia kubwa.