Utapeli mpya wa simu; mzazi au mtoto amezidiwa shuleni

23Jul 2020
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Utapeli mpya wa simu; mzazi au mtoto amezidiwa shuleni

HADI sasa kuna maendeleo makubwa katika manufaa yatokanayo na matumizi ya simu nchini, tukiungana na dunia ilivyo.

Pia, kuna sura nyingine ambayo ni mbaya, kuwapo matukio ya utapeli kupitia mitandao ya simu inayoendelea katika maeneo mbalimbali, watu kuibiwa pesa, wanaporubuniwa kupitia mifumo yao hiyo ya kimtandao.

Mtindo wanaotumia matapeli hao ni matumizi ya ujumbe mfupi wa simu wakijaribu kumrubuni mtu anayefanya biashara na hata kutoa wazo la kunufaika kiuchumi.

Watu mara nyingi wanaangukia kurubunika, hasa kutokana na uhalisia wa hali duni ya kiuchumi, hata kuhamasika huenda akajinusuru kiuchumi walau aambulie pesa kwa namna yoyote.

Pia, kuna mbinu ya pili ya hadaa kutoka kwa matapeli wanaowaeleza wenye simu hoja zisizo na ukweli, lakini zinafanana kwa karibu na uhalisia wa maisha ya mpokeaji, hata akatekwa kihisia akiamini kuwapo ukweli, kumbe anaangukia mikono ya mdanganyifu.

Hapo ndipo mpokeaji anapohangaika kuhudumia matakwa ya uongo, akidhani kuna la ukweli anaouhangaikia, kumbe yuko katika mawasiliano potofu. Ni baada ya muda mfupi tu utapeli unapokamilika, simu ya mpigaji inazimwa.

Sasa kuna lingine walilolibuni inalotawala sasa, matapeli wameanzisha njia nyingine za kumpigia mtu simu na kumhusisha mtu na lililo karibu zaidi, mathalani kuwapo dharura inayomhusu mzazi au mtoto wa mwenye simu.

Hapo wanasimama katika nafasi ya usamaria, wakidai wamewajibika kutumia pesa nyingi na wanahitaji kurejeshewa gharama walizoingia kutumikia dharura hiyo ya nusura, kama vile ugonjwa.

Ni aina ya taarifa inafikishwa katika hisia zenye simanzi baada ya kujitambulisha. Hicho ndicho kinachotokea kwenye shule mbalimbali sasa.

Mzazi anapigiwa simu kwamba mtoto wake ana hali mbaya ya dharura ya ugonjwa na hivyo huyo ‘mwalimu’ anayepiga simu, anajitambulisha kwamba wameshaingia gharama wanazohitaji kurudishiwa.

Ni hatua ambayo ama mzazi au mlezi anapowehuka na huangukia kutoa pesa kulipa pasipo kujitambua, akidhani anatatua tatizo, kumbe anawatatulia matapeli shida zao kwa mtaji wao wa hadaa.

Kuna mkasa wa ushahidi mzazi mmoja wa kike alipigiwa simu na hata katika utambulisho akahojiwa jina lake kwanza na kisha kuelezwa tatizo.

Hapo alifahamishwa kuwa wao ni walimu wako katika hospitali kubwa ya serikali jirani, wakiwa na mtoto aliyeanguka alipokuwa katika choo cha shule na ameumia anavuja damu nyingi mdomoni na puania, wakati huo anaendelea kupata matibabu.

Katika maswali yao ya awali, walimhoji kama mtoto ana kadi ya bima ya afya, kwani wao ‘walimu’ walipekua begi lake na hawajaona kadi. Mzazi aliwajibu ‘hana.’

Hapo ndipo wakaja na hitaji watumiwe pesa za awali walizotumia ‘walimu wasamaria’ hao kiasi cha Sh. 30,000 na zingine zaidi kuendeleza matibabu.

Mzazi alitia shaka na kuomba akate simu muda mfupi kuweka mambo sawa, ili awatumie pesa na kisha angewapigia tena baada ya muda mfupi.

Ni hatua ambayo mzazi aliwasiliana na shule moja kwa moja, alikohakikishiwa kwamba mtoto yuko salama na anaendelea na masomo darasani.

Ufafanuzi wa ziada aliopata mzazi ni kwamba siyo tukio la hadaa ya kwanza shuleni, kuna wazazi wenzake wengi tu walishapotoshwa na matapeli kwa staili hiyo.

Baada ya mawasiliano hayo, mzazi alipiga tena simu kuwadadisi na matapeli walipobaini mzazi ni mjanja, kama ilivyo mtindo wao wa kuagana wanapogundua anayetakiwa kutapeliwa ameshtukia njama, walimtukana matusi mazito na kisha wakazima simu.

Haijaeleweka kama ndio mtindo wa makubaliano yao ya kihalifu, lakini ndio mtindo mara zote wanaaga pindi wanapogundulika kwa ‘mabomu’ ya matusi ya nguoni, ikifuata kuzima simu.