Utajuaje mume au mke uliye naye ni sahihi?

15May 2016
Flora Wingia
Nipashe Jumapili
Maisha Ndivyo Yalivyo
Utajuaje mume au mke uliye naye ni sahihi?

MPENZi msomaji, tunaendelea na mada yetu kuhusu nini maana ya ndoa. Wiki iliyopita tulijifunza kwamba ndoa zilizofanikiwa zilianza na matatizo makubwa! Leo hebu nijikite katika swali hili; kwamba utajuaje huyu mwanaume/mwanamke uliye naye ni sahihi?

Kabla ya yote tutafakari andiko hili kuhusu uumbaji wa Mungu katika biblia Takatifu, Mwanzo 2:21-23, imeandikwa; “BWANA Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akaufunika nyama mahali pake, na ule ubavu aliutwaa katika Adamu BWANA Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu.

Adamu akasema, sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume”.

Andiko hili na mengine yenye dhana inayofanana na hiyo, yanatupatia ufunuo muhimu sana, kwamba ndoa haijatokana na mawazo ya mwanadamu. Mungu ni mchoraji, mjenzi na anajenga nyumba na siku zote anayo mipango mizuri juu ya ndoa. Siku zote huwaunganisha watu wawili katika ndoa kwa makusudi.

Mungu siku zote ana akili sana, na sanifu inapokuja kwenye suala la ndoa na huwaunganisha watu kwa kutumia hesabu za kiungu. Yeye anafahamu ni mwanamke yupi au ni mwanaume yupi anaweza kukuunganisha naye ili akamilishe kusudi alilopanga juu ya maisha yako.

Kama ni mwanamke unatakiwa kujua kuwa, kuna ubavu wa mwanaume uliotumika kukuumba. Kama ni mwanaume ni muhimu utambue kuwa ubavu wako ulitumika kumuumba mwanamke, na mara Mungu anaporuhusu muoane, ni lazima mtaoana.

Lakini swali la msingi linakuja; Je, Nitamtambuaje kuwa mume/mke huyu ni yule niliyepewa na Mungu? Ni swali ambalo wewe mwenyewe unaweza kujibu. Mafanikio yako kwenye ndoa yanategemeana na wewe mwenyewe.

Ukweli ni kwamba hatma ya maisha yako inategemeana na aina ya mwenzio uliye naye. Msaidizi wako wa karibu ni mwenzi wako, anasema mtumishi wa Mungu Nabii, B. G.Malisa mwanzilishi wa Kanisa la Ukombozi Church of All Nations, kwenye kitabu chake kiitwacho ‘Mwanamke Jitambue’. Kanisa hili lenye makao makuu Mwanza, lina makanisa mikoa mbalimbali nchini.

Mpenzi msomaji yatupasa kujua kuwa ndoa ni muunganiko mkubwa na wenye nguvu kuzidi hata familia yako. Na yapo madhara makubwa ya kuoa/olewa na mtu asiye sahihi. Ni hatari sana kuchagua ubavu mbovu. Mara tu unapofunga ndoa na mtu asiye sahihi, hatma yako yote inaathiriwa.

Shetani ni mjanja sana. Anafahamu uwezo uliopo katika ndoa zenye mafanikio. Na anajua ndoa zilizofanikiwa zinasababisha madhara makubwa sana katika ufalme wake. Na ili ujue shetani ni adui yako wa kwanza wa ndoa yako, anafanya juu chini kuiangamiza.

Jiulize; kwanini ndoa nyingi leo zimevunjika? Kwanini wanandoa wengi sana leo wanaandikiana talaka? Kwanini watu wengi waliookoka wanapambana sana katika eneo la ndoa bila mafanikio?

Jibu ni moja tu, kwamba msingi wa ndoa unakuwa umeshaharibiwa na shetani. Kama unatamani kuwa na nyumba yenye mafanikio, ni lazima uzingatie kuweka msingi mzuri. Ni muhimu uangalie msingi wa ndoa yako. Ukianza kwa kujenga msingi mzuri, utamaliza vizuri.

Kama msingi ni imara, hata kama dhoruba itakupitia, bado jengo litaendelea kusimama kwani limejengwa katika mwamba imara.

Mpenzi msomaji, bila shaka umeelimika kuhusu sababu za ndoa nyingi kupata misukosuko. Lakini ujue kwamba misukosuko hiyo haitokei kwa bahati mbaya bali kipo chanzo/vyanzo ambavyo vimesababisha hali hizo kutokea.

Niishie hapa. Wiki iliyopita niliahidi kwamba wiki hii ningeanza kuchambua vyanzo vya matatizo ya ndoa. Lakini niliona nitangulize mada hii ili mtiririko uwe mzuri zaidi. Kwa hiyo nitakwenda kutaja chanzo kimoja baada ya kingine kama ambavyo Nabii B.G.Malisa wa Kanisa la Ukombozi alivyotolea uchambuzi.

Wakati tunasubiri kujua vyanzo hivyo, hebu nikuulize msomaji wangu; Je, ndoa yako iko salama? Njoo Kanisa la Ukombozi lililoko eneo la Skanska, Tegeta DSM ufunguliwe kujua chanzo cha tatizo lako.

Pia ukiwa nalo jambo kuwa huru kuwasiliana nami kwa ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 0715268581 (usipige), au barua pepe; [email protected] au [email protected]