Utafiti wa tiba ya corona, usisahau watoto mitaani

14May 2020
Maulid Mmbaga
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Utafiti wa tiba ya corona, usisahau watoto mitaani

KUTOKANA na mlipuko wa ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (Covid -19), zinahitajika jitihada madhubuti katika kuwaokoa watoto wa mitaani dhidi ya maambukizo ya maradhi hayo.

Tanzania ni nchi ambayo katika baadhi ya miji yake mikubwa kama Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na Tanga, kuna watoto wanaonekana kuzagaa mitaani na inaelezwa kuwa hawana makazi maalumu.

Ni hali inayoelezwa, inaweza kuhatarisha afya zao, katika kipindi hicho janga la corona litakapotokea kuwafikia.

Wataalamu wa Afya walieleza kuwa, corona unaambukizwa kwa njia ya kugusana au kutumia barakoa iliyotumiwa na mtu mwenye maambukizo.

Serikali inalazimika kuwashauri wananchi kuepuka mazingira rafiki kwa maambukizo, ikiwamo kwenye misongamano ya watu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto iliyotolewa wiki mbili zilizopita - Aprili 29, idadi ya wagonjwa wa corona nchini ilifikia 480, vifo 16, waliopona na kuruhusiwa 167, na maambukizi mapya 196.

Aidha, katika sura ya kitaifa ilipata nyongeza, kwa Zanzibar kutangaza ongezeko la wagonjwa 29.

Hapo ndipo tunaona hali isiyoridhisha, nini kifanyike kuwalinda watoto hao?

Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ina wajibu wa kuweka taratibu maalumu za kuwasaidia watoto wa mitaani, kuwazuia wasizagae, kwa kuwapatia hifadhi maalumu, ili kuwakinga dhidi ya maambukizo ya virusi vya corona.

Pia, watoto ambao kila mara wanaonekana barabarani wakiwa wanaomba pesa na hata kujihusisha na usafishaji wa vioo vya magari katika maeneo ya mijini, hayo maisha yao ya mitaani wanapaswa kuwa na vitakasa mikono na wasiokuwa na uwezo wa kununua, ili iwasaidia kujikinga na corona.

Kwa upande wa wazazi na walezi, nao wanapaswa wajitahidi kuwa karibu na watoto hasa kipindi hicho wasiwaruhusu kuzurura mitaani pasipo na sababu maalumu, ili kulinda afya zao, kwani hawana uelewa mkubwa kuhusu corona.

Wakati nchi mbalimbali duniani zikielekeza nguvu kubwa kutafiti dawa ya kutibu corona, Madagascar imeshatangaza hatua, imepata dawa mitishamba yenye uwezo wa kupumbaza virusi hivyo, huku Taasisi ya Taifa Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu nchini (NIMR0)sasa ikizifanyia kazi.

Dawa hiyo inahusishwa na mmea wa Kichina unaoitwa Artemisia (pakanga) ambayo ni mojawapo inayochanganywa na mingine, ikitibu malaria.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ilisema Waziri wa Mambo ya Nje wa Madagascar, Tehindrazanarivelo Djacoba, alizitaka nchi za Kiafrika kuungana kupata suluhisho la maradhi ya Covid-19, itakayokuwa faraja kwa dunia zima.

Pia, Madagascar inaeleza furaha ya kuupatia ufumbuzi ugonjwa huo kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), akijionea dawa halisi kwa imani kukiwapo nguvu ya pamoja ndani ya Umoja wa Afrika (AU), kutakuwapo hatua.

AU ilifanya mazungumzo na Madagascar kupata viashiria muhimu za kiufundi kuhusu usalama na ufanisi wa dawa ya mitishamba iliyokwishatangazwa.

Umoja huo kupitia kituo chake cha udhibiti wa magonjwa (Africa CDC), ulisema unaendelea kutathimini data zilizokusanywa kuhusu usalama na ufanisi katika tiba hizo asili dhidi ya virusi vya corona.

Kimsingi, Africa CDC ni taasisi ya AU inayozisaidia nchi wanachama kuimarisha mifumo ya afya na kuboresha uchunguzi, kuzuia, kudhibiti na kukabiliana na dharura za magonjwa.

Hata hivyo, AU imesema tathimini yake inayoendelea kufanyika, pia itazingatia maadili ya kiufundi katika kukusanya ushahidi muhimu wa kisayansi wa ufanisi wa mitishamba husika.

Ni hatua baada ya Rais wa Madagascar, Andry Rajoelina, hivi karibuni ambapo aliwafahamisha viongozi wenzake wa AU kuhusu dawa ya mitishamba anayoamini inazuia na kutibu virusi vya corona.

Shirika la Afya Duniani (WHO), katika majibu yake lilisema ni muhimu kila dawa zinazodaiwa kuwa na uwezo wa kutibu virusi vya corona, zifanyiwe majaribio na uchunguzi wa kina, kabla hazijaanza kutumika na lilitahadharisha, huenda watu wanatjea imani na dawea ambazo hazijafanyiwa majaribio, pindi watakapopata nafuu.